Monday, January 4, 2016

Yanga moto mkali Zenj


Donald Ngoma alifunga mara mbili, huku mtokea benchi Paul Nonga akiongeza jingine na kuihakikishia Yanga ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Mafunzo FC katika mechi yao ya kwanza ya Kundi B la Kombe la Mapinduzi visiwani hapa jana.

Kikosi cha Yanga ambacho jana kilimkosa beki wake wa pembeni, Hajji Mwinyi huku kikiendelea pia kukosa huduma ya nahodha wake Nadir Haroub 'Cannavaro', kililazimika kusubiri hadi dakika ya 31 kuandika bao la kwanza la mashindano hayo mwaka huu lililofungwa na Ngoma.

Mshambuliaji huyo wa kimataifa kutoka Zimbabwe, alimalizia kwa shuti la mguu wa kulia ndani ya boksi pasi ya kiungo Mzimbawe mwenzake Thaban Kamusoko aliyemlamba chenga beki wa pembeni kushoto, Hassan Juma kabla ya kupenyeza mpira wa kutambaa kwa mfungaji.

Ngoma alirejea tena nyavuni dakika tatu baadaye, safari akikokota mpira ndani ya boksi baada ya kupewa pasi rula na Kamusoko aliyekuwa katikati ya uwanja na kuzifanya timu hizo kwenda mapumziko, huku Yanga ikiwa mbele kwa mabao 2-0.

Mafunzo FC inayonolewa na Hemed Morocco ilionekana kucheza kwa nguvu zaidi kipindi cha pili, lakini ikaangusha na washambuliaji wake ambao hawakuwa makini katika kumalizia nafasi walizozipata ikiwamo penalti ya dakika ya 81 ya Kheri Salum iliyopanguliwa na kipa Deogratius Munishi 'Dida'.
Mwamuzi mwenye Beji ya FIFA, Mfaume Ally Nassoro, aliamuru tuta hilo kutokana na Kelvin Yondani kumdondosha ndani ya boksi Shaban Ally aliyewalamba chenga ya fedheha beki huyo wa kati wa Yanga na beki wa pembeni Juma Abdul.

Straika aliyeifungia magoli matano Mwadui FC msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara kabla ya kutua Yanga, Paul Nonga alitokea benchi katika dakika ya 88 akipishwa na Amissi, aliipatia Yanga bao la tatu dakika mbili baadaye akimaliza kwa shuti 'mtoto' mpira wa krosi ya mguu wa kulia ya kiungo mtokea benchi mwenzake, Geofrey Mwashiuya kutoka wingi ya kushoto kusini mashariki mwa Uwanja wa Amaan.

Yanga ambayo mwaka jana iling'olewa hatua ya robo-fainali baada ya kukubakli kipigo cha bao 1-0 dhidi ya JKU FC (bao la mshambuliaji wa sasa wa JKT Ruvu, Amour Omary Janja), itacheza mechi yake ya pili ya Kundi B dhidi ya mabingwa mara mbili wa Kombe la Mapinduzi, Azam FC kesho.
Vikosi vilikuwa:

Deogratius Munishi, Juma Abdul, Oscar Joshua, Pato Ngonyani, Kelvin Yondani, Mbuyu Twite, Simon Msuva/ Malimi Busungu (dk 88), Thaban Kamusoko/ Sina Jerome (dk 70), Donald Ngoma, Amissi Tambwe/ Paul Nonga (dk 88) na Deus Kaseke/ Geofrey Mwashiuya (dk 70).

Mafunzo: Khalid Mahadhi, Juma Mmanga, Samih Nuhu/ Hajji Ramadhani, Kheri Salum, Hassan Juma/ Hajji Hassan (dk 67), Abdul Hassan, Ali Juma/ Jermaine Seif (72), Sadick Habib/ Shaban Ali (dk 58), Mohamed Rahim/ Ahmed Maulid (dk 89) na Ally Mmanga.
CHANZO: NIPASHE

No comments: