Advertisements

Sunday, February 7, 2016

Wafanyakazi TRL wataka ripoti ya mabehewa

By Beatrice Moses, Mwananchi beamoseka@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wafanyakazi wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), wameishauri Serikali kuweka hadharani taarifa za uchunguzi wa kashfa ya ununuzi wa mabehewa 274 yanayodaiwa kuwa mabovu, ili hatua za kisheria zichukuliwe kwa wahusika.

Ushauri huo ulitolewa jana na Kaimu Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli Tanzania (Trawu), Shehe Shughuli mbele ya Katibu Mkuu wa Uchukuzi, Dk Leonard Chamuliho aliyekwenda kumtambulisha Mkurugenzi Mkuu mpya wa TRL, Masanja Kadogosa.

“Tunaona kuna haja ya Serikali kuweka hadharani taarifa za uchunguzi wa mabehewa yanayodaiwa kuwa ni mabovu, kwa sababu wapo wenzetu wengine ambao wamehusishwa ikitoka hiyo tutajua nani mhusika na siyo watu wanaendelea kulipwa mishahara tu wakati sisi tunataabika,” alisema.

Shughuli alisema jambo hilo linawaumiza tofauti na wengine wanavyofikiria, hivyo taarifa ya uchunguzi huo itakuwa ni hatua mojawapo ya kutatua matatizo yanayowakabili likiwamo la mabehewa hayo kuanguka mara kwa mara.

“Tatizo kubwa ni kwamba, mabehewa haya yaliletwa bila hata vitabu vya mwongozo ambavyo pengine vingesaidia kubaini baadhi ya mambo, pia yamekuwa hayaingizwi kwenye karakana badala yake yanatengenezwa kinyemela,” alisema.

Dk Chamuriho alisema suala hilo lipo kwenye uchunguzi na kwamba, asingeweza kutoa taarifa za kina hadharani kwa kuwa ni jukumu za wale wanaochunguza.

Suala la mabehewa hayo hivi karibuni liliibukia kwenye mkutano wa Bunge uliomalizika juzi mjini Dodoma na kusababisha Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Jesca Kishoa kusimamishwa vikao viwili kwa kudai aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi katika Serikali ya Awamu ya Nne, Dk Harrison Mwakyembe anahusika.

No comments: