Alisema hayo jana wakati wa kikao chake na watendaji wa Tanesco na taasisi nyingine zilizo chini ya wizara hiyo, kilichofanyika katika kituo cha kuzalishia umeme cha Mtera.
Profesa Muhongo alitaja maagizo hayo kuwa ni kuunganisha huduma kwa wateja wengi, kuwa na makusanyo makubwa ya ankara za umeme, kupunguza manung’uniko ya wananchi katika huduma za umeme na uboreshaji wa mawasiliano kati ya Shirika hilo na wananchi.
“Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, ifikapo Machi mosi mwaka huu atatuthibitishia kama mameneja hawa wataendelea na majukumu haya wanayosimamia ama la, na hii itatokana na ufanisi wa utendaji katika majukumu tuliyowapangia,” alisema Profesa Muhongo.
Mbali na mameneja hao, Profesa Muhongo ameagiza Kitengo cha Uwekezaji cha Tanesco, kama hakitakuwa na miradi mipya ya umeme ifikapo Aprili 2 mwaka huu, watendaji katika Ofisi hiyo waondolewe katika nafasi hiyo kwa kushindwa kutimiza majukumu yao ipasavyo.
“Hapa hatuna mzaha kwani mahitaji ya umeme ni makubwa na tuna miradi mingi ya usambazaji umeme kwa wananchi ikiwemo miradi ya Rea (Wakala wa Umeme Vijijini). “Wananchi wanahitaji umeme kwa matumizi ya majumbani na kuanzisha viwanda vidogo, sasa bila miradi mipya ya umeme, tutashindwa kusambaza umeme kwa wananchi hawa kwa kuwa kiasi cha umeme tulichokuwa nacho sasa bado hakitoshi,” alisema Profesa Muhongo.
Profesa Muhongo pia aliwaasa mameneja wa Tanesco wa Kanda, kukaribisha wawekezaji mbalimbali wa umeme ikiwemo miradi midogo ya uzalishaji umeme wa maji, ili nchi iwe na umeme wa kutosha badala ya kuwakatisha tamaa wawekezaji hao.
Alionya watumishi watakaoleta urasimu katika kujadili masuala ya uwekezaji wa nishati, wataachia ngazi kwani ndio wanaokwamisha juhudi za Serikali katika kuongeza kiasi cha umeme nchini.
“Tanesco na Ewura (Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji) kwa sasa pale anapojitokeza mwekezaji wa miradi ya umeme, lazima mjadiliane naye kwa pamoja badala ya mwekezaji husika kwenda Tanesco na baadaye Ewura au TPDC (Shirika la Maendeleo ya Petroli). “Hivyo mwekezaji anapokuja, jadilini naye kwa pamoja ili msitumie muda mrefu katika utekelezaji wa suala moja na hivyo kuchelewesha utekelezaji wa miradi mbalimbali,” alisema Profesa Muhongo.
Pia amewaagiza watendaji wa TANESCO katika vitengo vya ukaguzi, kufanya kazi hiyo kwa ufanisi mkubwa ikiwemo usimamizi madhubuti wa nguzo za umeme, ambazo baadhi huanguka kila inapofika msimu wa mvua na kusema kuwa suala hilo halikubaliki.
Hatua hiyo ya Profesa Muhongo, imelenga kutekeleza malengo ya Wizara hiyo kuhakikisha asilimia 67 ya vijiji vyote nchini, vitapata umeme katika miaka miwili na nusu ijayo. Mbali na kuunganisha watu wengi na huduma hiyo, juhudi kuongeza uzalishaji wa umeme, Profesa Muhongo alizieleza mara tu alipoapishwa kushika wadhifa huo Desemba mwaka jana.
Katika hafla hiyo, Profesa Muhongo alisema Tanzania ina vyanzo vingi vya kuzalisha umeme, lakini bado umeme unaozalishwa hautoshi na kuwataka wawekezaji wenye uwezo watumie fursa hiyo kuwekeza katika sekta hiyo.
Aidha alisisitiza kuwa ili Taifa lifanikiwe kuwa nchi yenye kipato cha kati kufikia mwaka 2025, ni lazima nchi iwe na umeme wa kutosha, hivyo hadi kufikia mwaka huo, uzalishaji wa umeme unapaswa kufikia megawati 10,000.
HABARI LEO
1 comment:
Safi sana maana hii kero ya mgao wa umeme umezidi sana hadi inaudhi
Post a Comment