Mashuhuda wa tukio hilo lililotokea majira ya saa tatu asubuhi, waliokuwa katika mgahawa wa Makitoe, ulioko eneo la Masaki mwisho jijini Dar es Salaam, wameielezea Nipashe walivyoshuhudia tukio hilo kabla ya watu hao wanadaiwa majambazi hajauawa.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, ambaye aliomba hifadhi ya jina lake kwa sababu za usalama, alisema wakati akiendelea na shughuli zake, muda huo huo lilifika gari aina ya Toyota RAV 4, lililopaki upande wa pili wa barabara na watu waliokuwa katika gari hilo kwa zaidi ya nusu saa, hawakushuka.
Alisema kwa muda mfupi walifika watu wawili ambao walikwenda katika gari hilo ili kuwataka waliokuwamo ndani ya kushuka mara moja.
“Nilivyoona wale watu wawili wanawaamrisha waliomo katika gari kufungua vioo na kushuka katika gari, nikagundua kuwa waliokuwa wanawaamrisha ni askari waliovalia kiraia, wakapiga risasi moja hewani, tukahamaki na kuanza kukimbilia ndani,” alisema mhudumu huyo.
Alisema risasi nyingine ilimfikia mtu mmoja aliyekuwapo katika gari na kumfanya kufungua mlango na kukimbilia katika uvungu wa gari hilo, huku wenzake wawili wakikimbilia upande wa pili wa barabara.
”Wale waliokimbia walikimbizwa na kukamatwa ingawa walikuwa wakibishana na askari, lakini waliletwa pale lililopokuwa limepaki gari lao, tukaambiwa raia laleni chini. Mimi na wenzangu tulikimbilia ndani ya mgahawa huo, milio ya risasi iliendelea. Baada ya dakika chache askari wakatutangazia raia endeleeni na shughuli zenu, tumeshawakamata,” alisema shuhuda huyo.
Mashuhuda wengine wa tukio hilo, walidai kuwa watu hao wanaodaiwa ni majambazi, ni raia wa kigeni kutoka Rwanda ama Burundi.
Mama lishe, Sarah Charles, ambaye alikuwa na majeraha katika mkono wake wa kulia baada ya kuangukiwa na watu waliokuwa wanakimbia, alisema alisikia milio ya risasi ikiendelea huku akiwa amejificha hatua chache kutoka eneo la tukio.
“Mkono huu nimechubuka niliangukiwa na watu, baada ya kuona hapa hatuponi, milio ya risasi iliendelea baada ya muda mfupi niliona gari la polisi likija na kupakia maiti tatu za watu na kuondoka nazo,” alisema mama lishe huyo na kuongeza:
“Katika mgahawa ule huwa wanafika watu wenye pesa zao, wanapaki magari, wakinywa supu au chai sana sana majira ya asubuhi,” alisema.
Shuhuda mwingine, Ally Abdallah, alisema baada ya milio ya risasi kusikika watu wawili wakitokea eneo la tukio walikimbilia eneo la mama lishe, huku mmoja wao kiatu kimoja kikimvuka na kukimbilia katika bajaj iliyokuwa jirani.
“Alikimbilia katika bajaji baada ya kukimbizwa na askari nafikiri, kiatu hiki hapa, kilimvuka, akakamatwa na kupelekwa pale katika mgahawa, risasi zikaendelea na kiatu hiki ni moja ya viatu vilivyokuwa vimevaliwa na mtu mmoja ambaye alifariki dunia na kuchukuliwa na gari la polisi,” alisema Abdallah.
Hata hivyo, Kamishna wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro, akizungumzia tukio hilo mbele ya waandishi wa habari, alisema lilitokea jana saa 3:00 asubuhi, wakati marehemu hao ambao ni majambazi wakiwa kwenye gari aina ya RAV 4 ya rangi ya silver yenye namba za usajili T 135 AQJ.
Kamishna Sirro alisema watu hao wanaodaiwa kuwa majambazi waliuawa wakati wanajiandaa kufanya tukio la uhalifu katika moja maduka ya kubadilisha fedha za kigeni lililoko Masaki.
Alisema polisi walipata taarifa za watu hao kupanga kuvamia duka hilo, kwa ajili ya kumvamia mfanyabiashara mmoja maeneo ya hoteli ya Sea Cliff, aliyekuwa anapeleka fedha kwenye duka la kubadilisha fedha za kigeni.
"Baada ya kupata taarifa kutoka kwa wasamaria wema, tulituma askari wetu ambao walikuta majambazi hao wakiwa kwenye harakati za kufanya tukio hilo. Askari walipowaamuru wafungue kioo cha gari, askari walilazimika kuanza kujibishana nao hali iliyosababisha majambazi hao kupoteza maisha, "alisema.
Alisema majambazi wengine waliwili waliokuwa kwenye usafiri wa pikipiki, walifanikiwa kukimbia wakati mashambulizi yakiendelea.
Kamaishna Sirro alisema baada ya kuwaua majambazi hao, walikwenda kukagua na kukuta bastola tatu mbili aina ya Chinese ambazo ni za serikali, zinazotumiwa na polisi na nyingine aina ya Beretta.
Pia alisema walikutwa na hirizi mbili, bomu la kurusha la mkono na karatasi ambalo lilikuwa limeandikwa maneno ya kiaraabu.
Alisema polisi weanaendelea na upelelezi ili kubaini watu hao walikuwa wakitokea wapi na majina yao na kwamba wamejipanga kukabiliana na matukio hayo jijini hapa.
Aidha, alisema mwandishi wa habari, Salma Said, ambaye alitekwa hivi karibuni, ni mzima kutokana na kumkuta hana majeraha lelote katika mwili na kwamba wamechukua maelezo yake, ambayo wanayafanyia kazi kabla ya kuchukua hatua.
SOURCE: NIPASHE
No comments:
Post a Comment