Sunday, March 6, 2016

CHUO KIKUU CHA MZUMBE CHAPONGEZWA KWA KUIMARISHA ELIMU NCHINI

 Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Rajabu Rutengwe (kushoto) akimkabidhi madawati  Kaimu Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mindu, Bw. Samwel Mdee (wa tatu kulia) yaliyochangwa na wanafunzi wa somo la Menejimenti wa Chuo Kikuu Mzumbe mwishoni mwa wiki. Wengine ni Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Profesa Josephat Itika (wa pili kulia), Mkuu wa Skuli ya Utawala na Menejimenti, Dkt. Stella Kinemo (kulia) na wanafunzi wa shule hiyo ya msingi.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Rajabu Rutengwe aliyekaa baada ya kuikabidhi Shule ya Msindi Mindu madawati  yaliyochangwa na wanafunzi wa somo la Menejimenti katika Chuo Kikuu Mzumbe mwishoni mwa wiki.  Wengine ni Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Profesa Josephat Itika (wa pili kulia), Mkuu wa Skuli ya Utawala na Menejimenti,  Dkt. Stella Kinemo (kulia); Mratibu wa Mradi wa Madawati, Bw. Aloyce Gervas (kushoto), muwakilishi wa wanafunzi wa Menejimenti, Bw. Vivans Roseline (wa pili kushoto) na wanafunzi wa shule hiyo ya msingi.

Serikali imekipongeza chuo kikuu Mzumbe kwa juhudi zake za kuboresha elimu nchini kwa kujitolea kuchangia vifaa hasa madawati na mahitaji mengine katika shule za msingi na sekondari zilizo karibu na chuo hicho. 

 Akiongea baada ya kupokea madawati 20 kutoka uongozi wa chuo hicho mwishoni mwa wiki, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Rajabu Rutengwe alisema msaada huo ni mfano mzuri wa kuigwa na wadau wengine wa maendeleo kote nchini. Madawati hayo kwa shule ya msingi ya Mindu yametolewa kutokana na michango ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa somo la Menejimenti kwa matumizi ya wananfunzi wa shule ya msingi Mindu.
“Ubunifu huu ni mfano wa kuigwa katika maeneo yetu ili kukabiliana na changamoto zinazotukabili,” alisema Dkt. Rutengwe. 
 Kupitia ubunifu huo, Mkuu huyo wa mkoa alizindua kampeni itakayokuwa na mfuko maalum kwa ajili ya kukusanya rasilimali ili kutatua changamoto zilizopo katika shule za mkoa wa Morogoro. Alifafanua kwamba waraka wa serikali wa elimu bure inalenga swala zima la ada na tozo nyingine hivyo jamii bado inapaswa kuchangia ili watoto waweze kusoma katika mazingira mazuri. 
 Kwa upande wake, Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Profesa Josephat Itika alisema chuo chake kimekuwa na kawaidia ya kujitolea kusaidia jamii inayowazunguka kwa kujenga mahusiano mazuri katika sekta ya elimu na afya. Alisema ni muhimu kwa taasisi za umma na binafsi kujitolea kuchangia sekta ya elimu kwani ndio msingi wa maarifa kwa vijana ambao ndio nguvu kazi ya taifa. 
 ‘Ni muhimu kwa mashirika binafsi na taasisi za umma kujitolea kuwekeza katika elimu ili kuisaidia serikali kukabiliana na changamoto katika shule za msingi na sekondari,” alisema Prof.Itika. 
 Alisema changamoto zilizopo katika shule ya msingi Mindu ni kielelezo cha shule nyingine nchini hivyo ni jukumu la kila mmoja kuchangia rasilimali ili kupunguza changamoto hizo hasa madawati na matundu ya choo. 
 Akizungumza kwa niaba ya mwanafunzi wenzake Mzumbe, Bw.Vivans Roseline alisema walichangia baada ya kuguswa kutokana na mazingira ya shule hiyo kuwa magumu. Alisema zoezi hilo halitaishia kwenye madawati tu bali watachangishana kuhakikisha changamoto zote katika shule ya msingi Mindu zimekwisha. 
 Naye Kaimu Mkuu wa shule ya msingi Mindu, Bw. Samwel Mdee alishukuru kwa msaada huo na kuomba waendelee kusaidia zaidi ili watoto waweze kusoma katika mazingira mazuri. Alizitaja baadhi ya changamoto zinazowakabili kuwa uhaba wa vitendea kazi kwa walimu, matundu ya choo, maktaba, ukosefu wa nyumba za walimu na ukosefu wa maji. Chuo kikuu Mzumbe kuliahidi kutoa jumla ya shilingi milioni 5 ili kusaidia katika kufanya ukarabati katika shule hiyo.

No comments: