Thursday, March 3, 2016

MAHOTELIA WASOKUWA NA UJUZI WA KUTOSHA MOJA YA CHANGAMOTO INAYOIKABILI SEKTA YA UTALII HAPA TANZANIA

Imebainika kuwa Tanzania inakabiliwa na changamoto ya kuwaajiri hotelia wasio kuwa na ujuzi wa kutosha katika sekta ya utalii, hali ambayo inarudisha nyuma uchumi wa nchi tofauti na nchi nyinginezo za nje ya nchi.

Hayo yalisemwa na meneja mkazi wa kampuni ya Jovago Tanzania Andrea Guzzoni alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari katika uzinduzi wa ripoti ya mwisho yenye utafiti inayohusiana na sekta ya utalii, ilikuweka wazi hali inayoikabili sekta hiyo.

Alisema kuwa sekta ya utalii kwa hapa Tanzania imekuwa ikipanda na kushuka mwaka hadi mwaka lakini bado ina changamoto ya kuwaajiri wafanyakazi kwa mazoea badala ya kuwaajiri wenye ujuzi wa kutosha hali ambayo amesema kuwa inapaswa kuangaliwa kwa upya ili kuiwezesha sekta hiyo kupanda kiuchumi.

Aliongeza kuwa ili Tanzania iweze kufikia watalii milioni mbili miaka ijayo serikali inapaswa kuangalia utaratibu wa kuwachukua mahotelia na kuwapa mafunzo ya ziada ili waweze kujifunza jinsi ya kuhudumia wageni kwani wapo wengine ambao hawajui lugha na hata jinsi ya kuhudumia wageni wanaongia nchini hali inayowafanya watalii kukosa huduma nzuri.

Aidha Bw. Guzzoni aliwataka wadau wote ndani ya sekta ya utalii kuhakikisha wanachangamkia fursa ya kujitangaza na kuonyesha utofauti wao kwa umahiri ili kusaidia watanzania wenye nia na maendeleo kufanya utalii wa ndani.

Kwa upande wake Meneja wa Kitengo cha habari na uhusiano wa kampuni hiyo Lilian Kisasa akizungumza katika uzinduzi huo kuwa, kwa hapa Tanzania sekta ya utalii imeweza kuajiri watu zaidi ya laki sita na endapo huduma nzuri zitaboreshwa katika sekta hiyo upo uwezekano wa kuajiri watu zaidi ya hapo jambo ambayo itapunguza tatizo la ajira hapa nchini na kuongeza pato la taifa.

No comments: