
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akipokea Taarifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali kutoka kwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali Professa Mussa Assad Ikulu jijini Dar es salaam jana Machi 28, 2016.(Picha na Ikulu)
Rais John Magufuli, ambaye amejipa kazi ya “kutumbua majipu”, sasa anaweza kufanya kazi yake vizuri zaidi baada ya kukabidhiwa ripoti tano na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ambazo anaweza kuzitumia kama kitendea kazi.
Tangu aingie Ikulu, Rais Magufuli na Serikali yake amekuwa akifanya kazi ya kuibua uozo kwenye taasisi za Serikali, kusimamisha na kutengua uteuzi wa watumishi wa umma wanaojihusisha na ufisadi na wakati fulani amekuwa akiitaja ripoti iliyopita ya CAG kuwa ndiyo iliyoanika uozo anaofanyia kazi.
Jana, “mtumbua majipu” huyo alikabidhiwa ripoti ya kwanza ya CAG tangu aapishwe kuwa Rais Novemba 5 mwaka jana na sasa ana kitendea kazi rasmi cha kufanyia kazi.
CAG Mussa Assad alimkabidhi Rais Magufuli taarifa ya ukaguzi wa hesabu za Serikali ikiwa ni kwa mujibu wa Katiba inayomtaka akabidhi ripoti hizo kwa Rais kabla ya mwisho wa mwezi Machi.
Taarifa iliyotolewa na Gerson Msigwa, kaimu mkurugenzi wa mawasiliano – Ikulu, Rais Magufuli, ambaye aliwaomba wabunge kumpa ushirikiano katika kutekeleza kazi za wananchi wakati akizindua Bunge Novemba 20, atazikabidhi ripoti hizo kwenye chombo hicho ndani ya siku saba za mwanzo za Mkutano wa Tatu wa Bunge la Kumi na Moja utakaofanyika mjini Dodoma kuanzia Aprili 19.
“Rais Magufuli amempongeza CAG na timu yake kwa kuandaa taarifa hiyo na ametoa wito kwa chombo hicho kuendelea kufanya kazi kwa uhuru na ufanisi. Ameahidi kuwa serikali itatoa ushirikiano wa kutosha kufanikisha kazi zake,” inasema taarifa hiyo.
Madudu aliyoyaona CAG
Kwa kawaida ripoti hizo zimekuwa zikiibua ufisadi uliofanyika katika taasisi mbalimbali nchini, ukiukwaji wa kanuni na sheria za manunuzi, fedha na ajira huku zikiibua mijadala mikubwa bungeni, ambayo imewahi kuwang’oa mawaziri kwa shinikizo la Bunge.
Mwaka 2012, ripoti ya CAG iling’oa mawaziri sita na manaibu wawili wa Serikali ya Awamu ya Nne baada ya mjadala mkali bungeni wa taarifa ya CAG.
Mawaziri ambao waling’olewa ni Mustafa Mkulo, aliyekuwa Waziri wa Fedha, Dk Hadji Mponda (Afya na Ustawi wa Jamii), William Ngeleja (Nishati na Madini), Dk Cyril Chami (Viwanda na Biashara), Omar Nundu (Uchukuzi) na Ezekiel Maige (Maliasili na Utalii).
Panga hilo la mabadiliko liliwakumba pia manaibu waziri wawili, Dk Lucy Nkya (Afya na Ustawi wa Jamii) na Dk Athumani Mfutakamba (Uchukuzi).
Mkulo alituhumiwa kuhusika katika ubadhirifu wa Shirika Hodhi la Mali za Mashirika ya Umma (CHC), akielezewa kuwa alipoteza uaminifu na uadilifu kiasi cha kusema uongo bungeni ili kuficha maslahi binafsi katika ofisi za umma.
Pia Dk Chami alitajwa kumkingia kifua mkurugenzi mkuu wa Shirika la Viwango la Taifa (TBS), Charles Ekelege, ambaye alituhumiwa kujitetea kuwa kuna kampuni zimepewa kazi ya kukagua magari yanayokuja nchini, ambayo yanalipwa dola 37 milioni za Marekani, lakini kamati ya wabunge iliyokwenda kuhakiki nchini Singapore na Hong Kong, hawakukuta kampuni hizo.
Waziri mwingine, Dk Mponda alidaiwa kushindwa kusimamia matumizi bora ya fedha za umma kiasi cha kuruhusu nyumba yake kukarabatiwa kwa mamilioni ya fedha.
Ngeleja, ambaye ni mbunge wa Sengerema, alituhumiwa kushindwa kusimamia sekta ya madini na umeme, kuweko kwa manunuzi makubwa ya mafuta ya kuendesha mitambo ya IPTL ambayo yameongezwa bei.
Pia Maige alituhumiwa kushindwa kudhibiti ubadhirifu katika wizara yake kama ulivyobainika katika ugawaji wa vitalu vya uwindaji wa kitalii na usafirishaji wa wanyama hai nje ya nchi.
Nundu, waziri mwingine aliyekuwamo kwenye sakata hilo, alituhumiwa kuingilia mchakato wa kumpata mzabuni wa kujenga gati namba 12 na 13 katika Bandari ya Dar es Salaam.
Ukaguzi maalumu
Pia ripoti ya ukaguzi maalum wa Akaunti ya Tegeta Escrow iliyotolewa mwaka juzi ilianika uchotwaji wa Sh306 bilioni kutoka kwenye akaunti hiyo, fedha zilizohifadhiwa kusubiri kumalizika kwa mgogoro wa kimkataba baina ya Shirika la Umeme (Tanesco) na kampuni binafsi ya ufuaji nishati hiyo, IPTL.
Fedha hizo, ambazo hazikukatwa kodi ya Serikali, zilionekana zikiingia kwenye akaunti za mawaziri waliokuwa madarakani na wa zamani, wabunge, majaji, maaskofu na watumishi wa umma na kumlazimisha Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete kufanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri.
Ripoti ya 2013/14
Katika ripoti ya mwaka jana (2014/15), ofisi ya CAG ilibainisha ufisadi mkubwa wa fedha kwenye baadhi ya taasisi zilizokaguliwa ambazo ni taasisi 176 za serikali kuu, halmashauri 163 na mashirika 109 ya umma.
Madudu yaliyoibuliwa katika ripoti hiyo yalikuwa ni utoaji holela wa misamaha ya kodi, kuendelea kwa mishahara hewa, usimamizi mbovu wa mipango miji, madeni ya serikali kwenye mifuko ya hifadhi za jamii na Bohari Kuu ya Dawa (MSD).
Ripoti hiyo ilibainisha kuwapo kwa upungufu wa fedha za maendeleo Sh312 bilioni katika bajeti za mamlaka za Serikali za Mitaa na Sh1.8 bilioni kwa serikali kuu. Fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambazo hazikutumika lakini zilitolewa zilikuwa Sh 417 bilioni.
CAG alibainisha kudorora kwa uwekezaji wa Serikali kwenye kampuni ambazo inamiliki hisa kutokana na kuchelewa kuongeza mitaji, wakati inapohitajika ili kujiendesha bila kusubiri ruzuku.
Alitaja mashirika hayo ambayo bado yanasuasua kwa kuitegemea Serikali kuwa ni pamoja na Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara) na Shirika la Reli Tanzania (TRL) ambayo yote yanategemea ruzuku kutoka serikalini.
Katika ukaguzi wa malipo, CAG alibaini kwamba kampuni binafsi hazitumii mashine za elektroniki (EFDs), hivyo kusababisha hasara ya Sh4.4 bilioni kwa kutotumia machine hizo. Pia, alibaini kwamba taasisi za Serikali zilifanya malipo yenye thamani ya Sh4.6 bilioni bila kutumia mashine hizo.
Katika ripoti ya mwaka 2013/14, CAG alionyesha kuwa kulikuwa kuna ubadhirifu wa Sh163 bilioni katika kitengo cha maafa ambacho kipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kipindi cha miaka mitano. Fedha hizo ni wastani wa upotevu wa Sh32 bilioni kwa mwaka.
Taarifa hiyo ilionyesha kuwa mizigo inayoingizwa nchini kupitia bandari ya Dar es Salam kwenda nchi jirani haikulipiwa kodi. Mwaka 2013/2014 mizigo ya ‘transit’ iliyobaki nchini kiudanganyifu ilikuwa zaidi ya bidhaa 6,000. Kwa hiyo, kodi ya Sh836 bilioni haikulipwa kwa mizigo hiyo, sawa na 10% ya makusanyo yote ya kodi za ndani.
Gallawa aapishwa
Wakati huohuo, Rais Magufuli amemwapisha mkuu mpya wa Mkoa wa Songwe, Luteni Chiku Gallawa, ambaye hakuapishwa pamoja na wakuu wa mikoa wenzake Machi 15.
Taarifa hiyo ya Ikulu inaeleza kuwa uapisho huo ulifanyika jana, Ikulu jijini Dar es salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali akiwamo Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Gallawa, ambaye ni luteni mstaafu, anakuwa mkuu wa kwanza wa mkoa mpya wa Songwe, ulioanzishwa kwa kuugawa Mkoa wa Mbeya uliopo Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania.
No comments:
Post a Comment