ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, March 15, 2016

Kamati ya Bunge yaikamia Wizara ya Nishati na Madini



Waziri wa Nishati na Madini, Sospeter Muhongo.
By Beatrice Moses na Raymond Kaminyoge, Mwananchi

Dar es Salaam. Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini imekamia kuihoji Wizara ya Nishati na Madini na Kamishina wa Bajeti kwa nini walikwamisha utekelezaji wa miradi 21 ya maendeleo ukiwamo wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam kwa kutotoa fedha.

Hayo yalisemwa jana katika kikao cha kamati hiyo inayoongozwa na Martha Mlata, ambapo wajumbe walijadili suala hilo na kuonyesha kukerwa kwao baada ya kubaini kiasi cha Sh 109.85 bilioni zilipitishwa katika Bunge la Bajeti mwaka 2015/ 2016 kwa ajili ya kutelekeza miradi hiyo.

Kamati hiyo ilibaini pia kwamba kati ya miradi 25 iliyotengewa fedha, ni miradi minne tu iliyopewa fedha huku miwili ikizidishiwa fedha. Baadhi ya miradi ambayo ilitengewa fedha lakini Serikali ilishindwa kutoa ni za mradi wa ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam uliotengewa Sh10 bilioni na wa Kituo cha Kinyerezi MW 185 uliotengewa Sh40 bilioni.

Wakati Serikali ikishindwa kutoa fedha kwa ajili ya miradi hiyo, kamati imebaini mradi wa 220 KV wa Makambako – Songea ulitengewa Sh 22.6 bilioni lakini ulipewa Sh 30.2 bilioni na mradi wa Tanesco wa ukusanyaji madeni kutoka taasisi mbalimbali ulitengewa Sh 27.6 bilioni lakini ulipewa Sh 164 bilioni.

“Tunafahamu kwa sasa wanajiandaa kwa ajili ya bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017. Tutakutana nao tuone mipango yao kama wiki mbili zijazo, tutawahoji sababu ya kushindwa kutoa fedha hizo. Hii ni miradi muhimu na ya maendeleo,” alisema Mlata ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu.

Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo, Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ali Kessy alielezea kukerwa na hali hiyo akisema miradi hiyo ikikamilika itapunguza kero ya kukosekana kwa huduma ya umeme inayowakabili wananchi wengi, lakini pia Serikali ingejiongezea kipato chake kutokana na huduma hiyo kulipiwa.

Katika mwaka 2015/16, Wizara ya Nishati na Madini ilisema imeamua kuongeza mitambo mingine ya kuzalisha umeme kwa kiasi cha MW 185 katika Mradi wa Kinyerezi – I. Serikali ilisema imetenga fedha za ndani jumla ya Sh 40 bilioni kwa ajili ya kutekeleza kazi ya usanifu wa mradi huo ikiwa ni pamoja na kuajiri mshauri wa mradi.

Mitambo hiyo ilitajwa kuwa itasaidia kupunguza utegemezi wa mitambo ya kuzalisha umeme kwa kutumia nguvu za maji ambayo huathiriwa na ukame, na mafuta ambayo ni ghali.

Katika hatua nyingine, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad amesema amekwama kufanya ukaguzi katika halmashauri 20 kutokana na kutopewa fedha zilizoidhinishwa na Bunge.

Akizungumza jana mbele ya Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Profesa Assad alisema aliomba kupewa Sh16 bilioni lakini aliambulia Sh8 bilioni, hivyo ameshindwa kufanya ukaguzi uliokusudiwa.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Kangi Lugola alisema ukwamishaji huo wa ukaguzi ni kikwazo kwao kwa sababu wamekuwa wakifanya kazi kwa kutegemea ripoti za CAG.

Wakati huohuo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Balozi Adadi Rajabu amesema mikakati ya kamati yake itakuwa kuisimamia Wizara ya Mambo ya Nje ili iweze kutafuta fedha za kujenga majengo yake kwenye balozi za nje ya nchi kwa lengo la kupunguza gharama.

Akizungumza jana mara baada ya mafunzo ya wabunge wa kamati hiyo kuhusu utendaji wao wa kazi, Balozi Rajabu alisema ofisi za balozi nyingi ziko kwenye majengo ya kupanga ambayo ni gharama kubwa katika baadhi ya nchi.

Alisema sera ya wizara hiyo ni kuwa na majengo yake yenyewe kwenye nchi mbalimbali ambazo Tanzania zina ubalozi.

“Kwa hiyo kamati itahakikisha inasimamia na kushauri njia zitakazowezesha balozi zetu kuwa na majengo yetu wenyewe, tunapoteza fedha nyingi kulipa pango ugenini,” alisema Rajabu ambaye alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe.

Rajabu alisema kamati hiyo itaishauri wizara kuweka kupaumbele kwa kujenga ushirikiano wa kibalozi kwenye nchi ambazo tunashirikiana kiuchumi.

No comments: