Advertisements

Friday, February 5, 2016

Chama chasajiliwa kikiahidi kushirikiana na CCM

Msajili ya Vyama vya Siasa, Jaji Francis
Msajili wa vyama vya siasa, Jaji Francis Mtungi

By Mwandishi Wetu, Mwananchi mwananchipapers@mwanchi.co.tz

Dar es Salaam. Msajili ya Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi jana alikabidhi cheti cha usajili wa muda kwa chama kipya cha Maadili na Uwajibikaji (CM - Tanzania), ambacho kimeahidi kushirikiana na CCM.

Mwenyekiti wa muda wa chama hicho, Laban Nkembo alisema kimeanzishwa ili kusimamia maadili na uwajibikaji mambo ambayo yamekuwa tatizo kubwa katika jamii ya Watanzania.

Alisema walifanya mashauriano na viongozi wa dini na kupata mbadala wa kuanzisha chama kipya ambacho kitasimamia masuala ya maadili na uwajibikaji na kwamba wamekamilisha hatua hiyo ya awali iliyoanza miaka sita iliyopita.

“Chama chetu siyo cha upinzani, ni chama cha siasa. Tutashirikiana na Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa sababu ndicho chama tawala na kimekuwa madarakani kwa muda mrefu. Madhaifu waliyonayo ni ya kibinadamu ambayo yanaweza kumkuta mtu yoyote,” alisema mwenyekiti huyo. Nkembo alisisitiza kwamba watafanya kazi kwa bidii ili kuunga mkono jitihada za CCM katika kuleta maendeleo ya Taifa. Kiongozi huyo alisema lengo kubwa la chama hicho ni kurejesha uhai wa Taifa kimaadili na kiuwajibikaji katika mamlaka na jamii.

Akizungumza baada ya kukabidhi hati hiyo, Jaji Mutungi aliitaka Serikali kuiwezesha ofisi yake kufanya uhakiki wa vyama vya siasa ambavyo havifanyi kazi kwa mujibu wa sheria. Alisema uhakiki huo utaifanya nchi kuwa na vyama imara vya siasa wakati wote vitakavyotekeleza masharti yote ya kisheria.

Alisema chama cha siasa kinakuwa imara kama viongozi wake wanafuata katiba ya chama chao.


“Tumekuwa tukisikia migogoro ya ndani ya vyama vya siasa muda mfupi tu baada ya kupewa usajili wa muda. Tatizo hilo linasababishwa na uchu wa madaraka unaosababishwa na waanzilishi. Lazima muwe na demokrasia ndani ya chama chenu,” Jaji Mutungi aliwaeleza wanachama wa CM – Tanzania waliohudhuria tukio hilo.


Alisema chama ni taasisi na siyo mali ya mtu mmoja, hivyo waanzilishi wa vyama vya siasa waheshimu katiba zao na kuruhusu demokrasia.


Msajili Msaidizi, Sisty Nyahoza alisema kupata usajili wa kudumu ni suala gumu ambalo linahitaji nguvu ya pamoja katika kukamilisha vigezo na masharti vinavyotolewa. Alisema usajili huo wa muda utadumu kwa siku 180, baada ya hapo watapewa usajili wa kudumu endapo watakidhi masharti.

1 comment:

Anonymous said...

What is his job? does he register parties everyday? Do you really need a registrar of political parties?