Advertisements

Tuesday, February 9, 2016

Majangili 9 wanaswa na bunduki 29

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Lazaro Mambosasa
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Lazaro Mambosasa

POLISI mkoani Simiyu imewatia mbaroni watu tisa, wanaotuhumiwa kuwa ni majangili waliohusika na kifo cha rubani Mwingereza katika Pori la Akiba la Maswa, huku ikikamata bunduki 29 na meno ya tembo matatu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Lazaro Mambosasa alisema wamewakamata watuhumiwa tisa wa tukio la kuangusha helikopta pamoja na kusababisha kifo cha rubani wa ndege hiyo, Kapteni Gower Roger (24) ambaye mwili wake ulisafirishwa wiki iliyopita kwenda kwao kwa maziko.

Kamanda Mambosasa alisema walifanya msako mkali, uliowezesha kukamatwa watuhumiwa wawili ambao ni Shija Mjika (38) na Masasi Mandogo (48), waliofanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa wengine saba wa tukio hilo.

Alisema baada ya kukamatwa kwa watuhumiwa hao wawili, walitaja na kuonesha meno mawili ya tembo yenye kilo 31 aliyeuawa Januari 29, mwaka huu ambayo walikuwa wameyaficha kwenye daraja katika kijiji cha Itaba.

Alibainisha kuwa baada ya kukamatwa kwa watuhumiwa hao, Polisi iliwahoji na kukiri kuhusika na tukio hilo na kumtaja ambaye alifyatua risasi kwenye helikopta, ambaye ni Dotto Pangali (41) ambaye alikamatwa akitaka kujaribu kutoroka kwenda mkoani Shinyanga.

Kamanda Mambosasa alisema baada ya kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo, alikiri kutungua helikopta hiyo kwa kutumia bunduki ya Riffle yenye namba 7209460 CAR NA 63229 inayomilikiwa na Mange Balum ambaye kwa sasa anashikiliwa na Polisi.

Alisema baada ya upekuzi wa kina kwenye mji wa Pangali, kulipatikana bunduki aina ya Riffle yenye namba 3478 CAR Na 458 ikiwa na risasi sita, inayomilikiwa na Nghomango Jilala aliyekimbia na anaendelea kutafutwa.

Alifafanua kuwa katika operesheni hiyo pia waliwakamata watuhumiwa wengine ambao ni Njile Gonga (28), Iddi Mashaka (49), Mwigulu Kanga (40), Mapolu Njige (50) wote wakazi wa kijiji cha Sungu, Dotto Huya (45) mkazi wa kijiji cha Itaba pamoja na Mange Balum (47) pia mkazi wa Itaba wilayani Meatu.

“Katika msako huo tumefanikiwa kukamata bunduki 27 pamoja na risasi 141 ambazo zina wamiliki, ambao wamekuwa wakizikodisha silaha hizo kwa majangili kwenda kuulia tembo katika hifadhi za taifa na tumekamata Shot gun 11 na risasi 44, Riffle 10 na risasi zake 105 pamoja na magobole sita yakiwa na risasi mbili,” alisema Kamanda.

HABARI LEO

1 comment:

Anonymous said...

Tatizo la polisi wetu ni moja...inapotokea tatizo kama hilo utaona polisi wanafanya kazi kwa nguvu za soda wakikurupuka kukamata majambazi na majangili ambao polisi wanawafahamu badala ya kukamata wahusika moja kwa moja, ili kuonyesha kuwa wanafanya kazi.