JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mama Mwantumu Mahiza,
kufuatia vifo vya watu 11 waliopoteza maisha katika ajali ya barabarani
iliyosababishwa na Basi la Kampuni ya Simbamtoto kugongana uso kwa uso na Lori
lililobeba mchanga katika eneo la Pandamlima, Wilaya ya Muheza Mkoa wa Tanga.
Ajali hiyo imetokeo leo tarehe 11
Februari, 2016 majira ya saa 1:15 asubuhi katika eneo hilo lenye mteremko,
ambapo basi la Kampuni ya Simbamtoto lilikuwa likisafiri kutoka Tanga kwenda
Dar es Salaam na Lori lililokuwa limebeba mchanga, lilikuwa likielekea kiwanda
cha Saruji cha Tanga.
Rais Magufuli amewapa pole Ndugu, Jamaa na
Marafiki wote waliofikwa na msiba huo na amewataka kuwa wavumilivu na
wastahimilivu katika kipindi hiki kigumu.
"Nimepokea taarifa ya vifo hivi kwa
mshituko mkubwa, na kupitia kwako Mkuu wa Mkoa wa Tanga, napenda kuwapa pole
nyingi wote waliofikwa na msiba huu mkubwa na naungana nanyi katika kipindi
hiki kigumu cha maombolezo" alisema
Rais Magufuli.
Dkt. Magufuli amewaombea marehemu wote wapumzishwe mahali pema peponi, na amewapa pole majeruhi wote 21 walioumia katika ajali hii.
Aidha, Rais Magufuli amewakumbusha
watumiaji wote wa barabara hususani madereva wa vyombo vya moto, kuwa makini
watumiapo barabara kwa kuzingatia sheria zote zinazosimamia usalama barabarani
ili kuepusha ajali.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam.
11 Februari, 2016.
No comments:
Post a Comment