ANGALIA LIVE NEWS

Monday, January 4, 2016

Wakuu 15 shule za wazazi matatani

Mwenyeki wa JumuiyayaWazazi ya CCM, Abdallah
By James Magai na Raymond Kaminyoge

Dar es Salaam. Wakuu wa shule 15 zinazomilikiwa na Jumuiya ya Wazazi ya CCM, wako hatarini kuburuzwa mahakamani kutokana na tuhuma za ubadhirifu.

Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Abdallah Bulembo alisema jana kuwa kamati ya utekelezaji iliamua shule hizo zikaguliwe na baada ya ukaguzi walibaini ubadhirifu huo.

Alisema tayari wakuu wa shule tatu za sekondari za Tegeta, Tabata na Mwembetogwa wako mahakamani kwa ubadhirifu.

Mbali na hao alisema kuwa katika ukaguzi uliofanyika katika shule nyingine, 15 ziko hoi kutokana na vitendo hivyo vya ubadhirifu.

“Shule 15 ni hohehahe, wale watu hawezi kupona, wataelekea mahakamani,” alisema Bulembo.

Alisema matatizo waliyoyabaini katika ukaguzi huo ni upotevu wa pesa huku akitoa mfano kuwa unaweza kuikuta shule ina watoto 1,000 na mkuu wa shule kwa mwaka amenunua magunia 1,000 ya mchele, magunia 1,000 ya mahindi, yaani kilo 10,000.

Alisema kuwa pamoja na ubadhirifu huo, kuna watu wanatafuta kichaka cha kutengenezea ule ubadhirifu wao, huku akiwataka viongozi wenzake wanaoonekana kuwatetea watuhumiwa, kuachana na suala hilo.

“Suala la kusema tunampenda sana mwalimu halipo. Unaweza ukampenda sana lakini akawa mwizi sana na sisi hatuwezi kustahimili,” alisema Bulembo.

Akizungumzia maendeleo ya shule za wazazi, Bulembo alisema kuwa katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wake tangu ameingia madarakani wametoa mwanafunzi mmoja katika wanafunzi 10 bora na shule moja ya sekondari kuingia katika orodha ya shule tano bora nchini.

Alisema kwa sasa wanataka kwenda kwenye vyuo zaidi kuliko kubaki kwenye elimu ya sekondari, na kwamba vyuo hivyo vitakuwa kwenye maeneo ambako kulikuwa na shule.

“Lakini sasa tumeanzisha chuo cha Jumuiya ya Wazazi Kaole pale tayari kimeshaanza, Nacte wameshakisajili na watoto wameshaanza. Kuna shule yetu moja kule Tarakea tunaanzisha chuo cha ualimu,” alisema.

Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mnakongo, iliyoko wilayani Kongwa, Rukonge Mwero alisema wajumbe wa bodi za shule wamekuwa wakichangia ubadhirifu.

“Wakuu wa shule wanaweza kufikishwa mahakamani lakini hatua za kinidhamu zinatakiwa kuchukuliwa pia kwa viongozi wa bodi za shule,” alisema.

No comments: