Advertisements

Wednesday, March 30, 2016

Magufuli afyeka mishahara ya vigogo



Rais John Magufuli 
By Rehema Matowo, Mwananchi rmatowo@mwananchi.co.tz

Chato. Rais John Magufuli ametangaza kiama cha watendaji wakuu wa mashirika na taasisi za umma waliojipangia mishahara minono kufikia Sh40 milioni akiahidi kuifyeka hadi kiwango kisichozidi Sh15 milioni kuanzia bajeti ijayo ya fedha ikiwa ni punguzo la asilimia 63.

“Atakayeona kiwango hicho ni kidogo namshauri aanze kutafuta kazi sehemu nyingine kwa sababu hatuwezi kuendelea kulipana mishahara minono kiasi hicho katikati ya wananchi wanaoishi katika lindi la umaskini,” alisema Rais Magufuli na kushangiliwa kwa nguvu na wananchi.

Akihutubia mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Mazaina mjini Chato jana katika siku yake ya kwanza nyumbani kwake tangu achaguliwe kushika wadhifa huo, Rais Magufuli aliahidi kupandisha mishahara ya watumishi wa chini ili kupunguza tofauti ya kipato kati yao na wale wa juu. “Katika Serikali ninayoongoza, sitegemei kumlipa mtumishi zaidi ya Sh15 milioni; tayari nimeunda tume kushughulikia suala hilo,” alisema na kuongeza: “Kiwango tunachopunguza kutoka kwenye mishahara minono ya wakubwa tutawaongezea watumishi wa chini ambao baadhi wanalipwa mishahara midogo inayoanzia Sh300, 000.

Kodi ya mishahara

Akizungumzia malalamiko ya muda mrefu ya wafanyakazi kuhusu kodi kwenye mishahara, Rais alisema Serikali inakusudia kupunguza kiwango hicho hadi kufikia tarakimu moja, akibainisha kuwa haitazidi asilimia tisa kuanzia bajeti ijayo ya Serikali.

Ushuru wa mazao

Rais pia aligusia suala la kodi nyingi kwenye mazao aliyosema ni mzigo kwa wakulima na kuahidi kuzipunguza ili pamoja na kuwapa nafuu wakulima ambao ndiyo hubeba mzigo wa kodi hizo, pia kuleta tija kwenye sekta ya kilimo kinachoajiri zaidi ya asilimia 75 ya Watanzania. “Tunalenga kuhakikisha kodi na ushuru kwenye mazao yetu hayazidi tatu au mbili; hii itawawezesha wakulima siyo tu kunufaika na kilimo, bali pia kumudu ushindani wa soko la mazao ndani na nje ya nchi,” alisema.

Shule zenye matokeo mabaya

Rais alisema hatakuwa tayari kutumia mabilioni ya fedha za umma kutekeleza sera ya elimu bure ya msingi halafu wanafunzi wafeli darasa la saba au kupata alama sifuri katika mitihani ya kidato cha nne. “Maofisa elimu, walimu wakuu, wakuu wa shule, wajumbe kamati na bodi za shule zilizofanya vibaya katika matokeo yaliyopita wajitathmini na kutafakari kama wanastahili kuendelea kushika nafasi zao,” alisema.

Aliwaomba Watanzania kila mmoja kwa nafasi na uwezo wake, kujitokeza kuchangia maendeleo ya elimu, hasa changamoto ya madawati na vyumba vya madarasa iliyotokana na sera ya elimu bure ya msingi.

No comments: