ANGALIA LIVE NEWS

Friday, February 26, 2016

Magufuli aonyeshwa mawaziri majipu.

Wakati serikali ya awamu ya tano ikiongoza kutumbua majipu, Kamishana wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji Salome Kaganda, amesema baadhi ya mawaziri wamekiuka sheria ya maadili kwa kutokujaza fomu za tamko la rasilimali, maslahi na madeni pamoja na ahadi ya uadilifu.

Aidha, amesema Rais Dk. John Magufuli, Makamu wa Rais, Samia Hassan Suluhu na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, wamekuwa mstari wa mbele katika kutekeleza sheria hiyo na kuwataka mawaziri ambao hawajajaza fomu hizo kufanya hivyo haraka.

Jaji Kaganda aliyasema hayo jana Ikulu jijini Dar es Salaam, wakati wa semina ya siku moja kwa mawaziri na naibu mawaziri kuhusu sheria ya maadili, mgongano wa maslahi, mwongozo wa maadili ya viongozi wa umma na utekelezaji wa ahadi ya uadilifu.

Alisema majina ya mawaziri na manaibu hao yatakabidhiwa kwa Waziri Mkuu kwa hatua zaidi kwa kuwa walipaswa kuwa mstari wa mbele kujaza fomu hizo kabla ya watumishi wengine, lakini hawakufanya hivyo.

“Waziri Mkuu ameshasaini kiapo hiki na amekitundika ukutani ofisini kwake, anakisoma mara kwa mara. Nanyi mnatakiwa kuiga, kutosaini ni wazi kuwa mnapinga sheria hii,” alibainisha.

Alisema mawaziri waliorejesha fomu ya tamko na kutia saini ahadi ya uadilifu ni 15 kati ya 19 sawa na asilimia 78.9, ambao hawajarejesha ni wanne sawa na asilimia 21.1.

Upande wa naibu mawaziri, waliorejesha fomu za tamko ni 13 sawa na asilimia 81.3 na walio bado ni watatu sawa na asilimia 18.7, waliotia saini ahadi ya uadilifu ni 11 sawa na asilimia 68.7 na ambao bado ni watano ( asilimia 31.3).

Januari, mwaka huu, wakati wa kuwaapisha makatibu wakuu na manaibu, Rais alifuta utaratibu wa kiitifaki uliokuwa umetangazwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, wa kutia saini na kutaka kila mmoja kutamka kwa mdomo wake.

Katika hafla hiyo ya kuapishwa, makatibu wakuu na manaibu hao walitia saini kiapo cha uadilifu kilichoongozwa na Naibu Kamishna wa Maadili, Waziri Kipacha, na baada ya kukisoma kwa niaba ya viongozi hao aliwataka kutia saini na ndipo Rais alipoingilia kati.

“Hapana huwezi kula kiapo kwa niaba ya mtu mwingine wakati wenyewe wote wapo hapa. Kila mmoja aape kwa mdomo wake mwenyewe na kutia saini," alisema Rais Magufuli na kutoa angalizo:

"Kama kuna mmoja wao hajakubalina na kifungu kwenye hati hii tutajuaje?

“Kama yupo Katibu Mkuu au Naibu Katibu Mkuu anayeona kuwa hataweza kutekeleza mojawapo ya vifungu vilivyomo katika hati hiyo ya maadili akae pembeni, atuache wengine tuendelee.”

Katika semina hiyo, Jaji Kaganda alisema matarajio ya wananchi, viongozi wa umma watakuwa kioo na viongozi wazuri kwa manufaa ya wananchi na si kurushiana maneno hadharani na kutunishiana misuli.

Jaji Kaganda alisema Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya mwaka 1995, imeweka msingi wa kikatiba wa namna ya kujenga na kuimarisha viwango vya maadili na maadili ya kuzingatiwa na viongozi wa umma wakati wote wa kutekeleza majukumu yao katika uongozi wa umma.

“Mfano kiongozi wa umma anatakiwa kutoa tamko la rasilimali, maslahi na madeni, kutotumia vibaya rasilimali za umma, kujizuia na migongano ya kimaslahi, kutojilimbikizia mali na kutotumia madaraka vibaya,” alisema na kuongeza:

“Maadili hayo yamelenga kuhakikisha kuwa viongozi wa umma wanatekeleza majukumu yao kwa uadilifu, uaminifu, uwazi, haki, kutojipendelea na uwajibikaji ili kujenga, kuimarisha na kulinda imani ya wananchi kwa viongozi na serikali. Lakini mawaziri mnayo masharti ya ziada kwa mujibu wa sehemu ya nne, kifungu cha 17(10) cha sheria hiyo kuhusu uwajibikaji wa pamoja.”

MAWAZIRI WANATUMIA NGUVU
Aidha, alisema baadhi ya mawaziri waliopita walilalamikiwa na makatibu wakuu kwa kulazimisha kupewa fedha za matumizi binafsi na kiongozi huyo anapokataa kufanya hivyo “hujibiwa wewe ni Katibu Mkuu utajua mwenyewe, ninachotaka ni fedha.”

Aliwataka mawaziri kujiepusha na mambo hayo kwa kuwa yanasababisha mgongano wa maslahi na ni kinyume cha maadili ya viongozi wa umma na kwamba hawapendi kuwafikisha mbele ya Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma kuwaonyesha Watanzania lakini hulazimika kufanya hivyo inapobidi.

“Unaweza kuapa kuilinda katiba na sheria lakini kuitekeleza ni tatizo kubwa, ndiyo maana mnakumbushwa kwa ahadi za maadili,” alisisitiza.

UDANGANYIFU KATIKA FOMU
Jaji Kaganda alisema uchunguzi wa sekretarieti hiyo umebaini kuwa baadhi ya watumishi wa umma wanafanya udanganyifu katika fomu tamko la raslimali, maslahi na madeni kwa kubadili majina ya wamiliki wa mali husika.

“Unakuta jina la kiongozi ni Salome S. Kaganda, anatumia majina mawili ya mwisho kwa hoteli yake iliyoko jijini Mwanza. Huu ni udanganyifu na haukubaliki, ni lazima kumsaidia Rais ili kwenda sambamba na kasi yake,” alisema.

SEKRETARIETI YALIA UKATA
Aidha, alisema kutokana na bajeti finyu, sekretarieti imeshindwa kufanya uhakiki wa fomu ya tamko la rasilimali, maslahi na madeni ili kujua kilichojazwa ni sahihi. Alisema huko ndiko wanagundua mambo mengi kwa kuwa kama ni ardhi wanafuatilia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wakala wa Usajili wa Majina ya Biashara (Brela) na kwingineko.

“Kuna viongozi 15,379, watumishi wa sekretarieti hawafiki 200 nchi nzima. Tuna upungufu wa rasilimali fedha ndiyo maana tunalazimika kuomba msaada wa Marekani licha ya kwamba sheria hairuhusu,” alisema.

Alisema sekretarieti inapenda ifanye kazi zake kwa mujibu wa sheria lakini inakwamishwa na ufinyu wa bajeti. Alimwomba Waziri wa Fedha na Mipango, kulipa kipaumbele suala hilo katika bajeti ya mwaka 2016/17.

Kaganda alisema kutoa elimu ya maadili kwa viongozi wa umma na wananchi kwa ujumla ni moja ya majukumu yanayotekelezwa kupitia mafunzo kama hayo. Alisema sekretarieti inaamini elimu ni njia muafaka ya kukuza maadili ya viongozi kwa kuwa uwapo wa sheria pekee hautoshi.

Aidha, alitaja mamlaka ya sekretarieti hiyo ni kupokea na kusikiliza malalamiko kuhusu kiongozi yeyote wa umma, yawe ya mdomo au maandishi bila kuuliza majina wala anwani za walalamikaji, kuanzisha na kufanya uchunguzi wowote kuhusu ukiukwaji wa maadili yaliyotajwa katika sheria bila kusubiri kupokea malalamiko.

Mengine ni kukagua akaunti ya benki ya kiongozi pale inapotarajia kufanya uchunguzi kuhusu akaunti za benki ya kiongozi husika, kuruhusu watu kukagua daftari la rasilimali, maslahi na madeni ya viongozi wa umma na kumtaka kiongozi anayetuhumiwa kutoa tamko la uongo kuhusu raslimali zake kurekebisha au kuthibitisha tamko hilo.

Mada zilizowasilishwa katika semina hiyo ni sheria ya maadili, mwongozo wa maadili ya viongozi wa umma, mgongano wa kimaslahi na utekelezaji wa ahadi ya uadilifu ikiwa ni utekelezaji wa kukuza uelewa wa jamii kuhusu shughuli zinazotekelezwa na Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, unaofadhiliwa na Shirika la Misaada ya Maendeleo la Marekani (USAID).

Akifungua semina hiyo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alisema viongozi wanapaswa kutambua kuwa wanabeba dhamana ya umma au ya watu wanaowaongoza, hivyo uongozi ni cheo cha wajibu na huwajibika kwa matendo yao kwa wale wanaowaongoza.

“Pamoja na kwamba sisi ni viongozi, pia ni watumishi wa umma. Mtumishi ana wajibu wa kuwahudumia watu au jamii inayomzunguka. Mtumishi yeyote anapokubali kuwa mtumishi wa umma popote pale huo ni wajibu wake na analazimika kutumikia watu wote bila upendeleo wala kuhitaji ujira zaidi ya wajibu wake,” alisema.

Waziri Mkuu alisema kila kazi ina maadili yake na sheria ya maadili imeweka masharti maalumu kwa mawaziri na wakuu wa mikoa ambayo inasema waziri hatafanya jambo lolote linalopingana na dhana na uwajibikaji wa pamoja wa mawaziri kuhusu sera ya serikali na uendeshaji wa shughuli zake.

Alisema sheria hiyo inasema hataruhusiwa kupinga hadharani au kujiondoa katika uamuzi wowote unaofanywa na Baraza la Mawaziri, kutoa hadharani matamshi ya kumkosoa kiongozi mwenzake mwenye madaraka ya waziri na kutoa nje taarifa au zisizoruhusiwa za mijadala, uamuzi au nyaraka za Baraza la Mawaziri.

Alisema serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuondoa ucheleweshaji wa utoaji huduma, upendeleo, ubinafsi, rushwa na ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka na kwamba Rais hakusema hivyo wakati wa kampeni ili awarubuni wananchi kupata kura zao au sifa baada ya kushinda uchaguzi, bali serikali ina dhamira ya dhati ya kupambana na mambo hayo.

“Wote ni mashahidi kwamba tumeshaanza kuchukua hatua na tutaendelea hadi tutakapojiridhisha kwamba mambo yetu yanakwenda sawa kama tunavyotaka,” alisema Majaliwa.

Alisema wananchi wanachukia na wamechoshwa na rushwa na ufisadi kwa kuwa vinawanyima haki zao na kuitia hasara serikali kwa mamilioni ya fedha ambayo yangetumika kwenye miradi ya maendeleo na kwamba tatizo hilo litapungua iwapo kila mtumishi atazingatia sheria ya maadili na kuweka kipaumbele na umuhimu unaostahili kupambana na rushwa na ufisadi.

Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Angellah Kairuki, alisema lengo la mafunzo hayo ni kufikisha elimu kwa viongozi hao na itamfikia kila mwenye dhamana ya uongozi.

Alisema wizara yake imejipanga kusimamia sheria na kujenga misingi ya utawala bora, sambamba na mapambano dhidi ya rushwa.
CHANZO: NIPASHE

No comments: