Rais Dk. John Magufuli (wakati huo akiwa mgombea wa nafasi hiyo kupitia CCM) alitoa nyingi, akiongozwa na kaulimbiu ya ‘Hapa Kazi Tu’ na kibwagizo cha ‘Tanzania ya Magufuli itakuwa ya Viwanda’. Hatimaye alipata ridhaa ya kuunda na kuongoza serikali ya awamu ya tano.
Wakati leo anatimiza siku 100 tangu Novemba 5, mwaka jana, aliposhika Bbiblia na kuapa kuwa Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, wengi wanajiuliza: “Ameweza au amechemsha kuonyesha mwelekeo wa ‘Tanzania ya Magufuli ya Viwanda”?
Wakosoaji wake wanasema mpaka sasa bado dira yake ya kuongoza nchi haijaonekana, kwa kuwa sehemu ya kwanza ya kuiona ilikuwa kwenye mkutano wa pili wa Bunge la 11, ambapo serikali yake ilitarajiwa kuwasilishwa mpango wa maendeleo wa miaka mitano.
Jambo hilo halikufanikiwa baada ya watunga sheria kukosoa kile serikali ilichotaka kuwasilishwa kwa maelezo kwamba si mpango wa maendeleo, na pia ni kinyume cha kanuni za Bunge na Katiba.
Kwa upande mwingine, hatua zake za kupambana na rushwa ambazo mwenyewe anaita ‘kutumbua majipu’, zinaonyesha kufurahisha kundi lingine linaloona kuwa serikali ilikuwa imejaa wabadhirifu.
Jambo ambalo baadhi ya wakosoaji wake wanasema si sawa kwa kuwa kwa kiasi fulani anakiuka taratibu za utumishi na sheria za kazi katika kuwafukuza na kusimamisha watumishi wa umma.
Mbali na hatua hizo, jambo lingine ambalo limeonekana kufurahisha wengi ni hatua yake ya kubana matumizi ikiwa pamoja kupunguza safari za nje, kufuta maadhimisho ya Siku ya Uhuru Desemba 9 kwa kufanya gwaride na kupunguza matumizi ya fedha zilizokuwa zimepangwa kutumiwa na wabunge katika kujipongeza siku alipofungua Bunge.
Licha ya kuanza kutekeleza ahadi yake ya elimu bure kuanzia darasa la kwanza mpaka kidato cha nne, ile ya kugawa Sh. milioni 50 kwa kila kijiji, mwanga wa utekelezaji wake bado haujaonekana.
Mwelekeo wa bajeti ya serikali kwa mwaka 2016/17 ya Sh. trilioni 22.99 ambayo ni ongezekeko la asilimia 2.2 ya bajeti ya 2015/16 (Sh. trilioni 22.5), ilitarajiwa kuonyesha uwapo wa fedha hizo.
Jambo lingine ambalo bado liko gizani na linaiweka Tanzania njia panda kwenye sura ya dunia ni lile la Zanzibar, ambalo Rais Magufuli aliingia madarakani na kulikuta bado ni bichi. Watu wengi walitarajia angelipatia ufumbuzi wa haraka, kwa imani waliyojipa kuwa yeye si mtu wa siasa nyingi.
Sambamba na hilo, suala la uhusiano wa kimataifa linaleta ukakasi katika utendaji wake ndani ya siku 100. Katika muda huo, Rais Magufuli ameshindwa kusafiri nje ya nchi kwa shughuli za kiserikali, jambo ambalo wachambuzi wa mambo wanasema linatia doa katika ushirikiano wa kimataifa.
Tangu alipoingia madarakani, kumefanyika mikutano kadhaa ya kimataifa na kikanda ambayo Rais Dk. Magufuli ameshindwa kuhudhuria na kuwatuma wasaidizi wake kumwakilisha.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment