Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (mbele katikati), akiongea jambo wakati wa kikao kati yake na wawekezaji katika Sekta ya Nishati, katika Ukumbi wa Tanesco, Jijini Dar es Salaam. Kulia kwa Waziri ni Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Julieth Kairuki.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, akiongea jambo na baadhi ya wawekezaji mara baada ya kikao chake na wawekezaji ambao wameonesha nia kuwekeza katika vyanzo mbali mbali vinavyopatikana nchini na baadhi wamefika kupata taarifa kuhusu uwekezaji.
Baadhi ya Watendaji kutoka Taasisi zilizo chini ya Wizara na Maafisa kutoka Wizarani wakifuatilia kikao kati ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Muhongo na Wawekezaji katika Sekta ya Nishati,
Baadhi ya Wawekezaji wakiwasilisha taarifa zao za uwekezaji kwa Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (hayupo pichani). Baadhi ya maswali ambayo Profesa alihoji kutoka kwa wawekezaji hao wao ni uwezo wao kifedha, kiteknolojia,utaalam na uzoefu wa kazi katika vyanzo walivyochagua kuwekeza nchini.
Asteria Muhozya na Nuru Mwasampeta, Dar es Salaam
Kutokana na mahitaji makubwa ya Nishati ya umeme barani Afrika, ambapo kiasi cha wananchi wake wapatao bilioni 1 wanatajwa kuwa bado wapo gizani Tanzania ikiwa miongoni mwao, imeelezwa kuwa, wawekezaji katika sekta hiyo wanavyo vyanzo vya uhakika vya kupata fedha za uwekezaji.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo wakati wa mwendelezo wa vikao vyake na wawekezaji katika sekta ya Nishati vilivyoanza tarehe 15-18 Februari, 2016, ambavyo vililenga kukutana na wawekezaji wenye nia ya kuwekeza katika vyanzo mbalimbali vya nishati vinavyopatikana nchini ili kuhoji na kubaini kampuni ambazo ziko tayari na zina uwezo wa kuwekeza.
Prof. Muhongo amevitaja vyanzo hivyo kuwa ni pamoja na Mpango wa Serikali ya Marekani kusaidia maendeleo ya sekta ya umeme barani Afrika unaoitwa ‘Power Africa Initiative’ ambao umetengewa Dola za Marekani Bilioni 6 ambapo Tanzania ni moja ya nchi zinazopewa kipaumbele katika mpango huo.
Aidha, ameongeza kuwa, Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo ipo katika nafasi nzuri ya kufaidika na fedha za Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Nishati Endelevu kwa Wote (SE4ALL) ambapo mpango huo unaelekeza kuwa, ifikapo mwaka 2030 kuwe na upatikanaji umeme kwa wote na ongezeko maradufu la utumiaji umeme wa nishati jadidifu na matumizi bora.
Pia, Profesa Muhongo ameeleza kuwa, kutokana na mahitaji ya umeme Duniani kupanda kwa asilimia 26 tayari kiasi cha Dola za Marekani trilioni 48 zimetengwa, ili kuongeza kiasi cha watumiaji wa nishati hiyo ifikapo 2020-2035, ambapo dola za Marekani trilioni 40 zikiwa zimetengwa kwa ajili ya kusambaza umeme na kiasi cha dola za Marekani trilioni 8 kwa ajili ya matumizi bora ya nishati.
Vilevile, ameutaja mpango wa ‘China Afrika Partnership’ ambapo kiasi cha Dola za Marekani bilioni 60 zimetengwa kwa ajili ya miundombinu , huku nishati ikipewa kipaumbele na kuongeza kuwa, kutokana na urafiki wa muda mrefu na mahusiano mazuri kati ya Serikali ya Tanzania na Watu wa China, Tanzania iko katika nafasi nzuri za kupata fedha hizo.
Halikadhalika, Profesa Muhongo ameleeza kuwa, Umoja wa nchi za Ulaya (European Union) pia ni chanzo kingine kwa wawekezaji kupata fedha kwa kuwa, nishati imekuwa kipaumbele kwa taasisi hiyo.
“Wawekezaji makini macho yote sasa yapo Afrika. Tunataka fedha hizo zote zije Tanzania kuwekeza katika sekta ya nishati. Jipangeni vizuri mwende, ‘Power Africa’ na sehemu nilizotaja, fedha za uhakika za umeme zipo. fedha,”amesisitiza Prof. Muhongo.
Aidha, kutokana na umuhimu na uharaka wa kutekeleza mipango hiyo, Profesa Muhongo amewataka wawekezaji ambao wako tayari kuwekeza nchini kuzingatia muda na ratiba ya kutekeleza majukumu yao na kuongeza kuwa, “ikiwa kuna jambo litacheleweshwa na watendaji wa Serikali, tutachukua hatua, na ikiwa mwekezaji umeshindwa kwenda na muda wetu vizuri basi mradi wako utaachwa na wengine kupewa nafasi,”ameongeza Muhongo.
Profesa Muhongo amebainisha kuwa fursa za uwekezaji katika sekta ya nishati zinapatikana katika maeneo ya gesi asilia, makaa ya mawe, nishati jadidifu umeme wa maji, upepo, umeme wa jua biogas na vyanzo vingine.
No comments:
Post a Comment