ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, March 29, 2016

Chad yaitia TFF hasara Sh. ml 250

Kujiondoa kwa Chad katika michuano ya awali kusaka tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika, kumeisababisha Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), hasara ya zaidi ya Sh. milioni 250, imebainika.

Chad ilijitoa dakika za mwisho kurudiana na Taifa Stars katika mechi iliyopangwa kuchezwa juzi kwenye Uwanja wa Taifa, huku maandalizi yote yakiwa yamekamilika.

Leo, TFF inatarajia kutangaza hasara iliyotokana na mechi hiyo kufutwa, lakini Nipashe imebaini kuwa hasara hiyo ni zaidi ya Sh. milioni 250.

Taarifa kutoka ndani ya TFF zilidai kuwa, gharama hizo ni pamoja na kusafirisha wachezaji, kambi, posho, gharama za waamuzi, kamisaa na tiketi.

Jana, alipoulizwa Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa kuhusu hasara waliyopata, alisema kwa sasa bado wanaendelea na kazi ya kuhakiki kiasi cha fedha kilichotumika kwa ajili ya maandalizi ya mechi ya kwanza iliyofanyika N’Djamena na ile ya marudiano iliyotarajiwa kuchezwa juzi kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Mwesigwa alisema kwamba TFF imepata hasara na bado itaendelea kusikitishwa na uamuzi wa kujiondoa uliofanywa na Chad.

“Tumepata hasara kubwa, hado kesho (leo) bado kuna gharama zinaendelea kutumika,” Mwesigwa alisema kwa kifupi.
Alisema kama zilivyo nchi nyingine za Afrika kutoweka wazi taarifa za ujio wake, Chad pia walionekana ‘wazembe’ katika kila jambo walilokuwa wanaulizwa na TFF.

Aliongeza kwamba Chad walionekana kutotaka mawasiliano mara kwa mara na TFF na hata walipokuwa wakijiandaa na mechi ya kwanza, ambayo Taifa Stars ilishinda bao 1-0, viongozi wa nchi hiyo hawakuonyesha ushirikiano.

Alisema kwamba kikosi cha Stars kinatarajia kuvunja kambi leo na wachezaji wake kutoka nje, Samatta na Thomas Ulimwengu wa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) walitarajia kuondoka pia.

Wakati huohuo, TFF kurejesha fedha mashabiki wa soka waliokata tiketi kwa ajili ya kuingia uwanjani juzi kuishangilia Stars, watarejeshewa fedha zao.

TFF imeeleza kupitia kwa Afisa Habari wake, Baraka Kizuguto kuwa mashabiki watarejesha fedha hizo katika vituo vinne walivyonunua tiketi.

CHANZO: NIPASHE

No comments: