Dar es Salaam. Wizara ya Maliasili na Utalii imesema inatathmini mbinu za kukabiliana na ujangili na itaanzisha Jeshi Usu litakalokuwa na jukumu la kupambana na ujangili kwenye mbuga na hifadhi zote nchini.
Mpango huo umetangazwa siku moja baada ya Jeshi la Polisi kukamata watu tisa wanaotuhumiwa kuhusika na utunguaji wa helkopta iliyokuwa ikifanya doria kwenye Pori la Akiba la Maswi na ranchi ya Wanyamapori ya Mwiba.
Katika shambulio hilo la Januari 29, rubani wa helikopta hiyo, Rodgers Gower aliuawa na abiria kujeruhiwa.
Mbali na tukio hilo, kumekuwa na idadi kubwa ya wanyamapori wanaouawa na majangili, hasa tembo ambao kasi ya kutoweka kwao imeishtua dunia.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa jana, Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe alisema wizara yake imejipanga kuimarisha mapambano dhidi ya ujangili na usafirishaji haramu wa mazao ya wanyamapori na misitu.
“Wizara inarejea mbinu za kukabiliana na ujangili na kikosi maalumu kitaanzishwa ili oparesheni ziwe endelevu. Kutakuwa na mabadiliko ya kiutendaji kwa wahifadhi kutoka ule wa kiraia kwenda wa Jeshi Usu, paramilitary,” alisema Waziri Maghembe.
“Tulikuwa na wapiga shabaha raia, lakini sasa tutakuwa na askari watakaopambana na majangili hawa wanaotumia silaha nzito.”
Jeshi hilo maalumu litajumuisha askari kutoka Idara ya Wanyamapori, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tawa), Hifadhi za Taifa (Tanapa), Mamlaka ya Ngorongoro (NCAA) na Wakala wa Huduma za Misitu (TFS).
Profesa Maghembe alieleza kuwa oparesheni za kushtukiza zimefanikisha kukamatwa kwa watu kadhaa waliokuwa na silaha, risasi na nyara za Serikali hivyo wizara hiyo kwa kushirikiana na wadau wengine imejipanga kwa vifaa na mbinu bora zaidi.
Kuhusu waliokamatwa kwa tuhuma za kuangusha helikopta hiyo, alisema watu hao walikutwa na silaha mbili aina ya rifle pamoja na risasi tano za zana hizo za mapambano, pikipiki moja na kilo 31 za pembe za ndovu alizodai kuwa walimuua siku ya tukio.
Waziri Maghembe alisema katika wiki hiyo ya msako waliwakamata majangili wanane kwenye Hifadhi ya Selous wakiwa na silaha 20 na wilayani Tunduru walipata silaha 400.
Aliwapongeza wananchi na kuwataka kuendelea kushirikiana na mamlaka husika.
Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Ernest Mangu alisema askari wake watakagua watu wote wanaomiliki silaha kisheria baada ya kupata taarifa kuwa hujihusisha na ujangili kwa kuzikodisha kwa majangili.
Alisema wakiwabaini watu hao, watawanyang’anya ili kuzuia matumizi mabaya ya silaha hizo.
No comments:
Post a Comment