By Habel Chidawali, Mwananchi hchidawali@mwananchi.co.tz
Lakini mbunge huyo, ambaye aligoma kufuta kauli yake kuhusu tuhuma hizo kabla ya kupewa adhabu, alisema ana uhakika na alichokisema na yupo tayari kwa adhabu yoyote.
Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge, ambaye alisoma uamuzi huo wa Spika Job Ndugai bungeni jana, alisema muda ambao Bunge lilimpa Kishoa kuwasilisha uthibitisho wa tuhuma dhidi ya Dk Mwakyembe kuhusu ununuzi wa mabehewa ya Sh238 bilioni, ulishaisha bila ya kufanya hivyo.
Akichangia mjadala wa Mwelekeo wa Mpango wa Serikali mwanzoni mwa wiki hii, Kishoa alimtaja Dk Mwakyembe, ambaye wakati wa ununuzi wa mabehewa hayo alikuwa Waziri wa Uchukuzi, kuwa ni jipu lililochukuliwa upande mmoja na kupelekwa upande wa pili, hivyo linatakiwa kutumbuliwa na Rais John Magufuli.
Mbunge huyo alisema katika sakata la mabehewa, Samuel Sitta, ambaye baadaye aliteuliwa kuongoza wizara hiyo aliunda tume maalumu ya kuchunguza kashfa hiyo baada ya kubaini kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa Sheria ya Ununuzi wa Umma.
“Fedha zilitumika, ripoti iliundwa na taarifa zipo, lakini kwa nini hamtaki kuitoa ili umma wa Watanzania na wabunge tujue kilichoandikwa kwenye ripoti hiyo? Mwakyembe ni tatizo na ndiye mhusika mkuu katika sakata hili wala tusidanganyane,” alisema Kishoa.
Mvutano wa wawili hao, uliingiliwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Bunge), Jenister Mhagama na baadhi ya wabunge wa upinzani akiwamo Halima Mdee, jambo lililofanya kuwa mkali na hivyo Dk Mary Mwanjelwa, aliyekuwa mwenyekiti wa Bunge siku hiyo, na kumwamuru Kishoa atoe uthibitisho ndani ya siku tatu.
Hadi jana, mbunge huyo hakuwa amewasilisha ushahidi huo wala maelezo aliyokuwa ameyapeleka kwa Spika na alipoambiwa afute kauli yake alikataa kwamba hakuwa tayari hadi Mwakyembe apeleke uthibitisho wa bei za kununulia mabehewa hayo.
Katika kikao cha Jumanne, Mdee aliibua tena hoja hiyo na kusababisha Dk Mwakyembe atoe taarifa kuwa wakati wa ununuzi, mikataba huwa na kipengele kinachomlinda mnunuzi (defect liability period) ambacho hutumiwa kutathmini ubora wa bidhaa.
Alisema baada ya mabehewa hayo kuwasili nchini, kuliibuka tuhuma hizo na aliunda kamati iliyochunguza na kuibua suala hilo.
“Baadaye tuliwaita waliotuuzia na walitengeneza. Kwa hiyo tukimwambia Halima leo atuonyeshe behewa lililo bovu, hataweza,” alisema Dk Mwakyembe.
Nje ya Bunge
Akiwa nje ya viwanja vya Bunge, Kishoa alitetea msimamo wake, akisema hata kama angepewa adhabu kubwa zaidi ya hiyo, asingeogopa kwa kuwa anachokisimamia ni masilahi ya Taifa lake na wananchi.
“Bunge halikutakiwa kulinda Serikali. Wanajua kuwa mwaka jana Samuel Sitta aliunda kamati, ambayo hadi sasa hakuna majibu yoyote na kwa nini wasilete ripoti ndiyo imsafishe Mwakyembe badala ya kuendelea kulindana?” alihoji.
Alisema ripoti ya PPRA ilithibitisha mabehewa hayo yalikuwa ni mabovu na gharama iliyotumika ilikuwa kubwa, huku ununuzi zikiwa mbovu kwa kuwa walilipa kwa asilimia 100 hata kabla mabehewa nchini.
Pia, alihoji kitendo cha Bunge kuamini kauli za Dk Mwakyembe bila ya ushahidi na kukataa kuamini maneno yake, huku akisikitika kwa kile alichosema kunyimwa ripoti ya uchunguzi huo na Kamati ya Viwanda na Biashara.
No comments:
Post a Comment