ANGALIA LIVE NEWS

Monday, February 22, 2016

WAZIRI MUHONGO AITAKA TANESCO NA TPDC KUFANYA KAZI KISASA

Kaimu Mkurugenzi wa Kampuni ya Pan African Energy Andy Hanna ( wa pili kutoka kulia) akielezea majukumu ya kampuni hiyo mbele ya Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo pamoja na watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini pamoja na Taasisi zilizopo chini yake.
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo akielezea fursa za uwekezaji katika sekta ya gesi nchini.
Kaimu Mkurugenzi wa Kampuni ya Pan African Energy Andy Hanna akisisitiza jambo katika kikao hicho.
Kaimu Mkurugenzi wa Kampuni ya Pan African Energy Andy Hanna (kushoto) na Mwenyekiti wa Kampuni ya Pan African Energy Nchini Patrick Rutabanzibwa (kulia) wakinukuu maelekezo kutoka kwa Wiziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (hayupo pichani).

Na Greyson Mwase, Dar es Salaam

Waziri wa  Nishati na  Madini Profesa Sospeter Muhongo amelitaka  Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Shirika la  Maendeleo  ya Petroli Nchini (TPDC) kufanya kazi katika  mtindo wa kisasa ili nishati ya umeme iweze kuwa  ya  uhakika kwa maendeleo  ya uchumi wa nchi.

Profesa Muhongo aliyasema hayo katika kikao chake na Kampuni ya Pan African Energy kilichofanyika jijini Dar es Salaam  kilichoshirikisha pia watendaji kutoka wizara ya nishati na madini, TANESCO, TPDC na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).

Alisema  mahitaji ya gesi kwa ajili ya kuzalisha umeme wa uhakika ni makubwa, hivyo hakuna sababu  ya  kuwepo  kwa upungufu wa nishati ya umeme  nchini wakati kuna gesi ya uhakika.

Alifafanua kuwa haiwezekani shirika la TPDC likadai kuwa kuna gesi ya kutosha kwa ajili ya kuzalisha umeme, wakati kuna upungufu wa umeme nchini.

Alisema  serikali ina mpango wa kuhakikisha kuwa  wananchi wote hasa waishio vijijini  wanaunganishwa na umeme wa uhakika kupitia Wakala wa Nishati Nchini (REA) hivyo ni jukumu la mashirika hayo kuhakikisha yanabuni miradi na kukaribisha wawekezaji mbalimbali  katika uzalishaji wa umeme  wa uhakika ili wananchi wote waweze kuunganishwa na huduma ya umeme.

Alisisitiza kuwa amekwishawaalika wawekezaji mbalimbali kwa ajili ya kuwekeza kwenye uzalishaji  wa  Megawati 1000 za umeme  kwa ajili ya kuingizwa kwenye  gridi ya  taifa, hivyo ni vyema shirika la TPDC likahakikisha   gesi ya uhakika inapatikana ili  umeme uweze kuzalishwa mara moja.
“  Lengo la  serikali kupitia  Wizara ya Nishati na Madini ni kuhakikisha kuwa ifikapo  mwaka 2025 Megawati 10,000 zinazalishwa, hivyo sekta ya nishati  kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi na kutoka kwenye  kundi la nchi masikini duniani  na kuingia kwenye kundi la nchi za  kipato cha kati, kama   Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025, inavyofafanua,”alisema Profesa Muhongo.

Wakati huo huo, Profesa Muhongo aliitaka kampuni ya Pan Afrian Energy  kuhakikisha inatatua changamoto zote  inazozikabili  kwa kipindi cha miezi mitatu kabla ya kukutana naye  Juni 01 mwaka huu kwa ajili ya kupokea mapendekezo ya kampuni hiyo katika kuzalisha  gesi ya uhakika.

Alisisitiza kuwa kutakuwepo na utaratibu wa kukutana na kampuni hiyo kila baada ya miezi mitatu kwa ajili ya kujadili utendaji kazi wa kampuni hiyo, na serikali ipo tayari kutoa msaada pale kampuni itakapokwama.

Aidha, Profesa Muhongo aliitaka kampuni hiyo kuweka utaratibu wa kuajiri  vijana wa kitanzania wanaomaliza masomo ndani na nje  ya nchi baada ya kupata ufadhili kutoka serikalini.

“ Kwa sasa tuna  vijana wengi waliohitimu mafunzo  kwa ngazi  ya shahada za uzamili katika masuala ya mafuta na gesi katika  vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi kama Norway, Uingereza na China, hivyo ni vyema  wakapata ajira katika kampuni ya  Pan African Energy, ili nao waweze kufaidika na elimu na uwepo wa uwekezaji katika shughuli za utafutaji na uchimbaji wa gesi na mafuta nchini,” alisisitiza Profesa Muhongo.

Naye  Kaimu Mkurugenzi wa Kampuni ya Pan African Energy Andy Hanna, akielezea mafanikio ya uwekezaji kupitia  kampuni yake, alieleza kuwa kampuni hiyo imefanikiwa kutoa  ajira 87 kwa watanzania na kuboresha huduma  za jamii kama vile kutoa huduma ya umeme  bure katika eneo la Kilwa kilipo kituo chake za kuzalisha gesi.

Aliendelea kusema kuwa kampuni ya Pan African Energy imejenga  zahanati pamoja na kutoa mafunzo kwa waajiriwa wake lengo likiwa ni  kuhakikisha kuwa kampuni hiyo inakuwa na wataalam wazawa.

No comments: