ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, February 11, 2016

Watanzania wanne wauawa Msumbiji

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Henry
By Mary Sanyiwa, Mwananchi __ mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Mtwara. Wafanyabiashara wanne wa Tanzania wameuwa kwa kupigwa risasi kisha kuchomwa kwa vitu vyenye ncha kali nchini Msumbiji baada ya kuvamiwa na watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Henry Mwaibambe alisema tukio hilo lilitokea usiku wa Jumatatu iliyopita katika machimbo ya dhahabu, Kijiji cha Mtoro Mtupweshi Kamprigando.

Aliwataja waliofariki dunia kuwa ni Salum Mfanga (44) Mkazi wa Temeke, Dar es Salaam, Yusuph Twalibu (34) na Mariam Ramadhani (30) wakazi wa Tanga na Hamisi Mkapira (40) wa Morogoro.

Kamanda huyo alisema kifo cha Mariam ambaye alifanikiwa kujiokoa, kilisababishwa na kukosa huduma ya haraka baada ya kuvujika mguu.

Kamanda huyo alisema wafanyabiashara hao walivamiwa na majambazi waliokuwa na risasi pamoja na mapanga katika vibanda vya kubadilishia fedha nchini humo. “Miili ya wafanyabiashara hao ililetwa na ndugu zao ambao wanaishi Msumbiji,” alisema.

Wakizungumzia tukio hilo, Said Mfanga na Dotto Ramadhani ambao ni ndugu wa marehemu hao walisema baada ya kuwaua, majambazi hao waliwapora fedha pamoja na mabegi yao.

“Kaka Salumu alinunua dhahabu gramu 160 na rafiki yake alinunua gramu 150 baada ya kununua wakalala huko kwa sababu hakuna hoteli. Unalala kwenye matanda (mahema) nasi tukaenda kulala sehemu zetu baada ya saa 7.10 tukasikia risasi tisa zinapigwa,” alisema Mfanga.

No comments: