Advertisements

Tuesday, February 9, 2016

Mabalozi wakomalia maridhiano kabla ya uchaguzi Zanzibar

Mabalozi wa nchi mbalimbali nchini wakimsikiliza Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Augustine Mahiga wakati wa sherehe za mwaka mpya wa mabalozi zilizofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam jana. Picha na IKULU

By Nuzulack Dausen, Mwananchi ndausen@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Jumuiya ya mabalozi nchini imeendelea kushikilia msimamo wao wa kuitaka Serikali kutafuta suluhu shirikishi ya mgogoro wa kisiasa Zanzibar, licha ya Serikali kusema kuna nafasi ya mazungumzo ya namna ya kuboresha uchaguzi wa marudio.

Kaimu kiongozi wa mabalozi hao, Edzai Chimonyo alisema jana kuwa jumuiya hiyo inaiomba Serikali itumie busara kutafuta suluhu ya kudumu kumaliza mvutano unaoendelea visiwani humo ili Wazanzibari waendelee kuishi kwa amani.

“Kuhusu suala la Zanzibar, ni matumaini yetu kuwa kupitia busara na ushauri wako suluhu inayokubalika pande zote mbili itapatikana,” alisema Chimonyo ambaye pia ni balozi wa Zimbabwe nchini.

“Wazanzibari wameungana na kuacha tofauti zao na tunaamini wataendelea kufanya hivyo ili kudumisha umoja na amani.”

Alisema jumuiya hiyo inaamini pia kuwa Serikali itakamilisha mchakato wa Katiba mpya uliokuwa umeanzishwa na Serikali iliyopita ambao ulikwama kutokana na kutokamilika mapema kwa Daftari la Wapigakura.

Kuhusu mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar, Wazoro wa Mambo ya Nje, Dk Augustine Mahiga alisema pamoja na Zanzibar kuwa ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ina mfumo wake wa kisiasa, utamaduni, Serikali, Katiba na tume huru ya uchaguzi.

Alisema baada ya mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), Jecha Salim Jecha kufuta uchaguzi kwa sababu ya kukiukwa kwa sheria na kanuni za uchaguzi, kulianzishwa mazungumzo baina ya pande zinazohusika lakini muafaka haukufikiwa na mbadala ukawa kurudia uchaguzi. Dk Mahiga aliiomba jumuiya ya kimataifa kuunga mkono uamuzi huo wa kurudia uchaguzi akisisitiza kuwa bado kuna nafasi ya wadau na pande zinazohusika kufanya mazungumzo ya kuboresha uchaguzi huo.

Alisema Serikali yake itaendelea kushirikiana na jumuiya ya kimataifa katika masuala mbalimbali.

1 comment:

Anonymous said...

Mabalozi fungeni misaada waafrica ndo tabia yetu kutokubali kushindwa
Mtaaona