Katibu Mkuu mpya wa Chadema, Dk Vincent Mashinji (aliyesimama).
Katibu Mkuu mpya wa Chadema, Dk Vincent Mashinji ametamba kuwa licha ya umri mdogo alionao na kipindi kifupi cha uanachama ndani ya chama hicho, ana uwezo, nia, dhamira na lengo la kukiandaa kushika dola mwaka 2020.
“Nilikuwa mwanachama wa Chadema asiye na kadi ya uanachama kwa kipindi kirefu, baadaye bila malipo, kushawishiwa wala kutumwa, mimi na wasomi wenzangu tuliandaa na kutekeleza mikakati ya kukijenga chama nje ya mfumo rasmi wa chama,” ni kauli ya Dk Mashinji wakati akizungumza na wajumbe wa Baraza Kuu la Chadema juzi usiku.
Daktari huyo wa binadamu aliyetambulishwa jana kwenye mkutano wa hadhara jijini Mwanza, alisema baada ya kukutana na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, yeye na wenzake walikutanishwa na aliyekuwa Katibu Mkuu, Dk Wilbrod Slaa.
“Baada ya kutusikiliza na kuelewa mikakati yetu, Dk Slaa alituhoji iwapo sisi ni wanachama hai wenye kadi za Chadema. Swali lililotushtua kwa sababu miongoni mwetu hakuna aliyekuwa na kadi,” alisema na kuendelea.
“Tulimjibu Dk Slaa kuwa uanachama wetu uko mioyoni; hoja aliyoikubali, lakini akatuelekeza kujiunga na kuchukua kadi rasmi kwa sababu yapo majukumu ambayo hatuwezi kuyatekeleza bila kuwa wanachama hai,” alisema na kuongeza:
“Nilichukua rasmi kadi ya Chadema Machi Mosi, 2013 kutekeleza ushauri wa Dk Slaa,” alisema Dk Mashinji, mwenye umri wa miaka 43.
Ilani ya chama
Aliongeza: “Kwa sababu nilishiriki kuandaa ilani ya uchaguzi na sasa nimekabidhiwa jukumu la kuwa Katibu Mkuu wa chama, nitasimamia utekelezaji wa ilani hiyo katika halmashauri zote za wilaya zinazoongozwa na Chadema.”
Aliwataka mameya na wenyeviti wa halmashauri zilizo chini ya chama hicho kuisoma, kuilewa na kuitekeleza ilani hiyo aliyosema sehemu kubwa imeigwa na CCM ili kuwaonyesha wananchi tofauti ya vyama hivyo kivitendo linapokuja suala la maendeleo na maslahi ya umma.
Mshikamano kuelekea 2020
Akizungumzia mkakati wake kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka 2020, Dk Mashinji alisema dhamira yake kuu ni kuwaunganisha wanachama, viongozi, wapenzi na wafuasi wa Chadema kwa kutoa fursa kwa kila mmoja kutimiza wajibu wake kufikia lengo la kushika dola miaka mitano ijayo.
“Kila mwana Chadema aweke lengo la kukijenga chama tayari kwa ushindi 2020. Tuige tabia ya maji mtoni ambayo kila tone dogo hujiunganisha na tone lingine na kufanya mafuriko makubwa yanayotembea,” alisema.
Mashinji ni nani?
Akisimulia historia yake fupi, Dk Mashinji alisema alizaliwa mjini Musoma mkoani Mara, makuzi yake ni jiji la Mwanza na kusomea Uganda namna ya kuishi katika mazingira magumu, zikiwamo vurugu.
“Ninachomaanisha ni kutuma salaam kwa watani zetu kuwa mimi siyo mtu legelege hata kidogo,” alisema na kuibua shangwe ukumbini.
Alisema kwa kuzaliwa mkoani Mara, amefanikiwa kubeba tabia ya ujasiri, uthubutu na kutohofia lolote wanalosifika kuwa nalo watu wa mkoa huo na papo hapo amerithi tabia ya upole, lakini wenye msimamo wa jamii ya mkoa wa Mwanza na kuahidi kuzichanganya pamoja katika uongozi wake.
Maoni ya wachambuzi
Wakitoa maoni yao wachambuzi wa masuala ya siasa wamesema chama hicho kinahitaji mtu atakayekijenga ili kiendelee kuwa chama chenye nguvu nchini.
Profesa wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Rucu), Gaudence Mpangala alisema chama hicho kinahitaji mtu mwenye msimamo na uwezo wa kukabiliana na mbinu kali za chama tawala CCM.
Alisema katibu mkuu ndiye mtendaji wa chama, kwa hiyo nafasi hiyo inahitaji mtu mwenye uwezo wa kuwaleta watu pamoja na kukifanya chama kuwa kimoja.
“Siwezi kumzungumzia huyu aliyeteuliwa jana (Mashinji) kwa sababu simfahamu. Bila shaka Baraza Kuu limeona anafaa ndiyo maana amepitishwa. Wengi tulitarajia watu wenye majina makubwa kushika nafasi hiyo,” alisema Profesa Mpangala.
Hata hivyo, alisema hajashtushwa na uamuzi huo kwa sababu waliompitisha wanamfahamu vizuri na wanaamini atatekeleza majukumu yake vizuri.
Katibu Mkuu wa NCCR – Mageuzi, Mosena Nyambabe alisema nafasi ya katibu mkuu wa chama inahitaji mtu mkali ambaye atawasimamia watendaji wengine wa chini yake, maadili na katiba ya chama chake.
“Siwezi kumzungumzia huyo (Mashinji) moja kwa moja kwa sababu simfahamu. Lakini ana kazi kubwa ya kukijenga chama chake na kuhakikisha kwamba katiba ya chama inafuatwa,” alisema.
Nyambabe aliongeza kuwa ana imani Mashinji atafanya kazi vizuri kwa sababu viongozi wa juu wa Chadema wameridhia uteuzi wake.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Emily Jonathan alisema hana uhakika kama Mashinji anaweza kuvaa viatu vya Dk Slaa kwa sababu katibu huyo mkuu wa zamani wa Chadema alikuwa na nguvu na ushawishi wa kipekee katika uongozi.
Alisema pengo la Dk Slaa limeonekana wakati wote tangu alipoondoka Chadema. Alisema mtu wa kuziba pengo hilo anatakiwa kuwa na haiba yake au kuwa na mtindo mwingine wa uongozi ambao utamfanya kuwa na ushawishi kwa wanachama na viongozi wenzake.
Imeandikwa na Peter Saramba na Peter Elias
No comments:
Post a Comment