Balozi Ami Mpungwe akizungumza na waandishi wa gazeti jijini, Dar es Salaam. Picha na Anthony Siame
Wakati bei ya sukari ikiendelea kuipambanisha Serikali na wafanyabiashara, Mwanadiplomasia mkongwe nchini, Balozi Ami Mpungwe amesema siasa za bidhaa hiyo ni hatari kuliko dawa za kulevya iwapo zitakosekana njia madhubuti za kudhibiti biashara haramu iliyopo.
Mpungwe ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Kiwanda cha Sukari cha Kilombero, alisema Serikali inabidi ikaze kamba na kuvunja kundi la wafanyabiashara haramu wanaoingiza sukari nyingi kutoka nje.
Alisema sukari hiyo yenye ubora hafifu huingizwa kwa magendo na kwa kukwepa kodi, hivyo athari zake ni kubwa kwa afya za Watanzania na uchumi wa Taifa.
Katika mahojiano maalumu na gazeti hili yaliyofanyika hivi karibuni, Mpungwe mwenye uzoefu wa muda mrefu katika sekta ya sukari, alisema dawa za kulevya huingizwa na wafanyabiashara wabaya na kuharibu jamii ya watu wachache wasiojielewa, lakini sukari isiyo na ubora ikiingizwa hutumiwa na kila Mtanzania.
“Sukari mahali popote duniani huwa na mvurugano. Siasa ya sukari ni hatari kuliko hata dawa za kulevya kwa sababu inatumiwa na watu wa rika zote, kuanzia watoto hadi wakubwa.
“Watanzania wote takribani 50 milioni wanatumia sukari na kama athari zinatokea basi ni kwa wote, hivyo Serikali isiyumbe kupambana na wafanyabiashara hao wabaya wanaoua viwanda vya ndani na kukwepa kodi,” alisema Balozi Mpungwe.
Kwa muda mrefu sasa, takriban Serikali za awamu zote, wazalishaji wa sukari nchini wamekuwa wakilalamikia uingizwaji wa sukari ya bei rahisi kutoka nje inayohofiwa kuwa na ubora hafifu au iliyokaribia kuisha muda wake wa matumizi na kuhatarisha mustakabali wa viwanda vya sukari vya ndani.
Wafanyabiashara wasio waaminifu wamekuwa wakitumia vibali walivyopatiwa na Serikali kuingiza sukari ya viwandani na kuigeuza kwa matumizi ya binadamu, jambo linalowapatia faida kubwa huku wakiwaumiza wananchi na wazalishaji wa ndani wanaouza bidhaa hiyo kwa bei inayoakisi gharama zao za uzalishaji.
Balozi Mpungwe alisema Serikali ilishindwa kuvilinda viwanda vya ndani na kuwadhibiti wafanyabiashara hao wenye nguvu zaidi ya wazalishaji na wanaonekana kuungwa mkono na mfumo wa utawala. “Tusingetakiwa kuendelea kuzungumza sasa eti ‘sukari, sukari, sukari’ kila siku kwa kuwa ilibidi tujitosheleze kimahitaji miaka mingi iliyopita,” alisema huku akionyesha kukerwa na tatizo hilo.
Balozi Mpungwe aliendelea kusema: “Hapa tuna tatizo kwa sababu kwa miaka 14 niliyokuwapo kwenye biashara hii, suala la sukari halijawahi kukoma tangu (Rais mstaafu Benjamin) Mkapa, Jakaya Kikwete na sasa angalau Rais (John) Magufuli ameanza vizuri ndani ya miezi miwili.”
Mtindo wa uingizaji sukari kiholela nchini umeanza kukomeshwa katika utawala wa awamu ya tano, baada ya Rais Magufuli kupiga marufuku na kuagiza vibali vyote vya kuingiza bidhaa hiyo inapoadimika vitolewe na ofisi ya Waziri Mkuu pekee.
Hatua hiyo imesababisha ahueni kwa wananchi na taharuki kwa baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu, ambao wameamua kutengeneza upungufu bandia wa sukari na kusababisha bei kupanda hadi kufikia Sh2,400 kwa kilo jijini Dar es Salaam na Sh2,800 mikoani.
Kukabiliana na kasi hiyo ya upandaji bei, Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Sukari Tanzania (SBT), Henry Semwanza ndani ya siku mbili tofauti alitoa bei elekezi ya sukari akianza na Sh2,000 jijini Dar es Salaam na Sh2,200 kwa mikoani.
Baadaye Machi 8, Semwaza akatangaza tena bei mpya elekezi ya Sh1, 800 kwa kilo nchi nzima jambo ambalo baadhi ya wafanyabiashara wa jumla na rejareja wameonekana kulipinga wakidai watapata hasara.
Bei hiyo elekezi huenda ikawa pigo kwa wafanyabiashara wadogo kwa kuwa Balozi Mpungwe alieleza kuwa wastani wa bei ya jumla kutoka kiwandani katika viwanda vyote nchini ni kati ya Sh1, 700 na Sh1, 800 ambayo ni karibu sawa na bei elekezi.
Hadi sasa matumizi ya mwaka ya sukari nchini yanakadiriwa kuwa tani 420,000, lakini Balozi Mpungwe alisema takwimu hizo bado si sahihi na huenda mahitaji yakawa makubwa zaidi.
“Uzalishaji wa sukari husimama kwa miezi miwili tu wakati wa masika na kipindi hicho kifupi kinaweza kutengeneza upungufu wa tani 100, 000 pekee, hivyo tatizo siyo kubwa sana. Tulishamueleza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuwa sisi tupo tayari kuwekeza zaidi kutimiza mahitaji, ilimradi tu uwapo uhakika wa kulinda viwanda vyetu,” alisema Mpungwe.
Katika kutafuta suluhu ya mwanya wa mahitaji, Serikali ilikutana na wazalishaji kujadili utaratibu wa uingizaji wa sukari nchini na kuwapa majukumu ya kuleta bidhaa hiyo tofauti na wafanyabiashara waliokuwa wakiingiza kiholela.
Hata hivyo, Balozi Mpungwe alisema hadi sasa bado hawajaelezwa utaratibu kamili wa mchakato wa uingizaji na kuiomba Serikali iuwahishe ili kuzuia upungufu unaoweza kujitokeza na kuwapa mwanya wafanyabishara wasio waaminifu kupata sababu ya kukosoa kuwa wazalishaji hawawezi kazi hiyo.
Wakati Serikali ikitafuta suluhu ya sakata la sukari nchini, baadhi ya wakosoaji wanaona huenda hatua hiyo ikatumika kama njia ya kutengeneza ukiritimba kwa wazalishaji wachache kwenye soko jambo ambalo haliendani na kanuni za soko huria.
Balozi huyo wa zamani wa Tanzania nchini Afrika Kusini, alisema kiwanda chake kilikuwa na mtambo wa kuzalisha sukari ya matumizi ya viwandani, lakini baada ya sukari ya bei rahisi kuanza kuingizwa kiholela nchini walilazimika kubadilisha matumizi na kuanza kutengeneza pombe wanayoiuza kwa kampuni za bia.
No comments:
Post a Comment