CHAMA cha ACT Wazalendo kimepokea kwa masikitiko
uamuzi uliofanywa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job
Ndugai, kwa kuhamisha kamati, Wenyeviti, Makamu Wenyeviti na Wajumbe wa baadhi
ya Kamati za Kudumu za Bunge uliofanywa jana.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge
na Serikali za Mitaa ACT Wazalendo, Yeremia Maganja, amesema uamuzi huu wa
spika unafuatia kashfa nzito ya viongozi na wajumbe wa kamati mbalimbali za
Bunge kupokea rushwa kutoka mashirika tofauti ya umma kama ilivyoripotiwa na
baadhi ya vyombo vya habari
Amesema
bunge ni mhimili wenye jukumu la kuisimamia serikali , hivyo baadhi ya wabunge
akiwemo Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT Wazalendo) walimwandikia barua
za kujiuzulu Spika wa Bunge, Job Ndugai ili kupisha uchunguzi ufanyike na
wataobainika kupokea rushwa kuchukuliwa hatua za kisheria.
Maganja
amesema ACT Wazalendo imempongeza Mbunge wao na Wabunge wengine waliochukua
hatua ya kujiuzulu ujumbe kwenye kamati zao ili kupisha uchunguzi.
Aidha
amesema kuwa uamuzi huo wa mbunge wao unakwenda sambamba na misingi ya Chama
cha ACT Wazalendo ya uadilifu na uwajibikaji.
Amesema
mabunge yaliyopita, kamati za Bunge zimekuwa zikituhumiwa mara kadhaa kujihusha
na vitendo vya kupokea rushwa kutoka kwa Mashirika ya Umma, Makampuni na watu
binafsi.
Maganja
amesema rai zimekuwa zikitolewa mara kwa mara huko nyuma ya kuitishwa kwa
uchunguzi ili kulinda hadhi na heshima ya Bunge ilipuuzwa na matokeo yake,
kashfa hizi zimeliondolea heshima Bunge na Wabunge.
Amesema kwa
mujibu wa Ibara ya 63(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bunge
ndiyo chombo kikuu chenye madaraka kwa niaba ya wananchi kuisimamia na
kuishauri serikali na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu
yake.
Kinapotuhumiwa
kupokea rushwa, kinawezaje chenyewe kuisimamia serikali na kuongoza mapambano
dhidi ya rushwa?
Maganja
amesema uamuzi wa kuwahamisha Kamati viongozi na wajumbe wa Kamati
zilizotuhumiwa kupokea rushwa ni sawa na kuufunika uozo na kuendeleza utamaduni
mbovu wa siku nyingi hapa nchini wa kuwahamisha au “kuwapangia kazi nyingine”
viongozi na watumishi wa umma wanaotuhumiwa kupokea rushwa au kukosa
ufanisi.
Kimsingi
Utamaduni huu unafifisha mapambano dhidi ya rushwa na uwajibikaji.
Mwenyekiti
huyo amemtaka Spika kuonyesha kwa vitendo jinsi ofisi yake inavyochukizwa na
vitendo vya rushwa nchini kwa kuitisha uchunguzi utaovishirikisha vyombo vya
dola ili ukweli ujulikane.
No comments:
Post a Comment