Baraza la Sanaa la Taifa
(BASATA) limeufungia rasmi wimbo wa ‘Shika Adabu Yako’ ulioimbwa na Msanii Nay
wa Mitego kutokana na ukiukwaji mkubwa wa maadili, kashfa, uchochezi, kudhalilisha
watu na kuhatarisha amani na utengamano miongoni mwa wasanii na jamii kwa
ujumla.
Sambamba na kuufungia wimbo
huo, BASATA litampa karipio kali Msanii huyo na kumwagiza kuacha mara moja
kujihusisha kwa namna yoyote na tabia ya kuutangaza wimbo au kuusemea katika
vyombo vya habari vinginevyo hatua kali zaidi na za kisheria zitachukuliwa.
Ieleweke kwamba kwa mujibu
wa kifungu cha 4 (1) (j) cha sheria ya BASATA namba 23 ya mwaka 1984, Baraza
limepwa mamlaka ya kuratibu na kufuatilia mienendo ya mtu yeyote anayehusika na
kazi za Sanaa na kuhakikisha linalinda maadili ya kitaifa miongoni mwa Wasanii
wanapokuwa jukwaani au wanapobuni kazi yoyote ya Sanaa.
Aidha, kifungu cha 4 (2)
cha sheria hii kinalipa Baraza nguvu ya kisheria kufanya jambo lolote lile
kuliwezesha kufanya majukumu yake kwa faida na ustawi wataifa.Baraza la Sanaa la Taifa
limekuwa likipokea simu za maswali na malalamiko kadhaa kutoka kwa waandishi wa
habari na wadau wa Sanaa ambao kwa njia moja ama nyingine wameguswa na
kuchukizwa na kazi hiyo ambayo si tu inadhalilisha tasnia ya Sanaa bali
inawafanya watu makini kuanza kuhoji hadhi ya msanii, weledi na taaluma ya
Sanaa kwa ujumla.
BASATA mara kadhaa limekuwa
likikemea na kuchukua hatua kadhaa dhidi ya tabia hii chafu ambayo ilianza
kujitokeza kwenye kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka jana wa 2015. Kukemea huku
ni kwa msingi mmoja kwamba asili ya tasnia hii ya Sanaa ni kuelimisha jamii,
kukosoa pale kunapokuwa na tatizo, kuburudisha na kujenga jamii yenye staha, umoja
wa kitaifa, mshikamano na amani.
Ni wazi wasanii wengi
wanafanya kazi zao vizuri, kwa kubuni kazi zenye ubora, zenye kujenga jamii na
zaidi zinazoburudisha rika zote kiasi cha kuzifanya zililetee heshima taifa.
Kati ya hawa wengi, kuna wachache ambao wanaipaka matope tasnia ya Sanaa na kwa
kiasi kikubwa wanaonesha wazi kutokuwa na nia njema.
Kwa mantiki hii BASATA
halitavumilia hawa ‘wasanii’ wachache ambao wanataka kuigeuza tasnia ya Sanaa
na wasanii genge la wahuni, wasio na staha, wa kudharaulika na waliojipanga kuibomoa jamii na kuharibu
amani na utulivu uliopo nchini.
BASATA linapenda kueleza
yafuatayo:
1.
Vyombo vya habari viwe vya kwanza kuchuja
maudhui ya kazi yoyote ya Sanaa kabla ya kuingia kwenye mtego wa kuwa mawakala
wa uharibifu wa jamii kupitia kucheza kazi chafu za Sanaa. BASATA
lilishaziandikia radio zote kuzishauri kuwa na kamati za maudhui ya kazi za
Sanaa lakini inashangaza baadhi ya vyombo vya habari vinakuwa vya kwanza kushabikia
nyimbo hizo chafu na kuwapa muda mrefu wa mahojiano wasanii hao na baadaye
kurudi BASATA kuhoji uhalali wa nyimbo husika. Hii si sawa hata kidogo.
2.
Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt.
John Pombe Magufuli imejipanga kuwajengea mazingira bora ya utendaji Wasanii
wote nchini kupitia kuboresha miundombinu ya Sera, Sheria na Kanuni. Hata
hivyo, uwepo wa Wasanii kama hawa unafanya jamii kuhoji hadhi ya wasanii,
nafasi yao katika jamii na kwa maana hiyo kukatisha tamaa juhudi za kuipa
msukumo sekta hii maana wadau wakuu ambao ni wasanii wanaanza kuoneasha kuwa
mawakala wa uharibifu wa jamii.
3.
BASATA linawataka wasanii kujiuliza mara mbili
kabla ya kubuni kazi zao za Sanaa. Wafikirie wazazi, ndugu, jamaa na marafiki
zao watazipokeaje? Wavae nafasi ya wale wanaowatukana na kuwadhalilisha, Waelewe
kwamba Sanaa si uwanja wa kutusi na kudhalilisha watu hata kidogo. Ikitokea
wale wanaotukanwa na kudhalilishwa kughafilika Sanaa itakuwa uwanja wa vita.
Hili halikubaliki.
4.
Tunafahamu kuna wasanii wamekuwa wakifanya
hivyo makusudi kutafuta ‘umaarufu uchwara’ ambao wanadhani utakuja kutokana na
kuzungumziwa sana. Tunapenda kusema wazi kwamba umaarufu hauji kwa upuuzi wa
namna hiyo unakuja kwa msanii mwenyewe kujiheshimu, kujituma, kubuni kazi bora
na zenye kulifahamu vema soko la ndani na la kimataifa.
SANAA NI KAZI TUIKUZE,
TUILINDE NA KUITHAMINI
Godfrey
L. Mngereza
KATIBU
MTENDAJI, BASATA
No comments:
Post a Comment