Sumbawanga. Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe amewasimamisha kazi maofisa watano wa misitu akiwamo Kaimu Meneja wa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS), Nyanda za Juu Kusini, Bruno Mallya na Ofisa Maliasili Mkoa wa Rukwa, Nicholas Mchome ili kupisha uchunguzi.
Wengine ni Ofisa wa TFS Wilaya ya Kalambo, Herman Ndanzi, Ofisa Misitu wilaya hiyo, Geofrey Mwasomola na Ofisa Misitu TFS, Kalambo na Sumbawanga, Martin Hamis.
Profesa Maghembe amesema amewasimamisha kazi maofisa hao kwa kushindwa kusimamia na kudhibiti uvunaji haramu wa magogo aina ya mkurungu na kusababisha uharibifu mkubwa katika Msitu wa Kalambo.
“Tutaleta maofisa wengine wanaoweza kulinda rasilimali za Serikali kwa kuwa ninyi mmeshindwa na hamna uchungu wa rasilimali za nchi hii,” amesema.
Profesa Maghembe amefanya ziara ya kushtukiza mkoani Rukwa leo.
Profesa Maghembe ametoa wiki moja TFS kuhakikisha kuwa magogo yaliyovunwa katika msitu huo yanahifadhiwa katika vijiji vya Kasitu, Safu Jengeni na Kaluko.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Magalula Said alisema uvunaji huo haramu umeanza muda mrefu.
Mtendaji Mkuu TFS, Juma Mgoo alisema jitihada zinatakiwa zifanyike kwa maofisa misitu kushirikiana na kamati za ulinzi na usalama ili kulinda maliasili.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment