ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, February 21, 2016

SERIKALI YANUSA UFISADI MOSHI

Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama

Serikali imenusa harufu ya ufisadi katika uwekezaji wa kiwanda cha saruji cha Moshi Cement na kuiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kuchunguza sakata hilo.

Wingu jeusi limezingira sakata hilo baada ya Halmashauri ya Wilaya ya Rombo kuwalipa wananchi fidia ya Sh260 milioni ili kumpisha mwekezaji, wakati haina hisa kwenye kiwanda hicho.
Wakati halmashauri ikilipa fidia, mwekezaji Kampuni ya Jun Yu Investment International ya China anadaiwa kuwalipa baadhi ya viongozi wa Serikali Sh500 milioni ili walipe fidia hiyo.
Pia, imebainika kuwa licha ya kiwanda hicho kumilikiwa na kampuni binafsi kutoka China, bado inatua anuani ya boma.
Mwaka jana, aliyekuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Anjela Kairuki, aliagiza vyombo vya dola kuchunguza suala hilo ili kujua ni kiongozi gani alipokea mgawo huo wa fedha.
Sakata hilo liliwahi kufikishwa bungeni na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee aliyemtuhumu aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama kuwa miongoni mwa wanahisa.
Hata hivyo, baadaye Gama aliitisha kikao na wanahabari na kukanusha kuwa na hisa, lakini akakiri mtoto wake aitwaye Muyanga ni miongoni mwa wanahisa.
Lakini juzi, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Amos Makala aliiagiza Takukuru kuwachukulia hatua za kisheria watu wote waliohusika na ulipaji wa fedha hizo Sh260 milioni kwa ajili ya fidia ya wananchi.
Makala alitoa maagizo hayo wakati alipofanya ziara kwenye kiwanda hicho kilichopo Kijiji cha Holili kuangalia changamoto zinazokikabili.
“Licha ya Halmashauri ya Wilaya ya Rombo kuwa ndiyo iliyolipa fidia kwa wananchi, haina hisa wala siyo mbia wa kiwanda hicho kutokana na wawekezaji kukingiwa kifua,” alisema Makala.
“Kiwanda kinazalisha lakini halmashauri siyo mbia wala hakijawahi kutoa kodi yoyote. Kuna shida kubwa. Takukuru wafanye uchunguzi mara moja na waliohusika wachukuliwe hatua,” alisisitiza Makala.
Makala alisema kama halmashauri ilifidia eneo na kiwanda kikajengwa, inatakiwa kuwa na hatimiliki na siyo mwekezaji kama anavyotaka.
Alitoa mwezi mmoja kwa mwekezaji kuchukua hatua za dharura kudhibiti uchafuzi wa mazingira kwa wafanyakazi na wakazi wa eneo la Holili na kuwapa wafanyakazi mikataba ya ajira. Aliutaka uongozi wa kampuni hiyo kuwa na anwani yao ya posta na kuacha kutumia ya mkuu wa mkoa na kwamba ofisi ya Serikali haitakiwi kuwa sehemu ya kampuni hiyo. Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Lembrisi Kipuyo alisema halmashuri yake ilifidia wananchi waliokuwa na maeneo hayo fedha hizo kwa vikao ambavyo hana uhakika kama vilikuwa halali. Kipuyo alisema ekari 129 zilitengwa kwa ajili ya uwekezaji na eneo hilo lilikuwa likimilikiwa na watu tisa waliolipwa fidia na halmashauri kwa ajili ya uwekezaji uliosimamiwa na ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.
Awali, bila kujua ajenda ya Makala, meneja mauzo wa kiwanda hicho, Sofia Marina alisema kiwanda hicho kilianzishwa 2015 na mmiliki wake alitokea China na kilianzishwa kwa usimamizi wa Serikali ya mkoa.
Marina alisema kiwanda kina uwezo wa kuzalisha tani 7,000 kwa mwezi na kwamba hali hiyo inatokana na ukosefu wa mtaji. Alibainisha kuwa tatizo hilo la uzalishaji mdogo linachangiwa na kukosekana kwa umeme wa uhakika na kwamba unapokatika bila taarifa na kurejea, huua baadhi ya vifaa vya mitambo. Bungeni, Mdee alimtuhumu Gama kuwa na hisa 20,000 katika kampuni ya Jun Yu Investment International inayojenga kiwanda cha Saruji wilayani Rombo, huku mwanaye Muyanga akiwa mwanahisa pia.
Pia, alimtuhumu Gama kutaka kupora ardhi ya Ushirika Lokolova, Wilaya ya Moshi Vijijini ambako kunajengwa soko la kimataifa la mazao na mji wa kisasa wa viwanda na biashara.
Tuhuma hizo ziliungwa mkono na Mbunge wa Vunjo wakati huo, Augustine Mrema ambaye alikwenda mbali na kudai mkoa una dalali wa viwanja na siyo kiongozi.
Wakati huo, Gama alijitetea kuwa hajawahi kuchukua rushwa ya hata senti tano katika mradi wa ujenzi wa kiwanda hicho.
“Hao waliokuja kujenga kiwanda pale ni wawekezaji, lakini ambao ni rafiki na mtoto wangu. Mimi taarifa zao nimezipata kupitia kwa mtoto wangu Muyanga Leonidas Gama.
“Alichowahi kunijulisha ni kwamba kuna marafiki zake wanataka kujenga kiwanda Dar es Salaam au Bagamoyo. Mimi kwa mapenzi yangu nikaomba kiwanda hiki kijengwe Kilimanjaro.
“Baada ya kukubali kujenga kiwanda nilipeleka hii ajenda RCC (kikao cha ushauri cha mkoa) ambacho kilihudhuriwa na wabunge watatu, Philemon Ndesamburo, Joseph Selasini na Mrema”.
Gama alisema aliwaambia kwenye kikao hicho kuwa mwekezaji ameletwa na mtoto wake na RCC ikajadili kiwanda kijengwe wapi.
“Bahati nzuri wajumbe kutoka Rombo akiwepo Selasini walifanikiwa kuwashawishi wajumbe kijengwe Rombo. RCC ilitoa maelekezo kwa Halmashauri ya Rombo washughulikie uwekezaji ule,” alisema.
“Aliyetafuta kiwanja, aliyelipa fidia alikuwa ni Halmashauri ya Rombo. Mimi kama RC sikuhusika tena na sina hata senti tano niliyoipata kwa shughuli hiyo,” alisisitiza RC Gama.

No comments: