ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, February 17, 2016

Nyumba 160 za vigogo kubomolewa Moshi

By Daniel Mjema,Mwananchi dmjema@mwananchi.co.tz

Moshi. Nyumba za kifahari zaidi ya 160 za vigogo wa taasisi za Umma na wastaafu katika Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro zinatarajiwa kubomolewa kutokana na kujengwa maeneo ya hifadhi ya vyanzo vya maji.

Nyumba hizo zimejengwa ndani ya mita 60 katika mto Karanga kuanzia eneo la Shanty Town na mto Rau huku nyingine zikijengwa katika vyanzo vya maji kata ya Njoro.

Miongoni mwa nyumba zinazotajwa kujengwa ndani ya mita 60 ni za kigogo mmoja mstaafu wa Jeshi la Polisi, wafanyabiashara mashuhuri na nyingine ujenzi wake ukianza.

Akizungumza kwa niaba ya mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, Jeshi Lupembe, Ofisa Mipango Miji wa Halmashauri, Speratus Rutagenya, amethibitisha kuanza kwa mchakato huo.

“Zoezi la kwanza lilikuwa ni ku- identify (kutambua) watu walioingia ndani ya mita 60 na tumebaini nyumba zaidi ya 100 mto Karanga na nyingine 60 kule mto Rau naNjoro.”amesema.

Ofisa Mipangao miji huyo amesema zoezi hilo limeingia hatua ya pili ambayo ni kuwabaini kwa majina wamiliki wa nyumba hizo na zoezi hilo linatarajiwa kuwa limekamilika kufikia kesho kutwa Ijumaa.

Kwa mujibu wa Ofisa huyo, pamoja na sheria kuwa wazi na Serikali kutangaza bomoabomoa, bado wapo watu ambao wameanza ujenzi upya ndani ya mita 60.

“Tunachofanya sasa hawa wanaoanza ujenzi sasa tumewapelekea stop order (zuio) na wale wote waliojenga ndani ya mita 60 au kwenye vyanzo vya maji tutawapa notisi tukikamilisha,”amesema.

Desemba mwaka jana, mkuu wa wilaya ya Moshi, Novatus Makunga, alisema Serikali ilikuwa ikikamilisha mchakato wa kuzibaini nyumba zilizojengwa kwenye vyanzo vya maji ili kuzibomoa.

No comments: