Monday, February 29, 2016

Nitashinda urais uchaguzi wa maruidio Zanzibar'

Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha ACT- Wazalendo, Khamis Iddi Lila

Pamoja na chama chake kumpiga ‘stop’, mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha ACT- Wazalendo, Khamis Iddi Lila, amesema amekuwa akiomba dua usiku na mchana aibuke mshindi katika uchaguzi mkuu wa marudio uliopangwa kufanyika Machi 20, mwaka huu visiwani humo na kwamba ina imani atashinda urais.
Lila amesema ana matumaini makubwa ya chama chake kufikia malengo makubwa ya kisiasa visiwani humo baada ya kuibuka mvutano baina ya vyama vikuu vya CCM na CUF juu ya uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu na matokeo yake kufutwa na kusababisha CUF kususia uchaguzi huo wa marudio.

Akizungumza mjini hapa mwishoni mwa wiki, Lila alisema mvutano wa CUF na CCM una tija kubwa kwa vyama vingine vinavyoshiriki uchaguzi huo kama wananchi watakubali kufanya mageuzi ya kukomesha ukiritimba wa kisiasa katika visiwa vya Zanzibar baina ya vyama hivyo viwili.

Alisema pamoja na viongozi wa chama chake kutangaza kumsimamisha uanachama kutokana na kushiriki uchaguzi huo wa marudio, bado anajitambua kuwa mgombea halali baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, kueleza kuwa wagombea wote walioshiriki uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka jana ni wagombea halali katika uchaguzi wa marudio.

“Mvutano wa CUF na CCM una neema na tija kubwa kwa vyama vilivyobakia, ndiyo maaana naomba dua usiku na mchana nishinde urais wa Zanzibar,” aliongeza kusema Lila.

UONGOZI WAMKANA
Hata hivyo, uongozi wa chama ACT -Wazalendo Zanzibar haumtambui Lila kama mgombea wake na kama anashiriki uchaguzi huo atasimama kama mgombea binafsi.

Msimamo huo ulitolewa na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Juma Said Sanani, mjini Zanzibar jana, baada ya mgombea huyo kugoma kujitoa katika uchaguzi huo wa marudio.

Alidai Lila amefukuzwa uanachama wa ACT-Wazalendo kutoka na na kwenda kinyume na msimamo wa chama hicho wa kususia uchaguzi huo wa marudio.
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

Ndg Khamisi Iddi nadhani kwa mtizamo wako na kwa aliyekuagiza kusema hayo mwenyekiti wako wa chama, inaonyesha wazi kabisa jinsi vyama visivyotaka hakki kuwepo, na isitoshe chama tawala kinawarubuni kuingia kwenye uchaguzi wakti fika mnaelewa na wew mwenyewe unajua huwezi hata kupata asilimia 12 ya uchaguzi huo!! haya ni maajabu, kwani CCM hawataki kuambiwa kitu wao wanajiona wao ndio wao na kushiriki kelu uchaguzi huu ni wazi kwamba wamewaomba na kuwarubuni ili wao waweze kupit kwa kutumia mbinu zile zile zilizotumika bara. Hebu siasa mnazoziendesha zikidhi matakwa na washiriki.

nimepita tu sikutakiwa kutua.