Kampuni ya udalali ya Yono, imesema makampuni na wafanyabiashara wanaodaiwa kodi na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) baada ya kutorosha makontena kwenye Bandari Kavu ya Azam mwaka jana, wamekabidhi mali zinazokadiriwa kufikia Sh. Bn 6.
Mali hizo zitauzwa ili kulipa kwa TRA fidia ya kodi ya jumla ya Sh. bilioni 18 ambazo zilikwepwa kulipwa na wafanyabiashara na kampuni hizo.
Akizungumza na Nipashe jana, Mwenyekiti wa kampuni ya udalali ya Yonno iliyopewa kazi ya kuzifilisi kampuni zilizokwepa kodi, Stanley Kevela, alisema wafanyabiashara wengi wameonyesha ushirikiano wa kulipa deni hilo la serikali.
“Tulitaka kuanza kufunga maduka na mali za wahusika lakini katika hali ambayo hatukuitarajia wengi wanatoa ushirikiano mzuri na Kampuni ya Yono na wengine wameendelea kutuambia kuwa watalipa madeni yao ndani ya muda mfupi," alisema Kevela.
"Lengo letu siyo kuwatisha wafanyabiashara bali kuwezesha deni la serikali lilipwe.”
Mwenyekiti huyo wa Yono alisema hadi sasa wafanyabiashara mbalimbali wameshasalimisha kwa TRA zaidi ya Sh. milioni 300, baada ya kupewa hesabu za madeni wanayodaiwa.
Kevela alisema wameanza kamatakamata ya mali za wafanyabiashara wanaodaiwa na mamlaka hiyo lakini wale wanaoonyesha ushirikiano mzuri hawafungi wala kuchukua mali zao kwani huelewana namna bora ya kulipa.
“Kote tunakoenda kwa ajili ya kukamata mali imetushangaza kuona hakuna anayekataa kulipa hilo deni, wote wamesema watalilipa na wengine wanataka kupewa muda kidogo ili wajipange jambo ambalo ni zuri,” alisema Kevela.
"Sisi tutashirikiana nao kuhakikisha fedha za serikali zinapatikana."
Alisema mali zinazofikia Sh. bilioni sita ambazo wafanyabiashara wameikabidhi Yono zitauzwa kwa mnada ili zipatikane fedha za kwenda kulipa madeni ya wafanyabiashara hao kwa TRA.
“Sisi hatutaki kufanya kazi hii kwa kukurupuka na kwa jazba, tunakwenda kisomi na kwa mbinu za kisasa maana tunataka kuwaelimisha zaidi wafanyabiashara badala ya kutumia nguvu na kwa kweli mbinu hii inatusaidia kupata ushirikiano mkubwa.
"Kuna mfanyabiashara anadaiwa Sh. bilioni saba... tulitaka kukamata mali zake lakini kaonyesha ushirikiano kwamba atalipa hivi karibuni.”
Yono ilishinda zabuni ya kuwa dalali wa TRA na wiki mbili zilizopita iliwapa siku 14 wafanyabiashara hao wawe wamelipa fedha wanazodaiwa na Mamlaka hiyo vinginevyo watafilisiwa.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment