ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, February 11, 2016

Wasira: Sina hakika kama Magufuli anabana matumizi

Aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika
By Goodluck Eliona, Mwananchi

Dar es Salaam. Mwanasiasa mkongwe aliyekuwa waziri kwenye Serikali za Awamu Nne za Kwanza, Stephen Wasira amesema hana uhakika kama muundo wa Serikali ya Rais John Magufuli unapunguza matumizi ya fedha za umma.

Wasira anakuwa waziri wa tatu wa Serikali ya Awamu ya Nne kuzungumzia sera za kubana matumizi za Rais Magufuli, baada ya Bernard Membe na Dk Makongoro Mahanga kusema kuunganisha wizara na kubakia na idadi kubwa ya makatibu wakuu si kubana matumizi.

Baraza ambalo Rais Magufuli alilitangaza lina mawaziri 34, ikiwa ni pungufu ya mawaziri 20 ikilinganishwa na baraza la mwisho la Rais Jakaya Kikwete, huku kukiwa na wizara 18, baadhi zikiwa zimebakia na makatibu wake wakuu licha ya kuunganishwa.

Akizungumza kwenye mahojiano maalumu na Mwananchi, Wasira alisema licha ya Rais Magufuli kupunguza idadi ya mawaziri ikilinganishwa na mtangulizi wake, jambo hilo halimaanishi kwamba Serikali itatumia fedha kidogo.

Wasira, ambaye alikuwa miongoni mwa wana-CCM waliojitokeza kutaka kuteuliwa na chama hicho kuwania urais, alisema mtazamo kuhusu baraza la mawaziri unategemea malengo ya kiongozi husika.

“Lakini unaunda Serikali ya nini? Serikali kama zilivyo taasisi nyingine zozote, ina muundo ambao lazima uwe na shabaha, lazima iwe ajenda ambayo unataka Serikali hiyo iitekeleze,” alisema Wasira ambaye alikuwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika.

Alisema siku zote shabaha ya muundo wa taasisi yoyote ni kuongeza ufanisi na kupunguza matumizi makubwa ya fedha, hivyo ni vyema wananchi wakajiuliza iwapo muundo wa Serikali ya Magufuli unakuwa na ufanisi au la.

“Sasa kama ungeniuliza muundo huo una ufanisi au la, hapo tunaupa muda. Kwa sababu kama nitasema hauna ufanisi nitakuwa nasema bila kufanya utafiti. Muundo wenyewe umeundwa juzi halafu upo pale kutekeleza ajenda ya Rais na ajenda ya CCM. Mimi siwezi kusema ni fanisi au si fanisi,” alisema.

Akosoa baadhi ya wizara

Hata hivyo, mwanasiasa huyo alikosoa muundo katika baadhi ya wizara akisema zimewekwa kwa namna ambayo inaonekana ni wizara moja lakini zipo mbili ndani yake na hivyo akilitazama baraza hilo anawaona mawaziri 19 na wizara 19.

“Kwa mfano ipo wizara moja inaitwa Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa, Utumishi na Utawala Bora, lakini ina mawaziri wawili. Waziri mmoja anasimamia utumishi na utawala bora na mwingine anasimamia tawala za mikoa na Serikali za Mitaa, sasa hiyo ni wizara moja?” alihoji Wasira ambaye alikuwa Waziri wa Tamisemi kati ya mwaka 2008 na 2010.

“Kila wizara ina katibu mkuu wake, kwa hiyo ni wizara mbili zimepewa jina moja? Kwa hiyo mimi nikijumlisha naona wizara 19 na mawaziri 19,” alisema.

Mwanasiasa huyo, ambaye alikuwa waziri katika kipindi chote cha miaka 10 ya uongozi wa Rais Kikwete, alisema mtu anayetaka kujua iwapo muundo wa baraza la Rais Magufuli umebana matumizi ya fedha za umma anapaswa kufanya kwanza mahesabu.

“Hapa sina calculator (kikokotozi), lakini naweza kutoa maoni kwenye wizara mbili, moja ya Kilimo ninayoijua zaidi, ambayo imeunganishwa na mifugo na uvuvi na ina makatibu wakuu watatu,” alisema na kuongeza: “Mifugo ina katibu wake mkuu, kilimo ina katibu mkuu na uvuvi ina katibu mkuu. Sasa unahitaji calculator kujua kama gharama zimepungua, kwa sababu huko nyuma kulikuwa na mawaziri wawili na makatibu wakuu wawili.”

Kada huyo mkongwe alisema uamuzi wa kumteua waziri mmoja katika wizara hiyo na kuongeza idadi ya makatibu wakuu, unatia shaka kuhusu kuongezeka au kupungua kwa gharama za kuendesha wizara.

“Kama ni kweli kuna gharama imeokolewa, basi kuwa na mawaziri ni gharama sana ikilinganishwa na makatibu wakuu,” alisema kada huyo ambaye katika shahada yake ya kwanza na ya uzamili alibobea kwenye uchumi na uongozi.

Huku akicheka, Wasira alisema kwa kawaida waziri hupewa dereva mmoja na msaidizi wake, lakini katibu mkuu huwa na dereva mmoja na wasaidizi zaidi ya moja kutokana na majukumu mengi aliyonayo.

Ushauri kwa Magufuli

Wasira, ambaye aliongoza kamati iliyoandaa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015, alimshauri Rais Magufuli kuitoa Idara ya Umwagiliaji kutoka Wizara ya Maji na kuirudisha Wizara ya Kilimo ilikokuwa awali kwa kuwa ni sehemu ya kilimo.

“Kutoa umwagiliaji kutoka Wizara ya Kilimo kunamfanya Waziri wa Kilimo kuwa waziri wa kilimo cha mvua, msimamizi mzuri wa umwagiliaji lazima atakuwa Waziri wa Kilimo,” alisema.

Safari za nje

Akizungumzia uamuzi wa Rais Magufuli kuzuia safari za nje hadi kwa kibali maalumu kutoka Ikulu, alisema ni nzuri kwa sababu baadhi ya watumishi wa umma walikuwa wakisafiri nje ya nchi pamoja na watu wengi wasiohitajika.

Hata hivyo, alisema si kweli kwamba Rais Magufuli amezuia kabisa safari hizo kama inavyoelezwa na baadhi ya watu, badala yake alihoji kama ni kweli mbona Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisafiri kwenda Botswana hivi karibuni?

“Makamu wa Rais alikuwa Afrika Kusini juzi kwani huko ni ndani? Wanakwenda lakini kwa masuala yaliyo na umuhimu kwa Taifa,” alisema.

Alisema utaratibu huo si mgeni serikalini kwa kuwa tangu Serikali zilizopita mawaziri walikuwa wakitakiwa kuomba kibali cha safari kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu.

“Labda zamani vibali vilikuwa vinatolewa kwa urahisi zaidi. Hakuna waziri aliyetoka nje bila kupata kibali tena kibali chenyewe cha maandishi. Mimi nadhani kwa hili watakaolalamika ni mashirika ya ndege zaidi maana wao wanafanya biashara,” alisema.

Mchango wake katika sekta ya kilimo

Wasira alisema anaamini haiwezekani kupambana na umaskini nchini bila kuwekeza katika sekta ya kilimo. Serikali ilifanikiwa kuongeza ruzuku ya wakulima ya mbolea na mbegu kutoka Sh7 bilioni hadi Sh300 bilioni kwa mwaka.

Hata hivyo, alisema idadi ya wakulima na kiasi cha fedha kilichotolewa kwa mwaka havilingani, kwa kuwa wakulima walionufaika hawakuzidi milioni. Takwimu za Serikali zinaonyesha kuwa hadi sasa Watanzania maskini ni asilimia 28.

“Kitu ambacho najivunia, tulishauri na ikawezekana ni kuanzishwa kwa Benki ya Kilimo kwa kweli ni wazo ambalo tunadhani linaweza kusaidia kama likisimamiwa vizuri. Sikuianzisha mimi lakini sisi tulishauri kama Wizara ya Kilimo na Rais (Jakaya Kikwete) akakubali,” alisema.

Kuhusu migogoro ya wafugaji na wakulima inayotokea katika maeneo mbalimbali nchini, Wasira alisema kitu cha muhimu ni kujua kuwa wananchi hao wanagombania ardhi kutokana na ongezeko kubwa la mifugo.

Alisema kwa kulitambua tatizo hilo, CCM iliweka kwenye Ilani yake utaratibu wa kulishughulikia ikiwa ni pamoja na kuwachimbia wafugaji mabwawa katika maeneo yao na kule walikokimbilia.

“Lazima tuwape maji na kuwatengea eneo la malisho kwa kupima ardhi na kuikabidhi kwa wanaoitumia na kuwaambia ukweli kwamba ardhi hiyo waliyopewa haitatosha,” alisema.

Wasira, ambaye pia amewahi kuwa mbunge wa Bunda, alisema kinachotakiwa kufanyika ni kwa Serikali iliyopo madarakani kuisoma Ilani ya CCM kwa kuwa inaeleza namna ya kutatua changamoto mbalimbali.

“Ilani imeshauri kila kitu, hiki kitabu hiki (anaiinua juu) kina kila neno, huwezi kuwa na kila kitu kimeandikwa halafu akili yako ikaacha kufanya kazi,” alisema.

Alisema mapambano ya dhidi ya rushwa yanayofanywa na Rais Magufuli ni utekelezaji wa Ilani ya CCM na si ya Chadema kama ambavyo baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakidai.

Mgogoro wa Zanzibar

Kuhusu mgogoro wa kisiasa Zanzibar uliotokana na kufutwa kwa matokeo ya urais, uwakilishi na udiwani, Wasira alisema haukutokana na chama chochote cha siasa, bali Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ambayo ilidai imebaini kasoro.

Alisema kilichotokea Zanzibar ni sawa na timu mbili zinapocheza uwanjani halafu refa anakataa goli na mchezo unapomalizika, anasema hakuna aliyeshinda.

“Sasa mnafanyaje, mnagawana magoli yasiyokuwapo? Si mnasambaa halafu mnangoja refa awaambie mchezo wa marudio utafanyika lini? Sasa hapo ndipo tatizo la Zanzibar linapoanzia,” alisema.

Alisema ZEC iliyosimamia uchaguzi huo ilikiri kushindwa kusimamia kisha ikasema haukuwa huru na haki kwa kuwa baadhi ya vituo wananchi walipiga kura bila kuwapo kwa mawakala vya vyama.

“Hicho chama ambacho wakala wake hakufika na tume ndiyo imechelewa kutoa kibali, hicho chama kitasema haki ilitendeka wapi? Wanasema kule Pemba waliojiandikisha walikuwa 85,000 lakini waliopiga kura walikuwa 115,000, sasa unasema nini juu ya jambo hilo?” alihoji.

Pia, alisema Rais Magufuli ni ndiye mwangalizi mkuu wa usalama na amani ya nchi, hivyo ni lazima ahakikishe Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inakuwa na amani.

Kiongozi huyo alisema katika mchezo wa mpira wa miguu timu moja inapogoma kuingia uwanjani, ushindi hutolewa kwa timu pinzani na kwamba hilo ndilo linaloweza kutokea Zanzibar iwapo CUF itasusia uchaguzi.

“Mimi sipendi hali ifike huko. Ninaamini kwamba suluhu ya tatizo hilo itakuwa ya kudumu zaidi wakishirikishwa Wazanzibari wote,” alisema.

4 comments:

Anonymous said...

Were yalikushinda malizana Na Bulaya kwanza
Hapa kazi tu

Anonymous said...

This shud be the last guy to criticise anyone, let alone Magufuli.

Akae kimya mascandal yake alipokuwa Wizarani kwetu tusiyamwage.

Anonymous said...

Wakati mwingine kunyamaza ni busara kubwa.Kama huyu babu angekuwa ni bingwa wa craft muundo wa serikali yenye ufanisi,je performance tuliyoiona kwenye awamu ya JK ndio utaalamu wake alipoishia?
Ni vema wananchi wa Bunda walivyoamua kumstaafisha kwa nguvu otherwise angeendelea kutusumbua..

Anonymous said...

Lakini tuacheni ushabiki. Tuulize je ni kwanini watu hawa wanakuja na hoja hizo? Je ni kweli matumizi yanabanwa au si kweli?