ANGALIA LIVE NEWS

Monday, February 22, 2016

CHUMBA CHA KUDHIBITI UMEME CHAUNGUA


Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), limesema kuungua moto kwa chumba maalumu cha kudhibiti umeme katika kituo cha Gongolamboto ni sababu ya Wilaya ya Ilala na Kisarawe mkoani Pwani kukosa umeme.
Tukio hilo lilitokea juzi saa tano usiku chanzo kikiwa ni hitilafu iliyotokea katika kifaa kijulikanacho kama sacket breaker kwenye chumba hicho.
Miongoni mwa maeneo yaliyokosa umeme baada ya tukio hilo ni Gongolamboto, Kisarawe, Mongolandege, Chanika Ulongoni na maeneo ya jirani.
Akiwa katika kituo hicho, Meneja wa Tanesco Ilala, Mhandisi Athanasius Nangali alisema jana kuwa : “Kwa niaba ya Tanesco, tunawaomba radhi kwa hali hii iliyojitokeza na tuna imani itarudi kawaida mafundi wanalishughulikia.”
Alisema kituo hicho ni cha muda mrefu na baadhi ya vifaa vyake ikiwamo kilichopata hitilafu vilifungwa tangu mwaka 1952. Mhandisi Nangali alisema katika kuhakikisha wanatoa huduma ya umeme ya uhakika Tanesco imejenga kituo kingine jirani ambacho kitatoa umeme megawati 50, mara mbili ya kituo hicho cha zamani.
“Kituo hiki kipya tunatarajia kuanza kukitumia Juni, mwaka huu,” alisema Mhandisi Nangali.
Kaimu Naibu Meneja wa Usafirishaji Tanesco, Mhandisi Richard Msiyani alisema baadhi ya vifaa vilivyoharibika mafundi wamekwenda kuvifuata sehemu husika. “Wateja wetu wavute subira, kila kitu kitakuwa sawa, kwani mafundi wanajitahidi kadri ya uwezo kushughulikia jambo hili,” alisema Mhandisi Msiyani.

No comments: