ANGALIA LIVE NEWS

Monday, January 4, 2016

KARIMJEE YAKABIDHI SCHOLARSHIP KWA WASHINDI WA SAYANSI 2015, WAPAA KWENDA IRELAND


Wanafunzi John Method (kushoto) na Edwin Luguku (wa pili kulia) kutoka Shule ya Sekondari Mzumbe mkoani Morogoro wakipokea hati zao za ufadhili kutoka kwa Karimjee na Ofisa Ubalozi wa Ireland nchini, Bi. Carlo. Wanafunzi hao waliibuka washindi wa jumla katika maonesho ya Sayansi kwa Shule za Sekondari mwaka 2015 yanayoandaliwa na taasisi ya Young Scientists Tanzania (YST). (Picha zote na Daniel Mbega wa www.brotherdanny.com).

Ofisa Ubalozi wa Ireland nchini, Bi. Carlo, akizungumza na Edwin Luguku na John Method kutoka Shule ya Sekondari Mzumbe, Morogoro ambao waliibuka washindi wa jumla katika maonesho ya Sayansi kwa Shule za Sekondari mwaka 2015 yanayoandaliwa na taasisi ya Young Scientists Tanzania (YST). Wanafunzi hao wanaondoka leo hii kwenda Dublin, Ireland kwa maonesho ya sayansi.

Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Young Scientists Tanzania (YST), Dk. Gozibert Kamugisha, akizungumza wakati wa kukabidhiwa kwa scholarship kwa wanafunzi Edwin Luguku na John Thomas wa Shule ya Sekondari Mzumbe ambao walikuwa washindi wa jumla katika maonesho ya sayansi 2015. Wanafunzi hao walipewa scholarship hizo la taasisi ya Karimjee Jivanjee Foundation ya jijini Dar es Salaam.
Meneja wa taasisi ya Karimjee Jivanjee Foundation, Devota Rubama, akizungumza kabla ya kukabidhi hati za ufadhili kwa wanafunzi Edwin Luguku na John Thomas wa Shule ya Sekondari Mzumbe, Morogoro walioshinda katika maonesho ya sayansi 2015.
Mzee Karimjee, Mwenyekiti wa Taasisi ya Karimjee Jivanjee Foundation.

Toyota Tanzania Limited nao waliwazawadia vijana hao kwa ushindi walioupata.

Na Daniel Mbega wa brotherdanny.com
TAASISI ya Karimjee Jivanjee Foundation ya jijini Dar es Salaam leo hii imekabidhi scholarship kwa wanafunzi wawili wa Shule ya Sekondari Mzumbe, Morogoro, ambao waliibuka washindi wa jumla katika Maonesho ya Tano ya Sayansi ya YST kwa Shule za Sekondari Tanzania Agosti 2015.
Wanafunzi hao, Edwin Luguku na John Method, ambao leo hii wanakwenda jijini Dublin, Ireland kuhudhuria Maonesho ya 53 ya Sayansi, waliibuka washindi kutokana na utafiti wao wa sayansi usemao “Madhara ya Matumizi ya Mifuko ya Plastiki Tanzania na Namna ya Kupunguza Matumizi hayo” (The Effects of Using Plastic Bags in Tanzania and How to Reduce the Same).
Kutokana na udhamini huo, wanafunzi hao wawili ambao wanatarajia kumaliza kidato cha sita mwaka huu, watasomeshwa na taasisi hiyo chuo kikuu huku wakilipiwa ada pamoja na gharama nyingine zote kwa miaka yote watakayokuwa wanachukua shahada zao.
Itakumbukwa kwamba, Taasisi ya Karimjee Jivanjee mbali ya kutoa scholarship kwa wanafunzi hao, pia ilitoa ufadhili kwa shahada ya kwanza chuo kikuu kwa wanafunzi Petro Samson Ndegeleki na Juma Joshua Wiliam kutoka Nassa Sekondari ya Simiyu ambao utafiti wao ulihusu ‘How Different Natural Fertilizers Affect the Growth Of Maize’.
Washindi hao pia wanaondoka leo hii kwenda Dublin, Ireland kuhudhuria maonesho ya sayansi ya 53 maarufu kama BT YSTE.
Aidha, taasisi hiyo, ambayo ilianza kudhamini maonesho hayo tangu mwaka 2012, pia iliwazawadia washindi wa pili wa jumla ambao ni Emmanuel Lemalali na Emmanuel Sanga kutoka Tanga Technical na utafiti wao wa ‘A Simple Method For Controlling Ecto-parasites’.
Meneja wa taasisi hiyo, Devota Rubama, amesema kwamba taasisi hiyo imejikita katika kusaidia huduma za kijamii hususan elimu, ambapo kwa mwaka 2015 ilitenga kiasi cha Shs. 1 bilioni huku akiahidi kwamba, kwa mwaka 2016 wametenda Shs. 1.5 bilioni.
“Tumedhamiria kuwahamasisha wanasayansi chipukizi wa Tanzania ili kukuza vipaji vyao ili kulisaidia taifa,” alisema.
Akaongeza: “Tangu mwaka 2015 hadi sasa tumetoa ufadhili kwa wanafunzi 15 ambao walikuwa washindi wa jumla na kila mwaka hutoa ufadhili kwa wanafunzi wanne wanaoshinda katika maonesho ya YST. Wanafunzi walionufaika na ufadhili huo ni watatu kutoka Kibosho Sekondari (2012), wawili kutoka Ilongelo Sekondari, Singida na wawili kutoka Fidel Castro, Pemba (2013), wawili kutoka Lumumba Sekondari, Unguja na wawili kutoka Ngongo Sekondari, Lindi (2014) na sasa tunatoa kwa wawili kutoka Mzumbe na wawili Nasa, Simiyu walioshinda mwaka 2015.”
Rubama alisema kwamba taasisi yake ina mpango wa kuanzisha ufadhili wa shahada ya uzamili kuhusu Uhifadhi Afrika (African Conservation) katika Chuo Kikuu cha Glasgow, Scotland na Chuo Kikuu cha Nelson Mandela, Arusha ambapo wanufaika watakuwa watatu kila mwaka ambao watasoma mihula miwili Glasgow na mihula nane watamalizia Chuo Kikuu cha Nelson Mandela.
“Taasisi imekwishaanza kutoa ufadhili kwa shahada ya uzamili ya udaktari kuhusu Paediatric Oncology katika Chuo Kikuu cha Muhimbili ambapo madaktari wawili walihitimu mwaka 2015 na mwingine atapatiwa ufadhili mwaka 2016.
Katika maonesho hayo ya 5 yaliyoandaliwa na taasisi ya Young Scientists Tanzania (YST) kwa mwaka 2015 yalishirikisha jumla ya shule 240 na walimu 120 kutoka shule 120 nchini kote ambapo zawadi mbalimbali zilitolewa kwa washindi zikiwemo fedha taslimu, medali, vikombe, vifaa vya maabara pamoja na maktaba.
Dk. Gozibert Kamugisha, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji na Mwanzilishi Mwenza wa YST, ameishukuru taasisi hiyo pamoja na Serikali ya Ireland kupitia Shirika la Kimataifa la Misaada la Irish Aid na kuomba wadau wengine wajitokeze kufadhili maonesho hayo.


 (Imeandaliwa na www.brotherdanny.com)

No comments: