Advertisements

Saturday, February 27, 2016

POLISI WAZIMA VURUGU ZA WAMACHINGA MKOANI MBEYA

 Jeshi la Polisi mkoani Mbeya, limelazimika kutumia mabomu ya machozi kuzuia hali ya taharuki iliyokuwa imezuka katika maeneo ya Mwanjelwa, Kabwe hadi Soweto, jijini Mbeya, kufuatia vurugu zilizoambatana na uchomaji matairi zilizokuwa zikifanywa na wafanyibiashara ndogondogo, maarufu kama wamachinga.
 Chanzo cha sakata zima, kilikuwa zoezi lililoendeshwa na Halmashauri ya Jiji la Mbeya, la kuvunja vibanda vya wamachinga katika maeneo hayo, zoezi ambalo lilifanywa usiku wa kuamkia leo hii Februari 27.
Chanzo kimoja cha habari kimemueleza mwandishi wa mtandao huu kuwa, zoezi hilo lilifanywa ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa Jiji la Mbeya, kuweka mazingira yake katika hali ya usafi, huku ikidaiwa kuwa, wafanyibiashara hao, walishaelezwa mara kadhaa kuondoka katika maeneo hayo, lakini wakakaidi agizo la Jiji.

 Hata hivyo, kitendo cha kufanyika kwa zoezi hilo usiku, kimewakera wafanyibiashara hao, ambao wamedai kupata hasara kubwa kutokana na kuwa baadhi ya vibanda vilikuwa na mali zao na kwamba zimeharibiwa na mgambo wa Jiji, walioendesha zoezi hilo usiku.
Mapema asubuhi ya leo, wafanyibiashara hao wanaodai kuwa hawakuwa na taarifa za kuwataka kuondoka katika maeneo hayo, sanjari na kutokuwa na taarifa za ubomoaji huo wa vibanda, walipigwa na butwaa walipofika katika maeneo hayo wanakofanyia shughuli zao na kukuta vibanda vyao vimebomolewa huku kukiwa na mafungu ya masalia ya mbao za vibanda vyao.
Kufuatia hali hiyo, walihoji ni kwanini hatua hiyo ilifanyika, na baada ya kujibiwa kuwa Jiji walikuwa wakiendelea na usafi, nao wakaamua kukusanya mbao na masalia mengine ya vibanda vyao, na kulundika katika barabara kuu ya lami inayopita katika maeneo hayo, na kisha kuwasha moto mkubwa, wakieleza kuwa nao walikuwa wakifanya usafi.
Hali hiyo ikazua tafrani, ambapo njia hiyo pekee inayotumiwa na mabasi ya kwenda mikoani, pamoja na malori yatokayo na kuingia jijini Mbeya, ilifungwa kwa muda, hatua ambayo ilililazimu Jeshi la Polisi kuingilia kati na kutumia nguvu ili kutawanya makundi ya wafanyibiashara hao, pamoja na kuzima moto uliokuwa ukiendelea kuwaka na kuharibu lami.
Vurugu hizo zikadumu kwa muda, hadi Polisi walipofanikiwa kuzizima na kuweka hali ya utulivu, ingawa shughuli za kibiashara zilikuwa zimesimama kutokana na vurugu zenyewe, na tishio la wamachinga kwa wafanyibiashara wenye maduka rasmi katika maeneo hayo.
Baadhi ya wamachinga walioongea na mwandishi wa habari hizi, wamelalamikia Jiji kwa uonevu huo, lakini pia wakadai kuwa wenye maduka katika eneo hilo, ndio waliowachongea hadi kuingizwa hasara kwa kiasi hicho, na hivyo wakadai hawaoni sababu ya kuwaacha nao wafungue maduka yao, kwakuwa hawana ushirikiano nao.
Aidha, wameonya juu ya hatua hiyo, kuwa inaweza kupelekea vitendo vya uporaji na upigaji nondo, kuibuka upya jijini hapa, kwani ubomoaji huo, utasababisha kundi kubwa la vijana waliokuwa wakitegemea vibanda hivyo kujipatia riziki, kurudi mtaani wakiwa hawana shughuli maalum za kuwawezesha kuendesha maisha yao.

CHANZO: YANAYOJIRI BLOG

No comments: