ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, February 18, 2016

MAPAMBANO YA KUTHIBITI UHARIBIFU WA MISITU YAUNGWE MKONO NA SISI WOTE

Na. Ahmad Mmow.
Juhudi kubwa ya kufikisha elimu kwa jamii juu ya uhifadhi, usimamizi na uvunaji endelevu wa misitu iliyofanywa na serikali kwa kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali kupitia kampeni mbalimbali ikiwemo ya mama misitu inayofadhiliwa na nchi ya Finland imeanza kuzaa matunda.
Hifadhi ya Msitu
Baada vijiji kuanza kuhifadhi misitu, na wananchi kuunga mkono juhudi hizo baada yakuanza kunufaika na utunzaji huo.

Miongoni mwa vijiji ambavyo wananchi wake wameanza kunufaika na uhifadhi wa misitu ni kijiji cha Nanjirinji A, kilichopo wilayani Kilwa mkoani Lindi.

Wananchi wa kijiji hicho wameanza kunufaika na mpango huo kupitia mapato ya uvunaji wa mazao ya msitu wao wa Mbumbila.

Mwenyekiti wa serikali ya Kijiji hicho, Jafariri Nyambate alisema wameanza kutoa ruzuku kwa akinamama wajawazito wakazi wa kijiji hicho. Kila mjamzito hupewa shilingi 30,000 anapokaribia muda wake wakujifungua. Alisema.

Alise hilo nijambo moja kati ya mengi yaliyofanywa na kijiji hicho kwa wananchi kutokana na mapato ya msitu waliohifadhi unaojulikanakwa jina la Mbumbila.

Nyambate ambaye kijiji chake pia kimeweza kuwanunulia sare wanafunzi wa shule ya msingi ya kijiji hicho, kuchimba visima vya maji, kujenga soko la kijiji, madarasa, nyumba ya mwalimu, kuweka umeme jua kwenye shule ya kijiji hicho na kutoa ruzuku kwa akinamama wajawazito, alisema uenda mafanikio hayo yasiwe endelevu. 

Kutokana na uvamizi wa wakulima na wavunaji haramu unatishia kurudisha nyuma mafanikio hayo, kwani juhudi zakuwaondoa zimekuwa ngumu kufanikiwa kwasababu wakulima wamekuwa wakirejea kila unapofika msimu wa kilimo wa zao la ufuta.
"Wanatumia nguvu kulima ndani ya msitu na wanapambana na kamati yetu ya maliasili inapofanya doria, mara moja wamewahi kuwazidi nguvu walinzi wetu na kupora pikipiki," alisema Nyambate.

Kuhusu uvunaji haramu, Nyambate alisema wakulima na wavunaji haramu wengi wanatoka nje yakijiji na wilaya hiyo, akibainisha kwamba kuna mahusiano na ushirikiano mkubwa kati ya wakulima wavamizi na wavunaji haramu.
"Wakulima wengi wanaishi kwenye misitu ya hifadhi ya wazi ambayo inapakana na msitu wetu, wanawaongoza wavunaji haramu ambao mazao ya msitu wanayoiba wanahifadhi ndani ya vibanda vya wakulima hao," alisema Nyambate.

Ofisa mtendaji kata wa kata ya Nanjirinji, Haji Limba, alikiri kuwa mapato yanayotokana na msitu huo yamesababisha kuanza kuwa na uhakika wa ulinzi kwenye kata hiyo iwapo ujenzi wa kituo cha polisi kinachojengwa katika kata hiyo kitakamilika.

Alisema sehemu ya fedha zinazotumika katika ujenzi huo zilichangwa na kijiji hicho ambazo zilitokana na mauzo ya mazao ya msitu wa kijiji hicho.

Hata hivyo alibainisha kwamba wakulima wa ufuta na wavunaji haramu wnatishia kukwamisha mafanikio yaliyoanza kufikiwa.
"Hata hivyo juhudi kubwa inayofanywa na uongozi wa kijiji,kata,halmashauri ya wilaya na mkuu wa wilaya ya Kilwa zinapunguza kasi ya uvamizi wa wakulima hao na wavunaji haramu,maana msaada kutoka wilayani ni mkubwa sana," alisema Limba.

Naye mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Ngunichile wilayani Nachingwea, Seif Ng'wang'wa ambaye kijiji cha kimehifadhi msitu wenye ukubwa wa hekta 1296 unaojulikana kwa jina la Namitonga, alisema wavunaji haramu baada ya kumaliza miti katika misitu ya wazi ya vijiji jirani na kijiji hicho, wameanza kuvamia msitu huo.

Alisema kazi ya kuulinda imekuwa ngumu baada ya wavamizi kubadili mbinu."Tunajitahidi sana kufanya doria mchana, walipogundua kuwa mchana inawawia vigumu kufanya uhalifu wanafanya usiku," Alibainisha kuwa uharibifu unaofanywa na wavunaji haramu unatishia kufikiwa na kutekelezwa mipango ya maendeleo ambayo utekelezaji wake ulitegemea mapato ya mauzo ya mazao ya msitu huo.

Ofisa mtendaji wa kijiji hicho, Seleman Soya alisema licha ya wavunaji haramu lakini pia changamoto nyingine niwakulima kuvamia msitu huo.

Alisema."wavamizi niwengi nivugumu sisi wenyewe kukabiliana nao, watatushinda nguvu inahitajika nguvu kubwa kutoka serikalini vinginevyo watazidi kuumega,"alisema na kutahadharisha Soya.

Alisema migogoro ya mipaka baina ya vijiji hasa ambavyo havija hifadhi misitu inachangia kukwamisha wananchi kukosa matumaini ya kunufaika na msitu huo.

Bibi Arafa Batazari(80) mwananchi wa kijiji hicho, alisema licha ya wananchi kutarajia kunufaika na mauzo ya mazao ya msitu huo, lakini pia hali ya ukame inaweza kurejea katika maeneo hayo.
Maporomoko ya Maji
Anasema tangu waanze kuhifadhi misitu, ukame ulianza kupungua kutokana na mvua kunyesha mara kwa mara.
"Tulianza kupata mvua kama zamani, maana mito na vijito vilikuwa vinataririsha maji muda wote kwa sababu kulikuwa na miti kandokando ya mito na vijito" lakini wakulima walifyeka miti yote ikawa haitunzi wala haitirirish maji tena mvua ikaanza kuadimika," alisema bibi huyo.

Tatizo hilo lipo pia katika kijiji cha Miima, wilaya ya Lindi. Kaimu mwenyekiti wa kijiji hicho ambacho kimehifadhi msitu wenye ukubwa wa hekta 2262, Omari Katenda, alisema uvunaji haramu kwa kutumia misumeno ya moto umeshika kasi na kutishia uwepo wa msitu huo. 

Alisema hali ya msitu huo ni mbaya, aki taadhirisha zisipochukuliwa hatua za haraka kudhibiti kasi hiyo unaweza kutoweka.

Alisema baadhi ya wavunaji ambao leseni zao zinawaruhusu kuvuna kwenye misitu ya wazi wanavuna kwenye msitu huo bila kufuata taratibu na kwakutumia misumeno ya moto.

Mwenyekiti huyo ambae anakaimu baada ya viongozi wa awali wa kijiji hicho kuondolewa na wananchi kutokana na tuhuma ya kushindwa kudhibiti uvunaji haramu na kushirikiana na wavunaji hao.

Alisema hivi sasa wavunaji haramu wanapitia vijiji jirani ambavyo havija hifadhi misitu na kudai maeneo wanayovuna yapo nje ya kijiji na msitu huo. 

Aldophina Mbwago, mjumbe wa serikali ya kijiji hicho alisema uvunaji haramu unashamiri kutokana na kiwango cha adhabu wanachoadhibiwa wavunaji haramu.

Alisema udhaifu wa sheria uliopo unatumiwa na wavunaji kukiuka taratibu, kanuni na sheria.
"Wavunaji wanakutwa wametumia misumeno ya moto wanatozwa faini ya shilingi ya shilingi1,000,000 ambayo nikidogo ikilinganishwa na hasara na madhara yatayotokea baada ya nchi kugeuka kuwa jangwa," alisema.

Alishauri kosa la uvunaji haramu na kutumia misumeno ya moto liingizwe kwenye makosa ya uhujumu uchumi.

Tatizo hilo lipo pia katika kijiji cha Kiwawa katika wilaya hiyo ya Lindi. Diwani wa kata ya Kiwawa, Mohamed Mkulyuta, alisema msitu uliohifadhiwa na kijiji wenye ukubwa wa hekta 8896, upo katika hatari ya kutoweka kutokana na kasi ya uvunaji haramu unaofanyika.

Akibainisha kuwa mgogoro wa mipaka baina ya kijiji hicho na vijiji vya Namkongo na Mputwa unachangia kushamiri kwa uvunaji huo kwasababu wavunaji na wakulima wanasema maeneo wanayovuna na kulima yapo kwenye vijiji vya Namkongo na Mputwa.

Ahmad Tendele, mwananchi wa kijiji hicho, alisema msitu huo upokatika hatari ya kutoweka kutokana na kasi ya uvunaji haramu iliyopo kwenye msitu huo.
"Hali nimbaya sana kwenye msitu, lakini mgogoro wa mipaka kati ya kijiji na Mputwa na Mkongo unachangia uharibifu huu, na mpaka sasa hatujui serikali itamaliza lini mgogoro huu," alisema Tendele.

Baadhi ya viongozi na watendaji wa wilaya wamekiri kuwepo kwa tatizo hilo, huku wakieleza mikakati yao katika kudhibiti na kukomesha tatizo hilo.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Lindi, Oliver Vavunge alikiri kuwa tatizo la wavunaji haramu lipo pia katika vijiji vya halmashauri hiyo. Alisema kwa kutambua uzito wa tatizo hilo, halmashauri yake imetengeneza kikosi kazi kinachoundwa na watalamu kutoka katika idara mbalimbali za halmashauri hiyo.

Timu ambayo inafanya doria kwa kushirikiana na viongozi wa vijiji na kata inazotembelewa na timu hiyo, ambayo hupeleka taarifa zinazoelezea mafanikio na changamoto ya doria hizo kila wiki.

Alisema taarifa hizo husomwa na kuwekwa hadharani kila mwezi. Mkuu wa wilaya ya Lindi, Yahaya Nawanda, alisema anatambua umuhimu wa kuhifadhi na kuendeleza misitu.

Hivyo wamejipanga kukabiliana na wavunaji haramu na wakulima wanaovamia misitu ya hifadhi. Akionya kuwa kutakuwa na doria za mara kwa mara tena za kushitukiza, hata hivyo hakutakuwa na upendeleo wala ubaguzi kwa wale wote watakaokamatwa kupitia doria hizo au njia nyingine.
"Msako utakaofanyika hauta angalia cheo, hadhi wala madaraka ya mtu ambaye atabainika kutenda vitendo hivyo au kushiriki kufanikisha vitendo hivyo, maana kama sisi tumerithi misitu lazima jitihada zifanyike ili nasi turithishe kwa vizazi vijavyo," alisema Nawanda.

Kwa upande wake, mkuu wa idara ya ardhi na maliasili wa halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea, Lington Nzunda. Akizungungumzi kwa niaba ya mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, alisema halmashauri inamikakati na mipango mingi ya kuhakikisha kasi ya uvamizi wa misitu na uvunaji haramu unapungua kama siyo kwisha kabisa.

Miongoni mwa mipango aliyoisema na kuitaja ni pamoja na kuvihamasisha vijiji na kuviwezesha ili viingie kwenye mpango wa matumizi bora ya ardhi. Akibainisha kuwa wananchi wakianza kuona faida ya kuhifadhi misitu, watakuwa walinzi wazuri wa misitu hiyo na kuongeza kusema;
"Wananchi wanawatambua wavunaji na waharibifu wengine wa misitu kwa sababu wengine wanaishi nao, lakini hawawafichui ," alisema Nzunda.

Aliutaja mkakati mwingine ambao umeanza kutekelezwa ni Halmashauri hiyo kutoa mafunzo kwa askari wa vijiji, ambao watakuwa wanashirikiana na kamati za maliasili za vijiji kufanya doria kwenye Misitu yote iliyo kwenye maeneo ya vijiji. 

Uenda tatizo la uharibifu wa misitu halipo katika vijiji hivyo tu hapa nchini. Unaposikiliza maelezo ya wananchi na viongozi wa vijiji unagundua kuwa baadhi ya wananchi wameanza kutambua faida za kuhifadhi misitu na hasara zinazotokana na uharibifu wa misitu.

Kwa upande mwingine mipango na mikakati ya serikali katika kudhibiti na kukabiliana na uharibifu wa misitu. Jambo lililomuhimu kwetu wote nikusaidia mapambano hayo kwa nafasi zetu. Kwani madhara ya uharibufu huo hayataishia kwa wananchi wa vijiji hivyo wala kwa watendaji na viongozi wa serikali, bali kwetu sote. MWISHO

No comments: