ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, March 15, 2016

Kimanda wa Yanga aibukia Ubelgiji



Constantine Kimanda
By Edo Kumwembe, Mwananchi -- ekumwembe@mwananchi.co.tz

Brussels, Ubelgiji. Miaka 21 baada ya kuondoa nchini, beki wa zamani wa Yanga na timu ya taifa ya Burundi, Constantine Kimanda amesema bado ana mapenzi na timu hiyo na anawakumbuka wachezaji wenzake wa zamani pamoja na mashabiki wa timu hiyo.

Akizungumza na gazeti hili nyumbani kwake nchini Ubelgiji, Kimanda mwenye umri wa miaka 46, alisema maisha yake soka ya Tanzania yalikuwa na mafanikio makubwa.

“Yalikuwa maisha mazuri ya soka, Tanzania ilinikomaza na kunifungulia milango yangu ya maisha. Bila ya kuja Tanzania si ajabu nisingefika huku,” alisema Kimanda aliyechukua uraia wa Ubelgiji kwa sasa.

Kimanda licha ya jina kubwa aliloacha Tanzania, lakini amefunua kuwa alicheza soka kwa miezi tisa tu nchini kuanzia Januari hadi Septemba 1994 na amesimulia zaidi jinsi alivyoondoka akiwa ameambatana na nyota wa zamani wa Yanga, Marehemu Method Mogella. “Nasikia nakumbukwa Tanzania, lakini nilicheza soka kwa miezi tisa tu.

Sikutimiza hata mwaka. Wala sikuwa nataka kuondoka, lakini yule katibu Mpondela (marehemu George Mpondela) ndiye aliyetuuza. Kuna timu ya Uarabuni Sharjah FC ilikuwa inataka wachezaji wawili kutoka Tanzania.

Alikuja mchezaji wa zamani wa Yanga, Ahmed Amasha ndiye akatuchagua mimi na Method.”

“Method aliondoka na Mpondela, mimi nikaondoka baada ya siku mbili kwenda kujiunga nao. Nakumbuka Mpondela alipewa fedha nyingi, lakini sikumbuki ni kiasi gani. Na sisi pia tulipewa fedha nyingi. Hata hivyo tulivyopimwa afya, Method iligundulika kuwa alikuwa na matatizo ya kifua, akarudishwa. Baada ya miezi michache nikasikia amefariki,” alisema Kimanda.

Kwa sasa Kimanda ni mfanyakazi katika idara ya ustawi wa jamii jijini Brussels na ameoa mke kutoka kwao Burundi anayeitwa Veronica ana watoto wanne; Monica (10) Yasser (8), Rami (5) Amel (1).

Anakiri anayakumbuka kwa karibu maisha ya Tanzania huku akidai kwamba ameendelea kuwasiliana kwa karibu na baadhi ya wachezaji aliocheza nao katika kikosi cha Yanga cha mwaka 1994 ambacho msimu huo hakikufanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu.

“Bado nawakumbuka mashabiki na viongozi. Nawakumbuka wachezaji wenzangu wa zamani. Nimekuwa nikiwasiliana na Sekilojo Chambua, Edbily Lunyamila na wengineo. Nasikia Nico Bambaga alifariki, ni kweli?” alihoji Kimanda.

No comments: