ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, February 10, 2016

Rais Magufuli kaenda tena Muhimbili, kakutana na haya mengine


By Mwandishi Wetu, Mwananchi __ mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Akina mama waliokuwapo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), jana walizuia msafara wa Rais John Magufuli wakimtaka kwenda katika wodi ya wazazi ili kujionea jinsi wazazi wanavyokabiliwa na kero mbalimbali ikiwamo ya kulala chini kutokana na kukosa vitanda.

Taarifa iliyotolewa jana na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa imeeleza kuwa akina mama hao walimsimamisha Dk Magufuli alipokuwa akitoka katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete alikokwenda kumjulia hali Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir aliyelazwa katika taasisi hiyo.

Baada ya kujionea mwenyewe kero ya msongamano na kuzungumza na baadhi ya wazazi waliojifungua, Rais Magufuli aliwaahidi kuwa atashughulikia kero alizozishuhudia.

“Nimeiona hali halisi mimi mwenyewe, watu wanapata shida, watu wana mateso na ndiyo maana nimeamua kuja kwa makusudi, sikuomba ruhusa ili nijionee hali ilivyo, nimejifunza mengi, ninayabeba na nitajua namna ya kuyatatua,” alisema.

Kabla ya kutembelea wodi ya wazazi, Dk Magufuli alimjulia hali Mufti Zubeir na kumuombea apone haraka.

Pamoja na kupokea pole ya Rais, Mufti aliongoza dua ya kumuombea heri Rais Magufuli ili aweze kutekeleza vyema majukumu yake ya kuwahudumia Watanzania.

Dua kama hiyo ilifanywa pia na wananchi wengine waliokuwa wakimsubiri nje ya majengo ya Muhimbili.

“Mwenyezi Mungu mbariki Rais wetu, mpe hekima, busara na upendo katika kazi zake za kuiongoza nchi hii ili Watanzania wote wanufaike,” ilisema sehemu ya dua hiyo iliyoongozwa na mmoja wa akina mama.

1 comment:

Anonymous said...

Huu mtandao wa ccm blaza,shida kweli kweli.