MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeridhia waliokuwa Mawaziri wastaafu Basil Mramba na Daniel Yona kutumikia adhabu ya kifungo cha nje kwa kufanya usafi katika maeneo ya kijamii ikiwemo Hospitali ya Sinza Palestina.
Hatua hiyo inatokana na Mramba ambaye alikuwa Waziri wa Fedha na Yona aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, kupitia Mawakili wao kuwasilisha barua mahakamani hapo kutoka Magereza kuhusu kutumikia kifungo cha nje.
Mawaziri hao wa zamani waliwasilisha barua hiyo ya kuitaarifu mahakama yenye kumbukumbu namba 151/DA/3/11/223 ya Desemba 5, mwaka jana, wakiongozwa na jopo la mawakili wao watatu Peter Swai, Cuthbert Nyange na Elisa Msuya.
Katika barua hiyo waliyoiwasilisha kwa Hakimu Mkazi Mfawidhi Cyprian Mkeha ilikuwa na kichwa cha habari kisemacho ‘Wafungwa wenye sifa ya kutumikia vifungo vyao chini ya Mpango wa Huduma kwa Jamii”.
Hakimu Mkeha alisema mchakato huo ulianza baada ya Magereza kuwasilisha barua hiyo mahakamani hapo kwa kupeleka majina ya watu wanaotumikia kifungo cha nje ikiwemo mawaziri hao.
Alisema mahakama haihusiani na mchakato huo, kwani ilishamaliza kazi yake ya kuhumu, hivyo jukumu la kutumikia kifungo cha nje ni kazi ya Magereza.
“Baada ya kuleta barua hiyo kisheria mahakama inaishinikiza Ustawi wa Jamii ili ifanye uchunguzi kutokana na majina yaliyowasilishwa mahakamani,”alisema.
Hakimu Mkeha alisema kupitia barua hiyo, Mawaziri hao wa zamani wamepangiwa kutumikia adhabu ya kufanya usafi kwenye Hospitali ya Sinza Palestina kwa saa nne za kila siku.
Alisema awali kabla ya mahakama kuridhia adhabu hiyo, iliwaita Mawaziri hao kwa ajili ya kuwahoji kama wameridhia na adhabu watakayopangiwa sambamba na vipengele vinavyowahusu.
“Kutokana na barua hiyo mahakama ikaona ni vyema kuwaita wahusika wenye ambapo tuliwahoji kama wanaridhia kutumikia adhabu hiyo, ambapo walikubali ndipo tukaridhia,”alisema.
Kuhusu masharti yaliyotumika kuwapatia kifungo hicho, alisema kinatokana na sheria ya Jamii namba 6 ya mwaka 2002, kifungu cha 3(1).
Alisema baadhi ya vigezo vinavyotumika kwa wafungwa kutumikia adhabu ya nje ni muangalio wa ripoti yao ilikuwa inasemaje, umri, washtakiwa kama walishawai kutiwa hatiani, makosa namna yalivyo, kama wanafamilia, pia kama wanakubali kuitumikia jamii, kama wana ajira, tabia za mshtakiwa na umbali wa eneo analokaa na anapofanyia adhabu hiyo.
Inakumbukwa kuwa Oktoba 2, 2015 katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ilitoa hukumu ya rufaa dhidi ya mawaziri wastaafu, Basil Mramba na Daniel Yona ambapo Jaji Projest Rugazia, alikubaliana na hoja kwamba kwa mujibu wa mashtaka yaliyowatia hatiani kwa matumizi mabaya ya Ofisi na kwa mujibu wa kifungo cha 35 cha adhabu PC ambacho Mahakama ilikitumia walipaswa kupewa adhabu ya kutumikia kifungo cha miaka miwili na si miaka mitatu.
Katika rufani hizo, Mramba na Yona, waliwasilisha hoja tano kupinga hukumu iliyotolewa Julai 6, mwaka jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, na jopo la Mahakimu watatu, likiongozwa na John Utamwa.
Aidha DPP alipinga adhabu waliyopewa mawaziri hao kwa madai ni ndogo, pia hakimu alikosea kumuachia huru aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Gray Mgonja na pia iliiomba mahakama iamuru washtakiwa walipe fidia ya fedha walizosababisha hasara.
Katika uamuzi huo Jaji Rugazia alikubali hoja ya kina Mramba kuwa walipewa adhabu mbili kwa kosa moja.
“Haikuwa sahihi kuwashitaki kwa kosa la kusababisha hasara wakati kosa hilo lilishakuwa kwenye makosa mengine ambayo ni la tano hadi la 10,” alisema.
Aidha, alisema Yona aliunganishwa kimakosa katika shtaka hilo, hivyo alifuta shitaka hilo pamoja na adhabu ya kifungo cha miaka mitatu jela na faini ya Sh milioni tano iliyotokana na kosa hilo.
“Ninaondoa shitaka la kusababisha hasara, ninafuta adhabu ya kifungo cha miaka mitatu jela na faini ya Sh milioni tano, hivyo Yona na Mramba watatumikia kifungo cha miaka miwili kwa kila kosa,“ alisema.
Katika uamuzi huo, Jaji Rugazia alisema, “Nakubali Kifungu cha 6 cha Kanuni ya Adhabu kinachotaka mahakama itoe amri washitakiwa walipe fidia, lakini siwezi kutoa amri hiyo.”
Pia alikataa hoja za kina Mramba kuwa hati ya mashtaka ni batili, pia alisema hakukuwa na njama zozote kwa upande wa Jamhuri kutoita mashahidi waliosaini mkataba huo ili kuathiri upatikanaji wa haki, kwa kuwa utetezi walikuwa na haki ya kuomba watu hao wawe mashahidi wao.
Alisema wasitumie maelezo ya aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, kuficha kosa kwa kuwa alitoa maelekezo kutokana na barua aliyoipata kutoka kwa Mramba na hakujua kama tayari Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) ilishatoa angalizo la kutokutoa msamaha huo.
Kwa upande wa Mgonja, Jaji Rugazia alisema anahalalisha kuachiwa kwake huru baada ya kutopatikana na hatia. Alisema, “Siwezi kuilaumu mahakama kwa kumuachia huru”.
Katika hukumu hiyo, mawaziri hao walihukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela na kulipa faini ya Sh milioni tano, baada ya kupatikana na hatia ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 11.7.
Kwa mara ya kwanza washtakiwa hao walifikishwa mahakamani mwaka 2008, wakikabiliwa na mashtaka ya kuisababishia serikali hasara ya kiasi hicho cha fedha kutokana na kutoa msamaha wa kodi kwa Kampuni ya kukagua madini ya dhahabu ya M/S Alex Stewart ya Uingereza.
3 comments:
kweli ccm inafanya kazi...walio iba kuku bado wako ndani hawa wamtia hasara billion eti leo wako free...kidumu
Chama cha mapinduzi oyeee!
Hivi inamaana katika uongozi wa awamu ya 4 hawa tu ndio walikuwa wahujumu uchumi? au ?
Post a Comment