Advertisements

Sunday, February 28, 2016

Rais Kenyatta apingwa Israel


Jerusalem, Israel. Chama cha ukombozi wa Palestina (PLO) kimepinga ziara ya Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya katika Jerusalem ya mashariki na sehemu ya makazi ya Israel katika ukingo wa magharibi wa Mto Jordan.

Kamati ya utendaji ya PLO imesema makubaliano ya kimataifa yanataja ardhi ya Palestina iliyotawaliwa na Israel mwaka 1967 ni ardhi ya nchi ya Palestina na siyo vinginevyo.

Rais Kenyatta yuko katika ziara ya kiserikali nchini Israel. Hii ni ziara yake ya kwanza kwa Rais Kenyatta kufanyika nchini hapa wakati mataifa hayo yakiwa katika mkakati wa kuimairisha uhusiano wa kibiashara.

Awali, akizungumza na raia wa Kenya wanaoishi Israel, Rais Kenyatta aliwashutumu raia wake kuhusu jinamizi la ufisadi.

Alisema ni jambo la kusikitisha kwamba taifa la Kenya linasifika kwa mambo mabaya ikiwa pamoja na ufisadi uliokithiri, ukabila wa hali ya juu na matusi yanayoendelezwa hasa na wanasiasa.

“Sisi kama Wakenya pia, Mungu ametupatia nchi ambayo ni nzuri mara 20 kuliko hii tuko hapa. Lakini tukitembea ni kulia, ni kuiba,” alisema kiongozi huyo na kuongeza kuwa: “Tuna ujuzi pia, wa kuiba, kutukanana na kufanya mambo maovu na ya kuleta ukabila,”.

Rais Kenyatta alisema licha ya Kenya kuwa taifa lenye utajiri mkubwa, kasumba ya ufisadi miongoni mwa viongozi na raia imelemaza ustawi wa taifa hilo.

Kukiri kwa Rais Kenyatta akiwa ziarani Israel kwamba ufisadi umemea mizizi katika taifa lenye uchumi bora zaidi kanda ya Afrika Mashariki, kunajiri huku jinamizi hilo likiendelea kugonga vichwa vya habari na kutawala mijadala kwenye mitandao ya kijamii nchini humo.

Kashfa ya mamilioni ya fedha kuporwa kutoka mfuko wa huduma ya vijana wa taifa (NYS) na vigogo serikalini, ndiyo sakata la ufisadi la hivi karibuni linaloendelea kuandama utawala wa Rais Kenyatta.

Mwaka jana, Rais Kenyatta aliwatimua mawaziri watano na maofisa wengine wakuu serikalini kutokana na madai ya ulaji rushwa.

Pia, hivi karibuni Jaji Mkuu Willy Mutunga alizua mjadala mkali katika mitandao ya kijamii baada ya kunukuliwa na gazeti la Uholanzi akisema kwamba Kenya ni taifa la wanyang’anyi.    

MWANANCHI

No comments: