Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi akizungumza wakati wa Mkutano wa Bodi za Mashirika na Mifuko ya Umoja wa Mataifa siku ya jumatatu, ambapo pamoja na mambo mengine ameutaka Umoja wa Mataifa kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia misingi iliyojiwekea na pia kutowapa nafasi watendaji wenye ushabiki na wanaoweka mbele maslahi binafsi. Walioketi nyuma ni Maafisa wa Uwakilishi Bw. S. Shilla na Bi, Lilian Mkasa
Na Mwandishi Maalum, New York
Wakati Tanzania ikipongeza, kusifu na kushukuru uhusiano na ushirikiano wake na Umoja wa Mataifa kupitia Mifuko na Mashirika yake ya Maendeleo, imeutaka pia Umoja huo kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia, kanuni, taratibu, sheria na misingi iliyojiwekea ili iendelee kujijenga heshima.
Hayo yameelezwa jana jumatatu na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi, wakati wa mkutano wa Bodi za Mashirika ya Umoja wa Mataifa UNDP, UNFPA na UNOPS. Tanzania ni mjumbe wa Bodi katika Mashirika hayo.
Katika siku ya kwanza ya mkutano , mkutano uliofunguliwa na Mtendaji Mkuu wa UNDP, Bi Helen Clark, Balozi Manongi amesisitiza kwamba, ili Umoja wa Mataifa uendelee kujijenga heshima na kuheshimika, unapashwa kutoruhusu watendaji wenye ajenda na maslahi binafsi kufanya kazi katika Mashirika ya Umoja wa Mataifa.
“ Umoja wa Mataifa wakati wote umekuwa sehemu na mdau mkubwa katika uimarishaji na ujenzi wa utawala bora katika nchi nyingi , Tanzania ikiwamo. Wajibu wa Umoja wa Mataifa utabaki kuwa halali na wenye nguvu endapo wale ambao wamepewa dhamana ya kutenda kwa niaba yake watatambua na kuheshimu imani na wajibu uliotukuka ambao wamepwa kuutekeleza ” akasisitiza Balozi Manongi
Akaongeza kwamba, mashabiki hawapaswi kupewa nafasi, wala kuvumiliwa na kuwa sehemu ya miongoni mwa watendaji wa chombo hicho wasipewe nafasi, wala wasivumiliwe kuwa miongoni mwa watendaji wa chombo hicho.
Akizungumzia kuhusu rasimu ya Taarifa ya Mpango wa Utekelezaji kuhusu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Country report) kwa kipindi cha 2016-2021) ambayo imewasilishwa mbele ya Wajumbe wa Bodi wa UNDP, Balozi Manongi amesema, mapendekezo yaliyomo kwenye rasimu na ambayo imeshirikisha wadau mbalimbali inajumuisha mawazo na mapendekezo kutoka pande zote za Muungano na imetokana na misingi ya ushirikiano kati ya UNDP na Serikali ya Tanzania.
Vile vile akasema rasimu hiyo imejumuisha vipaumbele vinavyoainishwa katika Dira ya Taifa ya 2025 kwa upande wa Tanzania Bara , Dira ya 2020 kwa upande wa Zanzibar, mkakati wa kupunguza umaskini kwa pande zote za Muungano pamoja na Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano.
“ Tunaishukuru UNDP- Ofisi ya Tanzania kwa ushirikiano wake katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo ikiwano mikakati ya kupunguza umaskini, ushirikiano huu umekuwa mzuri ingawa unachangamoto zake” akasisitiza Balozi Manongi
Akaeleza kwamba, kutokana na umuhimu wa mwaka huu wa 2016 ambao pamoja na mambo mengine ni kuanza kwa utekelezaji wa Agenda ya Maendeleo Endelevu ( Agenda 2030) Tanzania itaendelea kushirikiana kwa karibu na UNDP katika utekelezaji wa Agenda hiyo huku mkazo ukiwa ni katika kupungua ama kuondoa umaskini uliokithiri kwa makundi ya mbalimbali ya jamii hususani wanawake.
Akasema , Serikali imejipanga vema katika utekelezaji wa mipango mbalimbali inayolenga katika kuboresha maisha ya wananchi wake. Ikiwa ni pamoja na kutatua tatizo la uhamaji wa wananchi wake kutoka vijijini na kwenda katika miji mikuu hususani vijana kwa lengo la kutafuta ajira na hali bora ya maisha.
Akasema kuwa wajibu au madhumuni ya msingi UNDP ni kupunguza umaskini, ni kwa sababu hiyo Tanzania ingependa kuiona UNDP ikijielekeza zaidi katika jukumu lake hilo la msingi kama inavyoelekezwa katika maazimio mbalimbali ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Kwa upande wa ukusanyaji na uchambuzi wa takwimu zinazohusu maeneo mbalimbali, Balozi Manongi amesisitiza kwamba UNDP inapashwa kufanya kazi kwa karibu na kwa ushirikiano na Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa kile alichosema ndicho chombo cha serikali chenye dhamana juu ya masuala yote yahusuyo takwimu.
Na kwa sababu hiyo akasema Tanzania inaridhishwa na taarifa ya kwamba UNDP itashirikiana na Ofisi hiyo ya Taifa ya Takwimu katika Nyanja mbalimbali zikiwamo za uwezeshaji kwa lengo la kusaidia katika uhuishaji wa takwimu.Aidha Tanzania imesisitiza kuhusu umiliki katika uendeshaji na usimamizi wa miradi ya maendeleo pamoja na kiushauri UNDP kuhakikisha kwamba fedha zinazotengwa kwaajili ya miradi ya maendeleo zinakwenda kufanya kazi iliyokusudiwa na si vinginevyo.
No comments:
Post a Comment