Waziri wa nchi ofisi ya rais, tawala za mikoa na serikali za mitaa, Tamisemi, George Simbachawene ameagiza mamlaka mbalimbali kuwafukuzwa kazi ndani ya siku 14 watendaji na wenyeviti wa vijiji watakaobainika kuhusika na uchochezi wa migogoro ya ardhi wilayani Mvomero, sambamba na kuhamishwa kwa watumishi waliokaa muda mrefu katika wilaya hiyo.
Waziri Simbachawene amesema hayo wakati akizungumza na viongozi na watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Mvomero na mkoa wa Morogoro, ambapo amepokea taarifa inayohusiana na changamoto za wilaya hiyo ikiwemo juu ya migogoro ya ardhi, huku lawama zikielekezwa na viongozi kwa baadhi ya watendaji na viongozi wa serikali katika kuhusika na kukuza na kuendeleza migogoro hiyo pamoja na ukosefu wa baraza la ardhi katika wilaya hiyo.
Mkuu wa mkoa wa Morogoro Dr Rajab Rutengwe katika kikao hicho, ameiomba mamlaka ya kuzuia na kupambana na rushwa Takukuru kuwaongeza wataalamu ili kukabiliana na maswala ya rushwa ambayo yameonekana kushika kasi katika baadhi ya wilaya na kusababisha migogoro ya ardhi kuzidi kukua, ambapo waziri Simbachawene akaagiza kuchunguzwa na kufukuzwa kwa watendaji wote watakaobainika kuchangia kukua kwa migogoro hiyo ya ardhi na kwamba serikali haitamvumilia yeyote atakayebainika kuwa chanzo cha migogoro hiyo.
Katika siku ya pili ziara yake mkoani Morogoro, waziri huyo wa Tamisemi ameweza kuembelea hospitali ya rufaa ya mkoa wa Morogoro na kueleza kuridhishwa na utendaji kazi na jitihada zinazofanywa na watumishi, wakiongozwa na mganga mfawidhi wa hospitali hiyo Dk Ritta Lyamuya, pamoja na kukagua mradi wa ujenzi wa kisasa wa kituo kikuu cha mabasi Msamvu, pamoja na kuzungumza na viongozi wa mkoa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri za wilaya. Source:ITV
No comments:
Post a Comment