Advertisements

Tuesday, February 9, 2016

Zanzibar kaa la moto.

Mgogoro wa kisiasa Zanzibar umegeuka kaa la moto baada ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk. Augustine Mahiga, kuwaeleza mabalozi wanaowakilisha nchi zao Tanzania kwamba, nafasi ya mazungumzo bado ipo, huku CUF ikisema hiyo ni danganya toto kwa kuwa CCM na serikali yake haitaki mazungumzo.

Zanzibar iko katika mkwamo wa kisiasa baada ya Tume ya Uchaguzi visiwani humo (ZEC) kufuta matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana kutokana na kile kilichoelezwa na Mwenyekiti wa tume hiyo, Jecha Salim Jecha, kwamba ulijawa na kasoro nyingi zilizopotezea sifa ya kuwa huru na wa haki.

Aliyekuwa mgombea urais visiwani humo kupitia CUF, Maalim Seif Sharif Hamad na wanachama wenzake walishatangaza kutoshiriki uchaguzi wa marudio na badala yake kusisitiza ZEC iendelee na majumuisho ya kura za uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana ili mshindi ajulikane.

Hata hivyo, Chama Cha Mapinduzi (CCM), kilichomsimamisha Dk. Ali Mohamed Shein, kutetea nafasi yake ya urais, kimeridhia uamuzi wa ZEC kuwa uchaguzi huo urudiwe.

MAGUFULI NA MABALOZI
Akizungumza na mabalozi na wawakilishi wa taasisi za kimataifa nchini kwa niaba ya Rais Dk. John Magufuli, Ikulu, jijini Dar es Salaam jana, Dk. Mahiga alisema bado mazungumzo na ushauri unakaribishwakuhusiana na sakata hilo ili kuhakikisha uchaguzi wa marudio unakuwa huru na haki.

Alisema ZEC imeshatangaza Machi 20, mwaka huu kuwa ndiyo tarehe rasmi ya kufanya uchaguz wa marudio, lakini Serikali ya Jamhuri ya Muungano bado inakaribisha mazungumzo kutoka upande wowote ili kufanikisha uchaguzi huo kwenda vizuri.

Alisema Watanzania wote kwa sasa wanatarajia kuwapo kwa uchaguzi wenye amani na utulivu visiwani humo na kwamba bado nchi haijachelewa katika kuleta amani visiwani humo.

“Uchaguzi utafanyika Machi 20 na leo (jana) ni Februari 8, hivyo kuna siku kama 40 kufanyika, hivyo muda bado wa kufanya mazungumzo tutaona namna gani uchaguzi huo utakuwa huru na haki,” alisema Balozi Mahiga.

Alisema serikali ya awamu ya tano itaendelea kushirikiana na nchi nyingine kimataifa zilizomo barani Afrika na nje ya Bara la Afrika.
Naye Mwenyekiti wa mabalozi waliopo nchini, ambaye ni Balozi wa Zimbabwe, Edzai Chimonyo, alisema mgogoro wa Zanzibar unaweza kumalizwa kwa mazungumzo ya pamoja visiwani humo.

Alisema wananchi wa Zanzibar wanapaswa kuweka tofauti zao pembeni na kujali maslahi ya nchi kwa maslahi yao na taifa lao.

MSIMAMO WA CUF
Jana Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, alisema wanamshangaa Balozi Mahiga kwa kauli yake hiyo kwani ni hivi karibuni walimsikia akisema kuwa mabalozi wasionane na vyama vya siasa bila kupitia ofisi yake.

“Kwenye nchi hii demokrasia inakandamizwa, inakanyangwa, sisi tumewaomba mazungumzo yafanyike, katikati ya mazungumzo wanatangaza tarehe ya uchaguzi,” alisema Mazrui na kuongeza:

“Kwa kawaida mpaka mazungumzo yaishe ndiyo mtangaze uchaguzi, sasa wao hawataki mazungumzo wanataka uchaguzi, ukisikiliza hotuba za Magufuli (Rais John Magufuli) hazungumzii mazungumzo ni uchaguzi tu, kwa hiyo hawaamini mazungumzo wanataka uchaguzi, sisi kama chama hatujakataa mazungumzo, tuko tayari kuzungumza na mtu yeyote, wakati wowote, lakini lazima haki itendeke, Lakini wao, wote wanataka uchaguzi, hawataki mazungumzo,ndiyo maana wakatangaza tarehe ya uchaguzi.”

Nipashe ilipotaka kujua ni kwa nini, Balozi Mahiga anadhani kwamba CUF wako karibu zaidi na wahisani na nchi nyingine za nje kuliko CCM ama serikali, Mazrui alisema wao tangu uchaguzi wa mwaka 1995 mpaka wa mwaka jana, hawajasaidiwa chochote na wahisani.

Alisema kwa sababu wao hawana serikali na pia hawawezi kuwa karibu na mabalozi ama nchi nyingine kuliko serikali, lakini wanapopata fursa huwa wanazungumza nao.

“Ukweli ni kwamba sisi tunaongea nao (CCM na serikali), Maalim Seif kakutana na Kikwete mara moja baada ya kumwandikia barua chungu nzima. Kaandika barua chungu nzima kwa Magufuli, kakutana naye mara moja tu na alipotaka kuonana naye tena mpaka leo hajakubaliwa.”

“Amekutana na viongozi sita wa CCM na wamefanya mikutano tisa, yeye akiwa mwenyewe tu, halafu leo anasema tunakutana na mabalozi zaidi, ameomba (Maalim Seif) kuonana na Mkapa (Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa), mara kibao mpaka leo hajakubaliwa.”

Alisema Maalim Seif amefungua milango ya mazungumzo kwa sababu ni muhimu kwa maridhiano yaliyofanyika miaka mitano iliyopita.
“Wao wanataka turudi kule nyuma, kwenye uhasama, hakuna kuzikana, kutembeleana, madukani hatuuziani vitu, hakuna maendeleo katika nchi, hakuna ushirikiano, hata wawekezaji hawaji, watalii hawaji, ni kugombana tu na maandamano, mabomu ya machozi, hakuna amani kwenye nchi,” alisema.

Alisema kwa miaka mitano waliyokaa kwa amani, maendeleo kwenye visiwa hivyo yameonekana, jambo ambalo kwa sasa lipo hatarini kupotea.

“Mimi nilikuwa waziri kwa miaka mitano na Shein (Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein) alikuwa bosi wangu, nimefanya naye kazi kwa utulivu, sasa hivi nitakuwa simuheshimu tena, ndiyo wanatupeleka huko. Mimi najua na matokeo yake ndiyo maana hatutaki turudi kwenye historia ya nyuma badala ya kwenda mbele, serikali wasema ukweli, wakae waone mazungumzo ni bora kuliko uchaguzi, huu siyo uchaguzi ni uchafuzi,” alisema Mazrui.

Naye Mkurugenzi wa Mawasiliano wa CUF, Ismail Jussa Ladhu, alisema: “Suala la CUF kukaa na mabalozi kuzungumza ni jambo la kawaida na tumekuwa tukikutana nao, lakini hatupo tayari kukaa kuzungumza ajenda ya kurudia uchaguzi kwani ni sawa na kuhalalisha kufanyika uchaguzi batili Zanzibar.”

Jussa alisema Dk. Mahiga alitakiwa kutumia diplomasia kwa kushirikiana na mabalozi kumshawishi Dk. Shein kuheshimu matokeo ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana.

“Mabalozi hawana uwezo wa kutulainisha kushiriki uchaguzi wa marudio wakati uchaguzi wa Zanzibar umefanyika na wananchi wametoa maamuzi yao muhimu yaheshimike,” alisema Jussa.

Alisema msimamo wa CUF upo wazi katika mkwamo wa uchaguzi wa Zanzibar kuwa ZEC irudi kazini kukamilisha uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka jana kwa kutangaza matokeo na mshindi katika uchaguzi huo.

KAULI YA DK. MAHIGA
Akizungumza na Nipashe mwishoni mwa wiki, Balozi Mahiga alisema: “Naona kwa sababu sisi wenyewe ile inaitwa confidence (kuaminiana) haipo sana… kati ya sasa na Machi tuendelee na confidence building period (kipindi cha kujenga kuaminiana), bado kuna nafasi ya mazungumzo.”

Alisema katika kipindi hiki (sasa hadi Machi), kuwe na ushawishi kwa pande zote kuhusiana na uchaguzi huo.
“Kupeana ushawishi wa namna fulani… unataka kuwe na maandalizi ya namna gani, ushiriki wa namna gani, tuna karibu siku 50. Lakini pia marafiki zao (CUF) wawashawishi.”

Alipotakiwa kueleza ni kwa nini anaona kwamba CUF ipo karibu zaidi na wahisani hadi kusema ni marafiki zao, alisema: "Ni kwa sababu ya ile ghadhabu wanayoifanyia serikali ya Tanzania, ni kama vile kwa nini huyu mmemfanyia hivi. Hebu fikiria, chama ambacho kina wafuasi wengi wasishiriki katika uchaguzi, tutakuwa na miaka mitano ya aina gani. Tutarudi kule nyuma tulipotoka?. Siyo sahihi, hatuwatendei haki watu wa Zanzibar, hatuwatendei haki Watanzania wengine ambao wote tunabeba mzigo sasa hivi kwa sababu ya maamuzi tu ya chama kimoja.”

Alisema mazungumzo baina ya CUF na CCM yalianza na kufanya takribani vikao tisa, huku kukiwa hakuna kitu kinachosemwa juu ya kinachoojadiliwa.

“Tukasema jamani eeeh, mbona hatusikii tamko lolote? na hapo ndipo Rais Magufuli akachukua uamuzi wa kuzungumza na pande zote mbili. Akazungumza na Seif (Mgombea wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad) na Dk. Shein (Rais wa Zanzibar), kwamba jamani vipi?”

“Na wao walisema wanazungumza wenyewe na wamejumuisha marais wa zamani wa Zanzibar, siyo marais wa zamani wa bara. Na kila mtu akawa anauliza hivyo, jamani vipi? Sasa wakati wanazungumza hivyo, baadhi ya wadau wetu wa maendeleo na marafiki zetu wakawa wanasema, Jamhuri ya Muungano hawafanyi vya kutosha, kusukuma na kutatua suala hili,” alisema.

“Wengine wakasema hata misaada tunasimamisha, kama vile Marekani (MCC)… tunasimamisha kwa sababu sisi tunaona haya mazungumzo hayatoi majibu na afadhali tu yatangazwe (matokeo ya uchaguzi) kama yalivyokuwa, lakini katika hilo baadaye tume ikasema jamani, afadhali tuitishe uchaguzi mwingine.

“Sasa mimi ninaloeleza katika hili kwa marafiki zetu, ni kwamba kama upinzani wanadai kwamba waliungwa mkono na kushinda, sasa hivi hawana cha kuogopa… wana uchaguzi mwingine. Wale waliowachagua na wanaodai kwamba waliwapa ushindi kwa nini wasiwachague kama walivyowachagua huko (awali),” alisema Balozi Mahiga.

SERIKALI Z’BAR YAWAJIBU MAKAMISHNA ZEC
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imesema hakuna vyombo vya juu vya serikali vilivyoshawishi Mwenyekiti wa Zec, Jecha kufuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana kama ilivyodaiwa na makamishna wawili wa ZEC kutoka CUF.

Hayo yalisemwa mjini Zanzibar jana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud Mohamed, siku moja baada ya makamishina hao kudai matokeo yalifutwa baada ya Jecha kushawishiwa na vyombo vya juu vya serikali visiwani Zanzibar.

Alisema matokeo ya uchaguzi mkuu wa Zanzibar yalifutwa na ZEC yenye bila ya kushawishiwa na vyombo vya serikali baada ya kujiridhisha kuwa uchaguzi ulikuwa na kasoro.

Alisema kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984, Zec ina uwezo wa kuratibu na kusimamia uchaguzi bila ya kuingiliwa na mtu au mamlaka yoyote.

Habari hii imeandaliwa na Fredy Azzah, Gwamaka Alippi, Dar es Salaam, Mwinyi Sadallah na Rahma Suleiman, Zanzibar.
CHANZO: NIPASHE

No comments: