ANGALIA LIVE NEWS

Friday, February 5, 2016

Dk. Mahiga aanika siri Magufuli kutosafiri nje

Zikiwa zimebaki siku sita, Rais John Magufuli, afikishe siku 100 za utawala wake bila kusafiri nje ya nchi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kanda na Kimataifa, Balozi Augustine Mahiga, ameeleza sababu zinazofanya kiongozi huyo kutosafiri nje ya nchi.

Akizungumza katika mahojiano maalum na Nipashe mjini Dodoma jana Balozi Mahiga alisema bado kuna uwezekano Rais Magufuli akaendelea kutosafiri kwenda nje ya nchi, akiyataja mambo hayo matatu kuwa ndiyo sababu kuu ya kufanya hivyo.

Aliyataja mambo hayo kuwa ni ukata wa fedha alioukuta serikalini wakati akiingia madarakani, kupata muda wa kuendelea kuuda serikali yake na sakata la uchaguzi wa Zanzibar.

Kauli hiyo ya Balozi Mahiga ilitokana na swali aliloulizwa na Nipashe juu ya athari ambazo Tanzania inapata kwa Rais Magufuli kutoudhuria mikutano ya kimataifa ukiwamo wa Umoja wa Afrika na ule wa Rais wa China aliyekutana na marais wa Afrika, nchini Afrika Kusini.

“Kwa kipindi hiki cha mwanzoni Rais ametoa maelezo, ameomba radhi kwamba yuko kwenye kuunda serikali maana hata kuunda baraza la mawaziri ilichukua karibu mwenzi mzima na hata tunavyozungumza hivi hajakamilisha uunda serikali yake. Mbali na kuunda baraza bado kuna kuteua wakuu wa mikoa, wilaya na wakuu wa taasisi mbalimbali,” alisema na kuongeza:

“Lakini pia alikuta serikali iko katika hali ngumu sana kifedha, akaona utendaji kazi lazima asimamie mwenyewe. Kwa hiyo kote huko ambako alitakiwa kwenda kwa miezi sita ya kwanza aliomba radhi na ameeleweka kabisa na ninadhani kazi hii ya kuweka msingi, mwelekeo na msimamo itaendelea kwa miezi minne au mitatu.”

Aidha, Balozi Mahiga alisema suala la Zanzibar ambalo hajalimaliza, huku Bunge likiwa ndiyo limeanza vikao vyake ni miongoni mwa mambo yaliyomlazimu Rais Magufuli kukaa nyumbani.

Alisema, mbali na kutoaudhuria mikutano hiyo, Rais Magufuli amekuwa akiwahakikisha marais wenzake kwamba baada ya kumaliza hatua za kuunda serikali yake atakuwa tayari kuonana nao.

Alipoulizwa ni vitu gani ambavyo Rais asipovisimamia vinaweza kuharibika, alisema: “Kwa mfano masuala ya usimamizi wa fedha, tumeona taasisi zinavyopambana, watu kupoteza ushahidi, komyuta zinaibiwa, mafaili yanaibiwa, kuna maamuzi mengine ni rais tu anaweza kutoa uamuzi.”

“Fikiri unaenda kwenye mkutano unakaa siku tatu huku mambo hayajakamilika, utaona tu bora urudi ukaliweke vizuri, kutengeneza serikali siyo sawa na kupanga timu ya mpira, inachukua muda, kuna kutafuta watu, kuwapima na kuwachuja, tusifikiri serikali ni mawaziri na wakuu wa mikoa tu.”

Alisema kuna taasisi muhimu, mashirika ya umma yapo mengi na yanahitaji mabadiliko, hivyo Rais ni lazima asimamie. “Kwakweli Rais wetu ana nguvu ya kipekee, kwa sababu kwa siku labda ana saa tatu tu za usingizi,” aliongeza kusema.

FEDHA ZILIZOOKOLEWA
Balozi Mahiga alisema hana takwimu za moja kwa moja za juu ya fedha zilizookolewa kwa Rais kutosafiri nje, ingawa ana amini gharama zimepungua kwa kiasi kikubwa.

“Naweza kusema tumepunguza sana matumizi ya safari na tumetenga kati ya safari za Rais na zile za wizara kwa sababu huko nyuma safari za Rais na watu wake viongozi wakubwa zote zilikuwa zinajumuishwa kwenye gharama za safari za wizara ndiyo maana zilikuwa zikionekana ni kubwa,” aliema.

Alisema pamoja na kwamba Rais hajaanza kusafiri nje ya nchi, lakini ametoa maagizo ambayo yameanza kutekelezwa, ikiwamo balozi zimeanza kupewa uwezo wa ziada kama wataalamu wanaofaa, watumizshi wa kutosha na kupatiwa fedha za kukidhi mahitaji katika kuwakilisha nchi na hasa katika kushirikiana na kampuni, mashirika na kanda.

“Agosti kuna mkutano wa Organ of Peace and Security wa Sadc ambao Tanzania itakuwa mwenyekiti, hii lazima Rais awepo, mwenyekiti wake lazima daima awe Rais, lakini siyo lazima aende Gaborone anaweza kuita wenzake hapa.”

“Rais mwenyewe ameeleza kwamba anapunguza matumizi, kwa hiyo yawezekana kabisa kwenye mkutano wa siku tatu anaweza kwenda kwa siku moja na nusu, au badala ya kwenda na wasaidizi 30 ataenda na 15, juzi tulivyokwenda na Makamu wa Rais Addisababa, Ethiopia, awali kwenye safari kama ile watu 30 mpaka 35 ndio walikuwa wakienda, lakini juzi alikuwa na watu 15, mimi kwa wizara yangu walikuwa wawili na wengine wote walionisaidia walitoka kulekulekule,” alisema.
CHANZO: NIPASHE

3 comments:

Anonymous said...

Rais sio lazima asafiri nje ya nchi. Hiyo ndio shida ya kuwa na Marais wanaotaka Mambo ya Nje. Hata wakati wa kampeni wapiga kura hawajali wala kuongelea mambo ya nje.mwanataka maji, afya, umeme, elimu nk. Hayo si lazima usafiri kuyapata. Ukiwa na Rais makini na mduatiliaji kama Magufuli na ukiwa na timu ya uongozi bora yenye kufanya kazi uchumi wetu wenyewe unaweza kuyafanikisha yote hayo.

Korea Kusini mwaka 1960 ilikuwa na hali ya kiuchumi sawa na Tanzania. Leo wanatupatia misaada! Rais Magufuli kasema tukisimamia mambo yetu vizuri sisi tunaweza kuwa donors (wafadhili). Yupo sahihi. Tumuombee kweli na sio kumtakia safari zisizo na tija. Mungu ibariki Tanzania.

Anonymous said...

Ingawaje marekani ni nchi kubwa lakini tujiulize maraisi wao au viongozi wao wengine wa nchi kwanini hatuwaoni kutembelea nchi zetu mara kwa mara? Marais wetu na viongozi wengine wa nchi wapo tayari ikiwezekana kusafiri kwenda marekani hata mara tatu kwa mwaka juu ya gharama ya serikali. Mwacheni magufuli afanye yake kwani ni mtu anayejitambua na ni mkereketwa namba one wa kuiona Tanzania inaondokana na unyonge.

Anonymous said...

Hatuhitaji raisi tourist.kama kusafiri kwa raisi ndio maendeleo ya nchi basi kwa tuliyoyaona katika awamu ya 4 nchii hii ingekuwa the most richest country in the world.