Pamoja na mawaziri wa tano wa Rais John Magufuli kuwasilisha fomu za tamko la rasilimali na madeni na kiapo cha uadilifu kukwepa kihunzi cha kutumbuliwa majipu na bosi wao, vigogo hao wanabanwa na adhabu saba kwa kuvunja Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma namba 13 ya mwaka 1995, ikiwamo kushushwa cheo au kusimamishwa kazi.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliwaambia wanahabari jijini hapa jana kuwa viongozi wa umma wanaoshindwa kuwasilisha fomu hizo ndani ya siku 30 zinazotakiwa kisheria, hutakiwa kutoa maelezo na iwapo hayataridhisha mamlaka husika huchukua hatua za kinidhamu.
Kifungu 9(1)(b) cha sheria hiyo kinawataka viongozi wa umma kuwasilisha matamko yao ndani ya siku 30.
Majaliwa aliwataja mawaziri waliozidisha muda huo na kushindwa kuwasilisha fomu hizo kwa wakati kuwa ni January Makamba ambaye ni Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Charles Kitwanga (Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi) na Profesa Joyce Ndalichako ambaye ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Mawaziri wengine ni Waziri wa Mambo ya Nje, Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk Augustine Mahiga na Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Luhaga Mpina.
Alisema kutokana na kutotimiza masharti hayo, Rais Magufuli aliwaagiza mawaziri hao kuzipeleka fomu hizo mapema iwezakanavyo kabla ya saa 12 jioni jana, la sivyo wangekuwa wamejiondoa wenyewe kwenye madaraka waliyonayo.
Mawaziri hao jana mchana ama wao au kwa kuwatuma wawakilishi, waliwasilisha fomu hizo hivyo kukwepa adhabu ya awali iliyokuwa imetolewa na Rais ya kujiondoa wenyewe kwenye mamlaka waliyonayo.
Hata pamoja na kuruka adhabu hiyo ya awali, bado sheria hiyo ya maadili inatoa moja ya hatua zinazotakiwa kuchukuliwa kwa viongozi wa umma iwapo watakiuka masharti ya sehemu ya tatu inayojumuisha kifungu cha 9 (1)(b), zilizobainishwa katika kifungu cha nane.
“Masharti katika sehemu hii yatakuwa ni sehemu ya maadili ya viongozi wa umma kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ukiukwaji wa maadili utasababisha kuchukuliwa hatua mojawapo, yaani (a) kuonywa na kupewa tahadhari; (b) kushushwa cheo na (c) kusimamishwa kazi,” kinaeleza kifungu cha sheria hiyo iliyojumuisha mabadiliko ya mwaka 2002 na kuongeza hatua nyingine ambazo ni:
“(d) kufukuzwa kazi; (e) kumshauri kiongozi kujiuzulu wadhifa unaohusu ukiukaji huo; (f) kupewa adhabu nyingine zinazoruhusiwa kwa mujibu wa sheria za nidhamu kuhusu wadhifa wa kiongozi na (g) kuhimiza kuchukuliwa hatua kwa kiongozi kwa mujibu wa sheria za nchi zilizopo.”
Hadi jana wakati Waziri Mkuu anatoa agizo hilo la Rais la kuwataka kuwasilisha fomu hizo haraka kabla hawajatumbuliwa majipu, Makamba, Mpina, Kitwanga na Balozi Mahiga walikuwa wameshatimiza siku 46, baada ya muda wa mwisho wa kurudisha fomu hizo kisheria kukamilika.
Profesa Ndalichako alikuwa ametimiza siku 63 tangu ateuliwe hivyo alikuwa ameshapitisha siku 33 baada ya muda rasmi unaotakiwa kisheria kuwasilisha fomu hizo kwa Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Umma.
“Mheshimiwa Rais ameelekeza majina yao yasomwe ili popote walipo warudi na watekeleze agizo hilo na ofisi yangu itasimamia kikamilifu kuhakikisha fomu hizo zinawasilishwa kama inavyotakiwa,” alisema Majaliwa.
Kamishna wa Sekretarieti wa Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji Mstaafu Salome Kaganda ambaye juzi aliwasilisha majina ya mawaziri hao kwa Majaliwa, alisema vigogo wote hao walizishawasilisha fomu hizo.
Mawaziri wawasilisha fomu
Baada ya agizo la Rais Magufuli kutolewa na Waziri Mkuu jana saa sita mchana hadi saa 9.30 alasiri mawaziri wanne na naibu waziri mmoja walikuwa wamewasilisha fomu zao na kumpa nafasi Jaji Kaganda kuondoka ofisini kwake saa 10 jioni.
Mawaziri Dk Mahiga, Kitwanga na Mpina walifika wenyewe kwenye ofisi hiyo na kukabidhi fomu zao, wakati Profesa Ndalichako na January walituma wawakilishi wao kupeleka fomu hiyo.
Makamba alisema jana kuwa alishawasilisha fomu hizo tangu saa 8:00 mchana na kueleza kuwa zilikuwa zimejazwa tangu mkutano wa kwanza wa Bunge la 11, Novemba mwaka jana.
“Miaka yote huwa namtumia mwanasheria wangu wa siku nyingi ambaye huwa anazihakiki fomu na kugonga muhuri wa kiapo na kuziwashilisha Sekretarieti, lakini kwa bahati mbaya safari hii alipata hudhuru wa muda mrefu na mtu niliyemtuma hakunieleza jambo hilo.
“Siku zote nilikuwa naamini kuwa zimeenda na sikuwa na wasiwasi wa kwenda kufuatilia, lakini nilivyosikia kuwa hazijafika ilibidi tukazichukue nizijaze haraka na kuziwasilisha haraka hata kabla ya kunifikia barua rasmi,” alisema Makamba.
Mpina aliyekuwa wa mwisho kuwasilisha fomu hizo alisema alikuwa na sababu ya kuchelewa kujaza , lakini kwa hali ilivyo inaonyesha kuwa Rais hakukubaliana nazo hivyo kutoa agizo ambalo amelitii baada ya kufanikiwa kupata taarifa zilizomzuia kukamilisha.
“Binafsi sina malalamiko na hilo agizo ndiyo maana nimejaza, ila kilichonichelewesha sikuwa na taarifa za mshahara wangu, lakini baada ya agizo la Rais kuna mawasiliano yalifanyika mhasibu alikuja leo ofisini kwangu tukajaza wote ndiyo nimezileta hapa,” alisema Mpina.
Alisema kuwa: “Ukiona hivyo kwamba bwana mkubwa (Rais Magufuli) ametoa saa 12 ina maana sababu zetu zimekataliwa, maana jana (juzi) kwenye kikao tulikubaliana kwamba mwisho iwe mwezi wa nne, lakini nafikiri alilikataa hilo.”
Dk Mahiga alisema kuwa alipeleka fomu hizo kabla ya saa 6:00 mchana baada ya kushindwa kuziwasilisha mapema kisheria kutokana ratiba ngumu ya kazi aliyonayo.
“Natumia muda mwingi kusafiri na kuhudhuria mikutano kama wadhifa wangu unavyonitaka, hata mheshimiwa Rais anafahamu hili nilishamueleza.
“Kiufupi tangu nianze kazi, nimetumia nusu ya muda wangu kwenda nje ya nchi kuliko hapa nyumbani, lakini agizo la jana lilikuwa ni ukumbusho mwema,” alisema Mahiga huku akibainisha kuwa amekuwa akijaza fomu hizo kwa miaka zaidi ya 40 bila kumletea matatizo.
Hata wakati Balozi Mahiga akieleza hayo, Waziri Kitwanga aliilaumu Sekretarieti kuwa alikuwa ameziwasilisha fomu hizo tangu Januari 4, lakini zilikuwa hazionekani baada ya ufuatiliaji jana zilipatikana. “Nilikutana na Kamishna (Jaji Kaganda) na alinieleza kuwa wameshazipata fomu hizo,” alisema.
Jana jioni taarifa kutoka katika Ofisi ya Waziri Mkuu ilisema kuwa agizo hilo la Rais Magufuli la kuwataka mawaziri ambao hawajajaza Tamko la Rasilimali na Madeni wakamilishe kabla ya saa 12 lilitekezwa ipasavyo.
“Waziri Mkuu amepokea barua kutoka kwa Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji Mstaafu Salome Kaganda ikithibitisha kuwa mawaziri na naibu mawaziri wote wametekeleza agizo hilo.
“Hadi kufikia saa 9.30 leo(jana) alasiri mawaziri wote walikuwa wamekamilisha fomu zao za kuzikabidhi katika Ofisi za Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma,” alisema Waziri Mkuu.
Wakati huo huo; Majaliwa alisema Serikali itaendelea na mtindo wake wa kuwawajibisha viongozi wasio waadilifu na kuwataka watendaji wote waliopewa ridhaa ya uongozi kuwatumikia Watanzania kwa uadilifu mkubwa.
Alisema hayo jana jioni alipozungumza na viongozi wa dini, akifafanua kuwa Serikali haitamuonea yeyote na itatenda haki kwa kila mmoja. Alikuwa akijibu hoja ya Askofu wa Anglikana, Valentino Mokiwa aliyesema utumbuaji majipu unapunguza kasi ya utendaji na kuwajengea hofu watumishi.
No comments:
Post a Comment