ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, February 21, 2016

BRIGHT MWANG’ONDA: KUTOKA KUWA WA MWISHO HADI KUONGOZA KITAIFA

Bright Mwang'onda. 


Februari 18, ni siku ambayo Bright Mwang’onda (17) aliandika historia katika maisha yake. Katika matokeo ya mitihani ya kidato cha nne 2015, alikuwa miongoni mwa wanafunzi 10 waliopata alama za juu.

Saa nane mchana, baada ya matokeo hayo kutangazwa na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), nilifunga safari na kwenda Kisukuru Makoka, Dar es Salaam ambako Bright anaishi na wazazi wake.
Nilipofika nilimkuta akiwa na furaha, huku akimshukuru Mungu kwa hatua hiyo.
Bright aliyehitimu elimu ya sekondari katika Shule ya Marian Boys, anasema licha ya kuamini kwamba angefaulu kutokana na bidii aliyokuwa nayo darasani, hakutarajia kuingia 10 bora.
Alipata mshtuko baada ya mjomba wake, Rashid Kejo ambaye ni Mhariri Msanifu Mkuu wa Gazeti la Mwananchi, alipompigia simu kwa furaha akimpa hongera kwa kufanya vizuri mitihani yake na kuingia 10 bora.
“Simu ya mjomba ilinishtua kwa sababu nilijua nimefaulu lakini sikujua kama nitaingia 10 bora, hakika nimefurahi kuona ndoto yangu ya kuwa mhandisi wa ndege inaanza kutimia, namshukuru Mungu kwa hatua hii,” alisema.
Mama yake, Hamida Kejo aliyekuwa bustanini wakati anapokea taarifa ya kufaulu kwa mwanaye, alitupa jembe na kuanza kushangilia ushindi huo, huku akimshukuru Mungu.

Safari ya Bright kielimu
“Niliwahi kuwa wa mwisho darasani wakati nikisoma chekechea. Wazazi na walimu wangu hawakunichukia, walinitia moyo wakinisihi nikazane kusoma wakiamini nitabadilika,” anasema.
Alipoanza darasa la kwanza katika Shule ya Msingi St. Theresa, aliongeza bidii katika masomo yake. Wanafunzi alioanza nao darasa la kwanza wakati huo, ndiyo wale ambao alikuwa nao chekechea wakati aliposhika mkia kwenye mtihani wake.
“Japo nilikuwa mdogo lakini nilielewa na ninakumbuka kila kilichotokea, nilijisikia vibaya kufeli,” anasema.
Akiwa darasa la kwanza, maendeleo yake ya shule yalikuwa mazuri kiasi cha kuwashangaza walimu na wanafunzi wenzake na hata wazazi wake.
Ndani ya mwaka mmoja, Bright alisoma madarasa mawili yaani la kwanza na la pili.
“Darasa la kwanza alisoma miezi sita na la pili miezi sita, tulifurahi kuona mtoto anaendelea vizuri kielimu,” anasema mama yake.
Akiwa darasa la tatu, Bright aliongeza bidii zaidi na kushika nafasi ya kwanza katika mtihani wake wa nusu muhula.
Anasema tangu alipobaini kuwa hapaswi kufanya uzembe darasani alikazana kusoma na kila alipokuwa hajaelewa alimfuata mwalimu wa somo husika au rafiki zake wamuelekeze.
Katika matokeo ya mtihani wa taifa wa darasa la saba, Bright aliongoza katika darasa lake kwa kuwa wa kwanza.

Siri ya kufaulu
Anasema tangu alipoanza kidato cha kwanza Marian Boys, alikuwa akisoma kwa bidii na akiwa kidato cha pili alifaulu kwa asilimia 97 masomo yake yote jambo lililomuongezea faraja na hivyo kuongeza bidii ya kusoma.
“Vitu vitatu vimenifanya nifaulu, kumcha Mungu, kusoma kwa bidii na heshima kwa watu wote walionizidi, nilionao sawa na wadogo zangu,” anasema.
Kila siku alikuwa akianza kusoma saa moja jioni hadi saa tano na nusu au sita usiku.
“Muda wa ‘prepo’ ni saa moja hadi saa tatu lakini nilikuwa nafikisha saa tano na nusu au saa sita. Pia, kila siku asubuhi baada ya ibada nilikuwa napitia madaftari yangu katika kujiandaa kuingia darasani,” anasema.

Maisha yake shuleni
Siku zote aliamini hawezi kufanikiwa bila kuwapenda wenzake. Anasema kuna wakati alikaa na kuzungumza na wanafunzi watukutu.
“Nilijitahidi kutengeneza urafiki na kila mwanafunzi, sikupenda ubaguzi na niliepuka kuwachukia wengine kwa sababu yoyote,” anasema.

Familia yake
Bright ni mtoto wa pili kati ya watoto watano kwenye familia ya Benny Mwang’onda, mtangazaji wa Azam TV.
Dada yake, Shantal anasoma kidato cha sita katika Shule ya Sekondari ya Wama Nakayana huku Shadya, John na Chriss wakiwa kati ya kidato cha kwanza hadi cha tatu.
“Nawapenda ndugu zangu na wamefurahi kusikia nimefaulu vizuri, wote wapo shule wanaendelea na masomo yao,” anasema.

Ndoto zake
Anatamani kuwa mhandisi. “Nataka kuwa injinia wa kutengeneza ndege. Lengo langu ni kubuni na kutengeneza ndege hatua kwa hatua, siyo kuwa fundi wa kutengeneza zilizotengenezwa na wenzangu,” anasema.
Masomo anayotarajia kusoma kidato cha tano ni kemia, fizikia na hisabati. Katika matokeo yake, Bright amepata alama A kwenye masomo yote isipokuwa Civics (Uraia) alilopata B hivyo kupata daraja la kwanza.

Ushauri wake kwa wazazi
Anawaomba wazazi kuwafariji wanafunzi walioshindwa kufikia malengo yao akisema, kushindwa darasani siyo mwisho wa maisha.
“Wasiwapige wala kuwafanyia mabaya kwa sababu kufeli kupo. Wakiwafariji na kuwapa nafasi nyingine ya kusoma, watafaulu. Kama mama angenichukia nilipokuwa chekechea kwa kuwa wa mwisho, ningekata tamaa na nisingefika hapa nilipo,” anasema.
Mama yake, Hamida anasema malezi bora ya watoto yanachangia kufanya vizuri darasani.
“Inatupasa kuwalea watoto katika misingi mizuri ya kimaadili kwa sababu kwa kufanya hivi tunawaandalia njia nzuri ya kufanya vizuri darasani,” anasema.

Walimu wake walonga
Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Marian Boys, Gilbert Martine anasema Bright ni miongoni mwa watoto watiifu na waliokuwa mstari wa mbele kufuata ratiba ya shule na binafsi.“Haikuwa rahisi kumkuta Bright akifanya makosa, ni msikivu na mwenye kupenda kusoma,” anasema.
Hata hivyo, anasema wanafunzi wengi shuleni hapo wamekuwa wakifanya vizuri katika masomo yao kutokana na utamaduni wa kupenda kujisomea ambao wamekuwa wakijengewa.

Shabiki mkubwa wa Magufuli
“Nampenda Rais John Magufuli kwa sababu ya ufanyaji wake wa kazi. Kiuhalisia sipendi kabisa siasa kwa sababu siwezi kuongea sana,” anasema.

No comments: