Thursday, March 3, 2016

Mdee akaa rumande saa 51, apanda kizimbani

By Tausi Ally na Suzan Mwillo, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wabunge wawili wa Chadema, Diwani wa Kata ya Saranga, Kimara na kada mmoja wa chama hicho wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na shtaka la kumjeruhi Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Theresa Mmbando.

Wabunge hao ni Mwita Waitara (40) wa Ukonga pamoja na Halima Mdee (37) wa Kawe aliyekaa korokoroni kwa saa 51 kabla ya kuachiwa jana mchana kwa dhamana.

Mashtaka dhidi ya wanasiasa hao yalisomwa kortini na Mwanaamina Kombakono akisaidiwa na mawakili watatu wa Serikali, Faraja Nchimbi, Mutalemwa Kishenyi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.

Mbali na Mdee na Waitara, washtakiwa wengine ni Diwani wa Saranga, Ephraim Kinyafu (33) na mfanyabiashara na kada wa chama hicho, Rafii Juma (21). Mshtakiwa mwingine, Diwani wa Kata ya Kimanga, Manase Njema (56), hakuwapo mahakamani na ilitolewa hati ya wito.

Saa 51 za Mdee mahabusu


Kabla ya kufikishwa mahakamani, Mdee alikaa rumande kwa saa 51 kisha kuachiwa kwa dhamana.

Mbunge huyo alikamatwa Jumatatu iliyopita saa 5.00 asubuhi baada ya polisi kuzingira nyumba yake na kuondoka naye kwenda Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam.

Vurugu zilizosababisha Mdee kukamatwa zilitokea Jumamosi iliyopita baada ya Mmbando kutangaza kuahirisha uchaguzi wa meya na naibu meya wa Jiji kwa zuio la muda bandia la Mahakama.

Siku iliyofuata, Mdee hakufikishwa mahakamani kama ilivyodhaniwa, bali ziliibuliwa tuhuma nyingine za kumpora Mmbando nyaraka wakati wa vurugu hizo, hivyo polisi kwenda kupekua nyumbani na baadaye ofisini kwake bila mafanikio.

Baada ya upekuzi, Mdee alirejeshwa kituoni jioni ambako kulizuka mabishano ya kisheria baina ya polisi na mawakili wake, Peter Kibatala, John Mallya yaliyoendelea hadi saa tatu usiku bila muafaka, hivyo Mdee kulala rumande tena.

Hata jana, ikitarajiwa kuwa angetolewa mapema asubuhi, mbunge huyo aliendelea kukaa ndani hadi saa saba mchana alipofikishwa mahakamani ambako aliachiwa kwa dhamana saa 8.30 mchana.

Mashtaka

Akiwasomea hati ya mashtaka, Wakili Kombakono alidai kuwa Februari 27 katika Ukumbi wa Karimjee, Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam washtakiwa hao kwa pamoja walifanya kosa hilo la kumjeruhi Mmbando na kumsababishia majeraha.

Washtakiwa walikana shtaka hilo na upande wa mashtaka ambao haukuwa na pingamizi kwa dhamana, ulidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na ukaomba ipangiwe tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Shaidi alimtaka kila mshtakiwa kujidhamini mwenyewe kwa kusaini hati ya dhamana ya Sh2 milioni kila mmoja, masharti ambayo waliyakamilisha na kuachiwa huru hadi Machi 16 kesi hiyo itakapotajwa.

Mamia wafurika

Kuanzia saa tatu asubuhi, wanachama, wabunge na viongozi mbalimbali wa Chadema walianza kuwasili mahakamani hapo kusubiri kesi hiyo.

Miongoni wa viongozi wa Chadema na Ukawa waliokuwapo ni Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu, Mbunge wa Mikumi, Joseph Haule, Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya, Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko na makada mbalimbali.

Washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo saa 6.30 mchana na ilipofika saa 7.15 mchana, Mdee na wenzake walipandishwa kizimbani katika mahakama ya wazi na kusomewa shtaka hilo.

Wakati huo mahakama hiyo ya wazi ilikuwa imefurika kiasi cha watu wengine kulazimika kusimama mlangoni ili kusikilia kinachoendelea.

Baada ya watuhumiwa kuachiwa kwa dhamana, Mwalimu, Mdee na Waitara walizungumza na wafuasi wao mahakamani hapo.

Mdee alituma ujumbe kwa Rais John Magufuli na Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga kuwa wakiwa polisi waliambiwa kuwa hakuna sababu za kuwaweka ndani, ila wamefanya hivyo kwa maagizo kutoka ngazi ya juu.

Alisema kitendo cha kuwekwa ndani hakitawazuia kufanya kazi zao na pia alilitaka jeshi hilo kufuata taaluma za kazi zao na kuacha kufanya kazi kwa kufuata maagizo.

Mwalimu alisema Serikali isithubutu wala kujidanganya kwamba itawaweka watu wao ndani ili kuitisha mkutano wa uchaguzi wa Jiji la Dar es Salaam.

No comments: