Rais John Magufuli ameendelea kuunda serikali yake, safari hii akifanya mabadiliko makubwa katika uteuzi wa wakuu wa mikoa 26 ya Tanzania Bara.
Katika uteuzi uliotangazwa jana, karibu nusu ya wakuu wa mikoa wa zamani wametemwa, huku wakuu wa wilaya watatu wakipandishwa.
Katika uteuzi huo, Dk Magufuli ameteua wakuu wa mikoa wapya 13, kuwatosa wa zamani 12, kuwahamisha vituo watano na wengine saba kubaki katika vituo vyao.
Katika uteuzi huo, sura nne miongoni mwa wakuu wa mikoa wapya ni za majenerali wastaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Wamo pia mawaziri wanne wa Serikali ya Kikwete, akiwamo aliyekuwa Naibu Waziri wa Elimu, Anne Kilango Malecela, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Tamisemi) Aggrey Mwanri, Godfrey Zambi aliyekuwa Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika na aliyekuwa Naibu Waziri wa Afya, Dk Stephen Kebwe.
Katika taarifa ya Ikulu iliyotangazwa na Kaimu Katibu Mkuu Kiongozi Mussa Iyombe, wakuu hao wapya wa mikoa wataapishwa kesho.
Katika mabadiliko hayo, taarifa ya Ikulu ilionyesha kuwa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, badala ya Saidi Meck Sadiki.
Sadiki amekwenda kushika nafasi ya Amos Makala aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro ambaye amehamishiwa Mbeya.
Sura mpya
Majenerali wanne kati ya 16 waliostaafu Machi 5, wameteuliwa kuwa wakuu wapya wa mikoa ambao ni Brigedia Jenerali Emmanuel Maganga aliyekuwa Mkuu wa Tawi la Ukaguzi jeshini, Meja Jenerali Ezekiel Kyunga aliyekuwa Mkuu wa Chuo cha Ukamanda na Unadhimu kilichopo Duluti mkoani Arusha na Meja Jenerali Raphael Muhuga wa JKT.
Kadhalika katika uteuzi huo, Rais Magufuli amemteua Luteni Mstaafu Chiku Galawa kuwa Mkuu wa Mkoa mpya wa Songwe. Kabla ya uteuzi huo Galawa alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.
Sura nyingine mpya ni ya Kamishna Msaidizi Mwandamizi Mstaafu wa Polisi, Zelote Steven ambaye alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Musoma amepanda cheo kuwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Martin Shigela ambaye alikuwa msaidizi wa Rais masuala ya Siasa ameteuliwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Antony Mtaka aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Hai ameteuliwa kuwa mkuu wa Mkoa wa Simiyu na aliyekuwa Mhandisi wa Tanroad, Mathew Mtigumwe, amekwenda Singida.
Katika mabadiliko hayo, wakuu wa mikoa 12 wameondolewa katika vituo vyao vya kazi na hawakupangiwa maeneo mengine.
Wakuu wa mikoa ambao hawajaguswa katika mabadiliko hayo ni Halima Dendego (Mtwara), Dk Rehema Nchimbi (Njombe), Joel Bendera (Manyara), Said Mwambungu (Ruvuma), Felix Ntibenda (Arusha), Amina Masenza (Iringa) na Mhandisi Evarist Ndikilo (Pwani).
Wapya walonga
Wakizungumza saa chache baada ya uteuzi huo, baadhi ya wakuu wa mikoa wapya walimshukuru Rais Magufuli na kuahidi kufanya kazi kwa kuendana na kasi yake.
Kwa upande wake, Malecela alisema kazi yake ni kusukuma maendeleo kwa Watanzania, kwa hiyo wakazi wa Shinyanga wasiwe na wasiwasi.
“Shinyanga napajua vizuri, nilisoma huko. Kwa hiyo Rais hajakosea kunipeleka mkoa huo,” alisema.
Kwa upande Dk Kebwe alisema bado hajapata taarifa rasmi, bali alizisikia kwa watu mbalimbali na katika mitandao ya kijamii.
“Wengine wameniambia wameona katika mitandao ya kijamii na mimi huwa siamini. Ila kama ni kweli nimestuka na uteuzi huu kwa sababu sikuutarajia,” alisema
Kwa upande wake, Mtaka alisema anamshukuru Rais Magufuli kwa kumteua kuwa ni miongoni mwa wakuu wa mikoa vijana.
“Ninachoweza kusema kwa sasa ni kumshukuru Rais Magufuli, kwani hakujali umri katika uteuzi wake,” alisema Mtaka ambaye pia ni mkuu wa wilaya ya Hai.
Mabosi Takukuru, TRA rasmi
Wakati huohuo, Rais Magufuli amewathibitisha watendaji wakuu wa taasisi mbili za Serikali, akiwamo Alphayo Kidata, aliyekuwa Kaimu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ambaye anakuwa Kamishna Mkuu wa TRA na Valentino Mlowola aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ambaye anakuwa Mkurugenzi Mkuu wa (Takukuru).
No comments:
Post a Comment