Fundi wa Shirika la Majisafi na Majitaka Dar es salaam (Dawasco), akiondoa bomba la maji lililounganishwa kinyume cha taratibu katika moja ya nyumba iliyopo eneo la Tabata Magengeni jijini Dar es Salaam. Dawasco imeanza operesheni
wizi wa Maji iliyoanza hivi karibuni katika maeneo yote ya jiji la Dar es
salaam.
Na Mwandishi wetu,
Shirika la
Majisafi na Majitaka Jijini Dar es Salaam (Dawasco), imenasa wizi mkubwa wa
Maji katika nyumba tano ambazo zimeunganishiwa huduma ya majisafi kinyume cha
utaratibu maeneo ya Tabata Magengeni, nyumba hizo zinamilikiwa na
mfanyabiashara mmoja ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja, nyumba
hizo zimepangishwa kwa familia tano tofauti (Apartments).
Akizungumzia tukio hilo katika operesheni ya mtaa kwa mtaa ya
kuhakiki matumizi sahihi ya Maji kwa wateja wa majumbani, Meneja wa Dawasco
Tabata, Bi. Victoria Masele, alisema kuwa amebaini wizi huo baada ya kuona bili
ya mwezi inayokuja haiendani na matumizi halisi ya Maji, hivyo wakaamua kufanya
uchunguzi na kubaini kuwa mteja alikuwa amejiunganishia huduma ya Maji kinyume
cha taratibu.
“Msoma mita wetu alikuwa na wasiwasi sana na matumizi ya Maji ya
hizi nyumba, kwa sababu bili ilikuwa ndogo ukilinganisha na idadi ya familia
zinazoishi kwenye hizi nyumba, ndipo tukaamua kufanya uchunguzi wa kina na
kukuta mteja amejiunganishia laini 3 za Maji, laini 1 ikiwa imepita kwenye
mita, 2 hazijapita kwenye mita, zimeelekezwa kwenye kisima na baadaye Maji
yanasukumwa na kujaza matenki 5 ya lita 10,000, na lingine la lita 6000”
“Baada kunasa wizi huo, tuliwasiliana na meneja wa nyumba hizo
ambaye hakuwepo eneo la tukio, na kudai kuwa hajui chochote kuhusiana na wizi
huo wa Maji kutokana na kuishi mbali na nyumba hizo na kwamba wizi huo
inawezekana wa wapangaji wenyewe, lakini aliahidi kufika katika ofisi zetu za
Dawasco kumaliza tatizo baada ya wapangaji kushindwa kutupa ushirikiano” alisema Bi. Masele
Hadi taarifa hizi zinakwenda mtamboni, meneja wa nyumba hizo
alifika katika ofisi za Dawasco Tabata na kufanya mazungumzo na Meneja wa
kituo, na kutakiwa kulipa faini ya kiasi cha shilingi milioni 5.3.
DAWASCO inaendelea kutoa rai kwa wananchi wote kuwafichua wezi wa
Maji kwa kuwa wanasababisha wateja halali kukosa huduma ya Maji kwa wachache
kujiunganishia huduma kinyume na taratibu, hivyo mwananchi yeyote ambaye
amejiunganishia Maji kinyume cha taratibu na ambaye hana huduma ya Maji afike
katika ofisi yoyote ya Dawasco iliyopo karibu yake ili aunganishiwe huduma ya
Maji kihalali.
No comments:
Post a Comment