Saturday, March 5, 2016

Chadema Monduli yamkubali Magufuli

Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Monduli, Isaack Joseph
BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Monduli mkoani Arusha ambalo linaundwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), limemuunga mkono kwa vitendo juhudi zinazofanywa na Rais John Magufuli za `kutumbua majipu’, wakisema hatua hiyo inarudisha heshima na nidhamu katika utumishi wa umma.

Aidha, jana walichukua hatua ya kupendekeza katika mamlaka husika kusimamishwa kazi kwa watumishi watatu wa Idara ya Ardhi wilayani hapa, kupisha uchunguzi wa hasara ya zaidi ya Sh milioni 700 kutokana na kuuzwa kwa viwanja 100 bila kufuata taratibu. Aidha, wametaka baada ya uchunguzi huo wahusika wafikishwe mahakamani kushtakiwa.

Wakimzungumza ndani ya kikao kwa nyakati tofauti, walisema wanamuunga mkono kwa dhati Rais Magufuli aliyejipambanua kuwa anakerwa na tabia ya ufisadi, rushwa na matumizi mabaya ya madaraka zinazofanywa na watumishi wa umma.

Akitangaza maazimio hayo mbele ya kikao cha Baraza la Madiwani juzi baada ya kukaa kama kamati, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Isaack Joseph maarufu kwa jina la Kadogoo, alisema maamuzi yote hayo ni kuhakikisha wanarejesha nidhamu ya utumishi serikalini na kuunga mkono jitihada za Rais kurejesha nidhamu kwa watumishi wa umma.

“Tumefikia uamuzi huu si kwa kukurupuka tumefanya uchunguzi tumejiridhisha kwa kushirikisha kila aliyestahili kushirikishwa na kufikia maamuzi haya ya kuwasimamisha kazi watumishi hawa wa idara ya Ardhi,” alisema.

Aliongeza kuwa, “ wamesimamishwa ili kupisha uchunguzi rasmi na ukikamilika wafikishwe katika vyombo vya sheria kwa hatua zaidi za kisheria na stahiki ili hatua zaidi zichukuliwe.”

Aliwataja watumishi ambao wamekumbwa na maamuzi hayo kuwa ni Leonard Haule ambaye ni mpimaji ardhi, Ofisa Ardhi mteule Kitundu Mkumbo na Mrasimu ramani, Leoni Mkwavi ambapo wanadaiwa kuuza viwanja na fedha kutoziwasilisha kwenye halmashauri na pia baadhi ya viwanja walivyouza kutoviingiza katika ramani ya halmashauri.

Alivitaja viwanja vilivyouzwa na watumishi hao kuwa vipo eneo la CDTI Monduli Mjini na kutaja idadi yake kuwa ni zaidi ya viwanja 100 ambapo halmashauri hiyo imeweza kukusanya fedha kiasi cha Sh milioni 500 pekee mpaka Desemba mwaka jana na kupata hasara ya Sh milioni 700.

Wakizungumzia kusimamishwa kwa watumishi hao, baadhi ya watumishi wa halmashauri hiyo walipongeza uamuzi huo na kwa kusema hauna chembe ya malalamiko kwani umefuata taratibu kutokana na malalamiko mengi yaliyopo Monduli baada ya kuuzwa kwa viwanja hivyo.

Akizungumza kwa niaba ya watumishi wenzake, Mhandisi wa Ujenzi wa Halmashauri hiyo, Daudi Sabiga alisema huo ni utaratibu wa kiutumishi na kwamba utasaidia kuleta nidhamu kwa watumishi wengine.

‘’Unajua hivi sasa kuna hii sera ya utumbuaji majipu katika maeneo mengine unasikia mtumishi kafukuzwa kazi kwa tuhuma ndogo ambayo haina uthibitisho… lakini kwa hii ya hapa kwetu imefanyiwa utafiti wa kutosha na wahusika kubainika na hatua zimechukuliwa za kuwasimamisha kama taratibu za utumishi zinavyotaka na ikibainika bila shaka uhusika wao, basi hatua zaidi za kinidhamu zinachukuliwa,” alisema Sebiga.

Aidha, madiwani hao wameazimia kwa pamoja kumuomba Rais Magufuli kuutupia macho Wakala wa Umeme na Ufundi Tanzania (TEMESA) mkoani Arusha kwa kile walichodai nao ni `jipu’ kutokana na kutoa huduma zisizoridhisha na zenye gharama kubwa.

Wamesema wakati wakisubiri `jicho’ la Rais Magufuli ndani ya taasisi hiyo, halmashauri ya Monduli haitapeleka vifaa na magari yao Temesa mkoani hapa kwa ajili ya matengenezo.

Akifafanua, Mwenyekiti huyo wa halmashauri hiyo alisema wameshangazwa na kupokea hati ya madai kutoka Temesa ya matengenezo ya kuweka kioo cha gari cha mbele cha Toyota Land Cruiser na raba zake inayowataka kulipa Sh 900,000 wakati gharama halisi katika maeneo mengine ni Sh 120,000.

“Ndugu zangu waheshimiwa madiwani huu ni wizi na hili la Temesa Arusha ni jipu ambalo Rais anatakiwa kulitumbua. Kutokana na huu ushahidi tulionao tumeazimia kabisa bila woga kutopeleka vifaa vyetu vyote pale Temesa kwa matengenezo na tutapeleka katika gereji nyingine ambazo zimeidhinishwa Kisheria,’’ alisema.

Maamuzi hayo mazito ya madiwani wa Halmashauri ya Monduli yamefanywa katika kikao chao cha kwanza cha baraza la kawaida la madiwani pamoja na maamuzi hayo kilipokea taarifa mbalimbali za kamati kwa robo mwaka ya Oktoba hadi Desemba, mwaka jana.

HABARI LEO

No comments: